TRA yaandika historia mpya ya makusanyo

Muktasari:
- Yavuka lengo la ukusanyaji kwa mwaka mzima, ikikusanya jumla ya Sh32.2 trilioni, ikiwa ni ufanisi wa asilimia 105, wastani wa ukusanyaji kwa mwezi ukiwa ni Sh2.7 trilioni.
Dar es Salaam. Wakati mwaka mpya wa fedha ukianza leo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imemaliza mwaka wa fedha 2024/2025 kwa mafanikio, ikivuka lengo la makusanyo yake na kuandika historia mpya ya ukusanyaji.
Katika mwaka huo wa fedha, lengo lilikuwa kukusanya Sh31.5 trilioni, ila hadi kufikia Juni 30, makusanyo yalifikia Sh32.2 trilioni, ambayo ni ufanisi wa asilimia 105.
Kiasi hicho ni kikubwa zaidi kuwahi kukusanywa tangu kuanzishwa kwake mwaka 1996, ilipowekewa lengo la kukusanya Sh539 bilioni, lakini hata hivyo, ilikusanya Sh531 bilioni, ikiwa ni wastani wa Sh44 bilioni kwa mwezi.
Akizungumza leo Jumanne, Julai 1, 2025, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda amesema katika mwaka wa fedha ulioshia Juni 30, mamlaka hiyo imeandika historia ya kuvuka lengo la makusanyo kwa miezi yote 12.
Mwenda, aliyeteuliwa katika nafasi hiyo Julai 2, 2024, ikiwa ni siku moja baada ya kuanza kwa mwaka mpya wa fedha, amesema mafanikio hayo ni matokeo ya kuimarika kwa ushirikiano kati ya TRA na walipakodi.
Amesema miongoni mwa maagizo aliyopewa na Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kumteua kwenye nafasi hiyo ni kuhakikisha TRA inaimarisha uhusiano wake na walipakodi, na kupunguza matumizi ya nguvu kwenye ukusanyaji.
“Sasa tunakusanya kodi pamoja, wafanyabiashara wanashiriki kutuonyesha tukakusanye, wanatupa taarifa za wanaotukwamisha. Niwahakikishie, tunapoanza mwaka mpya, tutaendeleza ushirikiano.
“Niahidi tutaendelea kutatua changamoto za wafanyabiashara kwa wakati, pia tutaendelea kusimamia usawa wa ulipaji kodi nchini kwa kuhakikisha kila anayestahili kulipa kodi analipa kwa kiwango kinachostahili,” amesema Mwenda.
Sababu nyingine iliyowezesha kuvuka kwa lengo la ukusanyaji, kwa mujibu wa Mwenda, ni kuongezeka kwa ufanisi wa ndani wa TRA, akieleza kuwa watumishi wamekuwa na ari kubwa kuhakikisha kodi inakusanywa.
Sambamba na hilo, amesema kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na mazingira bora ya ufanyaji biashara nchini kumechangia mamlaka hiyo kukusanya kiasi kikubwa cha mapato.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TRA, Mussa Uledi amesema Rais Samia ameiunga mkono kwa kiasi kikubwa mamlaka hiyo, hali iliyowezesha kufanya vizuri kiutendaji.
“Ametuwezesha kuwa na ufanisi mkubwa kwenye ukusanyaji wa kodi kwa kuwajengea uwezo walipakodi wa namna ya kulipa kodi bila shuruti. Kihistoria, hakukuwa na uhusiano mzuri na walipakodi, lakini ili kupata ufanisi, ni vyema pande hizi mbili zikawa pamoja.
“Rais alituagiza tuwe na mifumo inayorahisisha ulipaji kodi. Tunataka tufikie wakati ambapo mfanyabiashara anaweza kulipa kodi hata akiwa nyumbani kwake. Hata akisema anataka kwenda kumuona ofisa wa TRA ofisini, basi akutane na mazingira mazuri,” amesema Uledi.
Mwenyekiti huyo ametaka TRA kuwa mamlaka bora zaidi ya mapato barani Afrika, ikijilinganisha na mataifa yaliyoendelea duniani.
“Baada ya kuona yanayoendelea duniani, nilipata hofu inaweza kuathiri ukusanyaji wetu, lakini imekuwa tofauti, tumefanya vizuri. Sawa, tumevuka malengo, lakini nguvu hii tuiendeleze katika mwaka huu wa fedha unaoanza leo,” amesema.
Katika mwaka wa fedha 2025/2026, TRA imepewa lengo la kukusanya Sh36 trilioni.
Wasemavyo wadau
Akizungumzia hatua hiyo, Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (Taffa), Edward Urio amesema mawakala wa forodha wataendelea kushirikiana na TRA kuhakikisha ukusanyaji wa kodi unafanyika kwa ufanisi.
“Tunaendelea kuwaahidi ushirikiano. Malengo mliyopewa kwa mwaka ujao tutakuwa pamoja na kushiriki kikamilifu kufanikisha hilo. Tunachotaka ni kodi ilipwe kwa usawa ili Taifa lifanye maendeleo,” amesema Urio.
Mwakilishi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo, Mariam Othman amesema kwa sasa wafanyabiashara hao wanapata ushirikiano mzuri kutoka TRA, hivyo wataendelea kuwa mabalozi wa kodi.
“Sasa hivi sokoni kuna utulivu, hii inasaidia sisi kufanya biashara na kulipa kodi kwa wakati. Kwa hiki kinachoendelea, tutaendelea kutoa ushirikiano na kuhamasishana kulipa kodi,” amesema Mariam.