Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waagizaji mafuta watoa angalizo licha ya ruzuku kwa dizeli

Muktasari:

  • Bei za mafuta ya petroli imeshuka wa Sh29 kwa Dar es Salaam hadi Sh4, 086 kutoka Sh4, 115 wakati dizeli imepanda kwa Sh85 baada ya kuwekewa ruzuku ya Sh534 kwa lita.

Dar es Salaam. Wakati Tanzania inaonekana kuwa miongoni mwa nchi zenye bei ndogo ya mafuta, Chama cha Waagizaji wa Mafuta Tanzania (Taomac) kimewataka Watanzania kuendelea kufunga mkanda kwani bei zitaendelea kuwa juu.

Kimesema ni ngumu kuona ahueni kwa sasa kwa kuwa shinikizo la bei katika soko la dunia bado linaendelea, kutokana na sababu zilizochochea hali hiyo kuwapo.

Takwimu zinaonyesha bei ya petroli Tanzania ni Sh4, 086 kwa lita, ikiwa chini ya Kenya inakouzwa Sh4,339; Uganda Sh4,485, Rwanda Sh5,230 na Malawi Sh9,314 kwa lita.

Kwa upande wa dizeli ambayo kwa Tanzania inauzwa Sh4,333 kwa lita, nchini Zambia inauzwa Sh4,592, Kenya Sh4,715 na Malawi Sh10,031 kwa lita.

Hii ni baada ya bei za petroli nchini kushuka wa Sh29 kwa mafuta yaliyoingilia Bandari ya Dar es Salaam, kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura). Sasa itakuwa Sh4,086 kutoka Sh4,115 huku dizeli ikipanda kwa Sh85 licha  ya kuwekewa ruzuku ya Sh534 kwa lita.

Baada ya ruzuku hiyo, dizeli kwa mafuta yanayopita Bandari ya Dar es Salaam itauzwa Sh4,333 kutoka Sh4,248 iliyokuwapo Mei 2026 kuanzia Juni 3 mwaka huu.

Taarifa ya Ewura iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Gerald Maganga imeeleza mabadiliko ya bei za mafuta nchini kwa Juni 2026 kuwa yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati tangu Februari 28, 2026, vikihusisha nchi za Marekani, Israeli na Iran.

Maganga amesema kwa kuwa Tanzania inaagiza sehemu kubwa ya mafuta yake kutoka nchi za Mashariki ya Kati na athari za mabadiliko hayo zimejitokeza moja kwa moja katika soko la ndani.

"Miongoni mwa hatua hizo ni utoaji wa ruzuku ya takriban Sh534.91 kwa kila lita moja ya dizeli ambayo ni muhimu katika shughuli za kiuchumi na kijamii, zikiwemo uzalishaji viwandani, usafirishaji wa bidhaa na huduma za usafiri wa umma," amesema.

Kwa upande wa mafuta ya taa yanayopita Bandari ya Dar es Salaam yatanunuliwa kwa Sh4, 685 kutoka Sh4,677 Mei mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la Sh8.

Kwa upande wa watumiaji wa petroli inayopitia katika Bandari ya Tanga, lita moja itauzwa kwa Sh4,157 kutoka Sh4,176 ikiwa ni ongezeko la Sh19 kwa kila lita.

Wanaotumia mafuta ya dizeli yanayopita katika bandari hiyo sasa watanunua lita moja kwa Sh4, 404 kutoka Sh4,309 ikiwa ni ongezeko la Sh95 kwa lita.

Akizungumzia mwenendo wa bei za mafuta, Mwenyekiti wa Chama cha Waagizaji wa Mafuta Tanzania (Taomac), Raphael Mgaya amesema hakuna dalili za haraka za kushuka kwa bei kutokana na sababu zilizochochea ongezeko hilo kuendelea kuwapo.

Mgaya amesema mvutano unaoendelea kati ya Marekani na Iran pamoja na mashambulizi dhidi ya miundombinu ya mafuta katika Mashariki ya Kati bado unaendelea kuathiri soko la mafuta duniani.

“Vihatarishi vilivyosababisha bei kupanda bado vipo pale pale. Marekani na Iran bado wanaendelea na mvutano na mashambulizi dhidi ya miundombinu ya mafuta yanaendelea. Kwa hiyo hali bado ni tete na bei katika soko la dunia bado ziko juu,” amesema.

Ameeleza kuwa bei zinazoonekana katika soko la dunia kwa sasa ndizo zitakazokuwa msingi wa mafuta yatakayoingia nchini katika miezi ijayo kutokana na mzunguko wa biashara ya mafuta.

“Bei zilizopo sasa duniani ndizo zitakazoathiri mafuta yatakayouzwa katika miezi inayofuata. Kwa hali ilivyo sasa tunatarajia bei kuendelea kubaki juu kwa sababu mazingira ya soko bado hayajatengamaa,” amesema.

Kwa mujibu wa Mgaya, hata vipindi ambavyo kulikuwa na taarifa za kusitishwa kwa mapigano kwa muda mfupi, havikuweza kuleta nafuu katika bei za mafuta kwa sababu hali ya kutokuwa na uhakika iliendelea kutawala soko.

“Tatizo ni kwamba mapigano yanaweza kusimama kwa wiki moja na baadaye kuanza tena. Hivyo, pamoja na kuwepo kwa vipindi vya utulivu wa muda mfupi, bado kulikuwa na sintofahamu kubwa kuhusu hatima ya mgogoro huo, jambo ambalo liliendelea kushikilia bei katika viwango vya juu,” amesema.

Ameongeza kuwa bei za mafuta hazipangwi kwa kuzingatia mabadiliko ya siku moja katika soko la dunia, bali hutegemea wastani wa bei za kipindi kizima cha mwezi.

“Huwezi kuona leo Marekani na Iran wametangaza kusitisha mapigano na kesho ukategemea bei ishuke moja kwa moja, pia wakati wa kukokotoa bei kinachoangaliwa ni wastani wa bei za mwezi mzima kwa sababu mafuta yanaagizwa kwa nyakati tofauti ndani ya mwezi huo.

“Ndiyo maana mabadiliko ya muda mfupi mara nyingi hayaonekani moja kwa moja katika bei za mwisho kwa watumiaji,” amesema.