Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vijana wachimba madini wafundwa

Baadhi ya vijana ambao ni  wachimbaji wadogo wilayani Tarime wakiwa kwenye uzinduzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo kabla ya kuanza uchimbaji baada ya kupewa leseni na serikali.  Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

  • Mradi huo ambao umeelezwa kuwa ni wa kwanza kwa ukubwa nchini na barani Afrika unaohusisha mahusiano mazuri kati ya mgodi na jamii pamoja na kuimarisha uchumi wa vijana unatarajiwa kuwawezesha wachimbaji wadogo kuboresha shughuli zao na kuongeza uzalishaji wenye tija.

Tarime. Vijana zaidi ya 1,700 wilayani Tarime waliopewa leseni kwa ajili ya kuanzisha uchimbaji mdogo wa dhahabu wametakiwa kuweka malengo juu ya nini wanatarajia badala ya kipato watakachokipata kuwa chanzo cha matatizo.

Mei 3, 2025 Serikali ilitoa leseni 96 kwa vikundi 48 vya vijana wanaotoka katika vijiji vinavyozunguka mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uchumi wa vijana na kuwawezesha wachimbaji wadogo kuboresha shughuli zao ili kuongeza uzalishaji wenye tija.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo vijana hao leo Ijumaa Mei 20, 2025, Mkurugenzi wa Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Mroni, Kelvin Mroni amesema uchimbaji wa madini unazo changamoto nyingi ambazo vijana hao wanatakiwa kujipanga na kuweka mikakati ya kupambana nayo ili waweze kupata mafanikio yaliyolengwa.

"Mnatakiwa kutambua thamani ya hizi leseni mlizopewa,sisi wenzenu hatukupata fursa kama hii lakini tumepambana hadi kufika hapa tulipo,zipo changamoto nyingi hasa pale mtakapoanza kupata faida msiruhusu anasa ziwatoe kwenye malengo," amesema.

Amesema vijana hao wakitumia sekta ya dhahabu vizuri upo uwezekano mkubwa wa wao kuwa mabilionea kwani dhahabu ni moja ya njia kuu zinazotumika kuinua uchumi wa dunia hivyo kinachopaswa kufanyika ni matumizi sahihi ya fursa hiyo.

Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka amesema serikali imeamua kutoa mafunzo hayo kwa vijana hao ili waweze kuwa na uwezo wa kufanya shughuli hizo kwa ufanisi.

Amesema vijana hao kupewa leseni hizo ni moja ya mikakati ya serikali kuhakikisha kuwa changamoto ya ukosefu wa ajira iliyokuwa ikisababisha vijana wengi kuvamia mgodi inapata ufumbuzi wa kudumua.

Chikoka amewataka vijana hao kufanya shughuli zao kwa ushirikiano na kuepuka migogoro ambayo inaweza kuwa chanzo cha kuvunjika kwa vikundi hivyo na kusababisha lengo la serikali kushindwa kutimia.

"Leseni hizi zimetolewa tukitarajia vijana wa hapa mtainuka kiuchumi hivyo kati ya vitu ambavyo mnatakiwa kuvuepuka ni migogoro kwani penye migogoro kamwe hakuna maendeleo wala ustawi, serikali ina imani kubwa sana na nyie kwahiyo msiiangushe," amesema Chikoka

Ofisa Madini Mkoa wa Mara, Amini Msuya amesema mafunzo hayo yanayotarajiwa kufanyika kwa muda ws siku 14 ni moja ya sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kuwawezesha wachimbaji wa madini vijana nchini.
Amesema washiriki wa mafunzo hayo pamoja na mambo mengine watafundishwa kuhusu usalama mahala pa kazi, matumizi sahihi ya fedha, utunzaji wa mazingira sambamba na uchimbaji wa kisasa.
Amesema baada ya mafunzo vijana hao wataanza kuonyeshwa maeneo yao ya kuchimba ambayo yapo katika wilaya za Tarime, Serengeti na Butiama ili waanze rasmi uchimbaji kama ambavyo imekusudiwa.

Meneja Mahusiano wa Barrick North Mara, Francis Uhadi amesema mgodi wake umewezesha kufanyika kwa mafunzo hayo kwa wachimbaji hao ili kuhakikisha urasimishaji wa wachimbaji wadogo unakuwa na tija.

"Tunaamini katika elimu,na ili shughuli zao ziweze kuwa na ufanisi tumeona ni vema wakapata mafunzo haya ambayo yatakuwa mwangaza wa shughuli zao wanazotarajia kuanza baadaye," amesema.

Baadhi vijana hao wameishukuru serikali kwa hatua hiyo huku wakiomba mchakato wa kuonyeshwa maeneo ufanyike kwa haraka ili uzalishaji uanze.

Joyce Marwa amesema elimu watakayoipata itawasaidia katika shughuli hizo ili waweze kufanya kazi kulingana na maendeleo ya teknolojia.

"Wengi wetu hatuna elimu kabisa kuhusu haya mambo,licha ya kuwa tunafurahi kumiliki leseni lakini tulikuwa tunawaza tunaanzaje ila sasa serikali imekuja na majibu tunaimani baada ya mafunzo tutakuwa tumeiva," amesema Mkono John.