Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanachovuna madereva, makondakta wa daladala

Madereva wa daladala, Mussa Kizu (kulia) na Omar Maswa (katikati) wakizungumza na mwandishi wa Gazeti la Mwananchi, Exuperius Kachenje, Dar es Salaam jana.

Muktasari:

Kila mmoja anaingiza wastani wa Sh900,000 kwa mwezi, hiyo ni mbali na matumizi mengine ikiwamo Sh20,000 wanazotenga kila siku ‘kuzima matatizo ya trafiki barabarani’

Dar es Salaam. Wakati jana Taifa lilishuhudia mgomo wa madereva wanaodai mambo mbalimbali ikiwamo mikataba ya ajira na mshahara wa Sh250,000 kwa mwezi na kupinga kwenda kwa mara nyingine katika shule ya udereva, imebainika kuwa wengi wao hasa wa daladala, huingiza kati ya Sh900,000 hadi Sh1,050,000 kwa mwezi.

Gazeti hili limebaini kuwa kiasi kama hicho hupata pia makondakta wa mabasi hayo baada ya kugawana walichopata na madereva wao.

Hata hivyo, viwango hivyo hutofautiana kutokana na njia wanazotoa huduma, aina ya magari wanayoendesha, uamuzi wa dereva, hata hali ya hewa ya siku husika na idadi ya kukamatwa na askari wa usalama barabarani.

Uchunguzi unaonyesha kuwa madereva na makondakta hao kila siku, baada ya kutenga ‘hesabu’ ya tajiri ambayo ni kati ya Sh100,000 na 150,000, hubakiwa na kati ya Sh80,000 hadi Sh160,000 baada ya kazi ya siku nzima na hugawana kati ya Sh40,000 hadi Sh80,000 na kiasi kingine hununulia dizeli kwa ajili ya kufanyia kazi siku inayofuata. Mabasi mengi yanatumia kati ya Sh60,000 hadi 100,000.

“Inategemea, kwa siku unaweza kupata Sh260,00, au hata Sh280,000. Kwa mfano, mimi tajiri pesa yake kila siku ni Sh100,000. Kinachobaki hapo ndicho cha mafuta.

Pia hutegemea aina ya gari, dereva na konda mgawo wenu hutegemea kinachobaki,” anaeleza dereva wa daladala, Maswa Omari (38) wa Dar es Salaam. Anaongeza kuwa kwa wastani, kwa siku hubakiwa na Sh70,000 ambazo hugawana sawa na kondakta wake hivyo kila mmoja huambulia Sh35,000.

“Lakini fedha hizo ni nje ya kuwalipa ‘deiwaka’. Unapompa dereva mwenzio ‘deiwaka’ inategemea uhusiano wenu, ingawa kwa kawaida hulipwa Sh4,000 kwa kila safari,” anasema Omari aliyeeleza kuwa alianza kazi ya udereva miaka ya 1990.

“Kwa madereva na makondakta wa daladala, chai ni matumizi nje ya posho, chakula cha mchana, maji, sigara haviingizwi kwenye hesabu ya siku. Hayo ni matumizi ya kawaida, mtu anaweza kunywa hata soda tatu kwa siku, akienda hotelini anakula anachotaka kwa gharama yoyote.

 Ndiyo sababu ukiingia kwenye hoteli nyingi za mjini ni rahisi kumjua kondakta au dereva wa daladala kwani huagiza tofauti na watu wa kawaida,” anasema Omari.

Dereva mwingine, Njila Shabani anasema fedha wanazopata kumlipa tajiri na wao kujilipa kwa siku ni nje ya zile zinazotumika kuwalipa wapiga debe kwenye vituo, kulipia faini kwa askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani (trafiki) pamoja na ile ya kula wake na kondakta wake.

“Mwanzo wa safari tunawalipa wapiga debe Sh400 kwa kila safari. Kila kituo tukipakia abiria tunatoa Sh200 au 300 kwa wapigadebe, hata kwa trafiki kwa siku tunatozwa faini ya Sh30,000 ni ngumu kukwepa, kama siyo faini halali, basi unaweza kujituka umetumia hata Sh20,000 kwa siku kutoa kwa askari,” anasema Shabani anayeendesha gari linalofanya safari zake kati ya Gongo la Mboto na Makumbusho.

Akizungumzia suala la mikataba ya kazi, Omari anasema wengi wao wana mikataba bandia, waliyotia saini ili kuwawezesha wamiliki wa daladala kupata vibali vya kuendesha biashara hiyo.

