Wajasiriamali wanawake wapewa mbinu kuvutia wateja kuelekea maonyesho ya Sabasaba
Mwenyekiti wa Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF), Anna Mkapa akizungumza wakati wa mafunzo ya wajasiriamali wanawake takribani 250 yaliyofanyika leo Juni 23, 2026 jijini Dar es Salaam
Muktasari:
- Wajasiriamali wanawake nchini wamepewa mbinu za kuvutia na kudumisha mahusiano mazuri na wateja kuelekea maonyesho ya Sabasaba wakihimizwa kuzingatia uaminifu, uvumilivu, ukweli na weledi katika huduma kwa wateja.
Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku nne kuelekea ufunguzi wa maonyesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), wajasiriamali na wafanyabishara nchini wametakiwa kuzingatia misingi ya huduma bora kwa wateja ikiwemo uaminifu, uvumilivu, ukweli na weledi ili kuongeza mauzo na kujenga mahusiano ya kudumu na wanunuzi.
Wito huo umetolewa leo Juni 23, 2026 na Ofisa Biashara Mwandamizi wa TanTrade, Beatrice Nahoyo wakati wa mafunzo kwa wanawake wajasiriamali yaliyoandaliwa na Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF) na kufanyika jijini Dar es Salaam.
Akitoa mada wakati wa mafunzo hayo, Nahoyo amesema mafanikio ya biashara hayategemei ubora wa bidhaa pekee, bali namna mjasiriamali anavyowahudumia na kuwajali wateja wake.
Nahoyo amesema miongoni mwa mambo muhimu yanayoweza kumshawishi mteja kununua bidhaa ni uwezo wa mfanyabiashara kuwa mchangamfu, kumsikiliza kwa makini na kujibu maswali yake kwa usahihi.
“Mteja anapokuja kuuliza kuhusu bidhaa yako, hakikisha unamsikiliza kwa umakini na kumpa majibu sahihi. Hilo linamjengea imani na kumfanya awe tayari kununua bidhaa au huduma unayotoa,” amesema Nahoyo.
Ameeleza uaminifu ni nguzo muhimu katika biashara, akiwataka wafanyabiashara kuepuka kutoa taarifa za kupotosha kuhusu bidhaa zao kwa lengo la kupata mauzo ya haraka.
Kwa mujibu wake, baadhi ya wafanyabiashara huwashawishi wateja kununua bidhaa zao kwa kuwaambia zinadumu kwa muda mrefu au kuwa na uwezo mkubwa kuliko uhalisia wake, jambo ambalo huwasababisha kupoteza wateja pindi matarajio yao yanaposhindwa kutimia.
“Usimwambie mteja kitu ambacho si kweli. Kama bidhaa ina uwezo fulani, eleza ukweli wake. Mteja akigundua ulimdanganya, utapoteza uaminifu wake na huenda asirudi tena,” amesema.
Nahoyo amesema uvumilivu ni sifa nyingine inayopaswa kuzingatiwa hasa wakati wa maonesho ambapo wafanyabiashara hukutana na wateja wa aina mbalimbali wenye mahitaji na maswali tofauti.
“Wapo wateja wanaouliza maswali mengi sana kiasi cha kukukera, lakini mfanyabiashara mzuri anatakiwa kuwa mvumilivu. Msikilize na mjibu kwa utulivu kwa sababu kila mteja ni fursa ya biashara,” amesema.
Amesisitiza pia umuhimu wa weledi katika utoaji wa huduma, akieleza kuwa wafanyakazi wote wanaosimamia mabanda ya biashara wanapaswa kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu bidhaa au huduma zinazotolewa.
Amesema si jambo la busara mteja kuuliza kuhusu bidhaa na kukosa majibu kwa sababu mhudumu aliyepo hana taarifa sahihi au analazimika kumpigia simu mwenye biashara.
“Ikiwa umeajiri watu wa kusimamia biashara yako, hakikisha wanafahamu vizuri bidhaa au huduma unayotoa. Mteja akija na kukosa maelezo sahihi unaweza kumpoteza kwa sababu muda wake ni muhimu,” amesema.
Pia amewasisitiza ni muhimu kushughulikia malalamiko ya wateja bila kumkatisha wakati akieleza changamoto yake na kuomba radhi ambapo huduma au bidhaa imesababisha usumbufu na kisha kutafuta suluhisho la haraka ili kuimarisha uhusiano na kuongeza uwezekano wa kurejea tena kufanya biashara.
“Msikilize mteja hadi amalize kueleza malalamiko yake. Usimkatize. Hilo litakusaidia kuelewa tatizo na kutafuta njia ya kulitatua,” amesema.
Meneja Rasilimali Watu kutoka GS1 Tanzania, Marie Kigalu amewahimiza wanawake wajasiriamali nchini kutumia mafunzo ya ujasiriamali na teknolojia ya kidijitali kama nyenzo ya kuongeza ushindani wa biashara zao, kupanua masoko na kuimarisha kipato chao katika mazingira ya biashara yanayobadilika kwa kasi.
“Biashara za mtandaoni kwa sasa zina fursa kubwa sana. Ni muhimu mkazingatia mafunzo haya, msikilize wataalamu wa mada na kuuliza pale ambapo hamjaelewa ili muweze kunufaika kikamilifu,” alisema.
Mwenyekiti wa Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF), Anna Mkapa amesema mfuko huo umekuwa ukitoa mafunzo kwa wajasiriamali kila mwaka kwa takribani miaka 28 mfululizo.
Anna amesema hadi sasa tayari mafunzo hayo yamenufaisha wajasiriamali takribani 7300 kutoka maeneo mbalimbali nchini ambao wamefanikiwa kuuza bidhaa zenye thamani ya takribani Trilioni 1.8.
“Mafunzo ya mwaka huu yamewakutanisha wanawake 250 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, wengi wao wakitoka maeneo ya pembezoni,”amesema.