“Ni mikataba hewa kwani ni kwa ajili ya kumsaidia tajiri. Mimi nina mkataba lakini sijawahi kulipwa mshahara, lakini utafanyaje? Ni lazima uridhike kwa sababu ndiyo hali halisi,” anasema na kuongeza:

“Kima cha chini cha makubaliano ya mshahara kwenye mikataba mingi ni Sh150,000 lakini hatupewi, huwezi ‘kusevu’ pesa , lakini akili kichwani mwako. Kwa kazi hii isiyo na mshahara, tunaishi nyumba za kupanga hapa Ilala, vyumba Sh60,000 na watoto wanakwenda shule kwa ada ya Sh600,000 kwa mwaka.”

Dereva wa daladala ya Buguruni kwenda Makumbusho kupitia Barabara ya Uhuru, Mussa Kizu anasema anao mkataba na mwajiri wake. Analipwa Sh250,000 kwa mwezi ingawa wapo madereva wengine ambao hawalipwi mishahara.

“Matatizo mengi yapo kwa madereva, ingawa ni waajiri wachache wanaolipa mishahara kwa wakati. Wengi wana mikataba na mishahara hawapewi,” anasema Kizu mwenye uzoefu wa miaka minne akiwa dereva wa daladala Dar es Salaam.

Anasema makubaliano yake na mwajiri ni kuwasilisha Sh100,000 kila siku na kwamba hufanikiwa kubaki na kiasi cha Sh35,000 kwa siku aliyosema inaweza kuzidi au kupungua kutegemea siku.

“Inaweza kutokea ukarudi nyumbani na Sh2,000 au 3,000 kwa kuwa kuna matatizo kadhaa njiani. Kuna trafiki anaweza kukukamata na kukutoza faini, hapo sasa ni bora kosa liwe la gari bosi atakuelewa, tatizo umetanua au una makosa ya kutovaa sare, hapo utatoa fedha na mwishowe hesabu inapungua. Inawabidi fedha ambayo mngegawana na kondakta wako, iingie kwenye pato la siku la kuwasilisha kwa mwajiri,” anasema Kizu.

Hata hivyo, anasema trafiki wengi wamekuwa wakichukua fedha hata mara nne kwa siku kutoka kwao hali inayofanya waone kazi yao ngumu.

“Wakati mwingine tunakamatwa na kutozwa faini za hapa na pale. Kwa kawaida kila siku huwa tunatenga Sh20,000 kwa ajili ya trafiki njiani na hii fedha lazima itumike.”

Kizu mwenye mke na mtoto mmoja, anasema maisha ni magumu kwa madereva wengi kutokana na kukosekana kwa mikataba inayowatosheleza, ingawa mwajiri wake humwezesha katika matibabu, maendeleo na kumuunga mkono anapotaka kufanya jambo kwa ajili ya familia yake.

“Masilahi madogo na mikataba hewa isiyo na mishahara, hili ndilo tatizo linalozaa mengine mengi yanayojitokeza kila siku. Dereva ana mawazo familia yake inakufa njaa,” anasema.

Anasema mgogoro uliopo ambao pia ndiyo sababu ya mgomo wao siyo wa kushinikizwa, bali waliamua kutokana na suala lililojitokeza la kutaka warudi darasani kila wanapoomba leseni mpya za udereva.

“Mgomo wa kwanza ambao ulihusisha mabasi ya mikoani haukutuhusu, lakini huu wa pili unatuhusu na si kwamba tumeshinikizwa. Suala la kurudi darasani mwezi mmoja na kulipia Sh561,000 linanihusu na mimi,” anasema na kutoa wito kwa Serikali kuwa makini na kutafakari kabla ya kutoa uamuzi ambao huathiri wananchi na Taifa.

“’Hizi ajali zinazotokea barabarani siyo kwamba madereva wote wanazisababisha ni wachache ambao wanafanya hivyo kutokana na matatizo ya kutofuata sheria za barabarani, kama imebainika kwamba dereva amefanya tatizo apelekwe mahakamani, sheria zifanye kazi na si miswada ya kila siku wakati tuna Katiba na sheria za kutuongoza.”

Kizu anapendekeza kuwapo kwa semina za mara kwa mara kwa madereva zitakazochukua muda mfupi, ili kuwawezesha kupata elimu na pia kujua wajibu wao wawapo barabarani sanjari na kukumbushwa sheria za barabarani badala ya kurudi darasani kwa siku 30.

Kauli hiyo ya Kizu inaungwa mkono na Omari anayesema: “Mgomo ni sahihi, ni kweli yanayodaiwa na madereva kuhusu ajira na mikataba bora ya kazi. Huwezi kutoka Bukoba au Kigoma basi likiwa na dereva mmoja, hiyo ni hatari, ndiyo sababu wanapiga ‘overtake’ hata kwenye milima au kona kama tulivyoona picha kwenye gazeti la Mwananchi.”