Wateja wakosa taarifa za benki, wataka amana zao

Dar es Salaam. Kutokana na kukosa taarifa za kina kuhusu hatima ya amana zao, wateja wa Benki ya Yetu Microfinance wameunda kamati kufuatilia uwekezaji walioufanya ndani ya taasisi hiyo ya fedha iliyowekwa chini ya uangalizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa siku 120.

Kamati hiyo ya watu watano, inawawakilisha zaidi ya wateja 80 waliojitokeza Machi 13 kwenye tawi la benki hiyo lililopo Mbagala jijini Dar es Salaam, kutaka taarifa za kina baada ya kumalizika kwa siku 90 za mwanzo ambazo BoT ilikuwa ikiisimamia Benki ya Yetu Microfinance kabla ya kuongeza siku nyingine 30 kabla ya kutoa taarifa kamili kuhusu mustakabali wake.

Mwenyekiti msaidizi wa kamati ya ufuatiliaji wa amana hizo, Stewart Dyamvunye amesema wanachodai ni amana zao, kwani tangu benki hiyo iwekwe chini ya uangalizi hawapati mrejesho wowote.

“Wangekuwa wanafanya juhudi wawasiliane na sisi hata kupitia kwa maofisa wa Benki ya Yetu, lakini hakifanyiki chochote, tunapata wasiwasi wa uslama wa amana zetu,” amesema Dyamvunye.

Matarajio yao anasema yalikuwa kupata taarifa zinazotoa mwelekeo wa namna wanavyoweza kupata amana zao kila tarehe ya mwisho iliyowekwa na BoT inapofika, lakini imekuwa kinyume chake, ndiyo maana waliamua kumpeleka Kituo cha Polisi Maturubai meneja wa benki hiyo tawi la Mbagala.

BoT iliiweka Yetu chini ya uangalizi wake kutokana na upungufu wa mtaji na ukwasi ili kulinda masilahi na haki za wateja pamoja na wadau wengine, wakiwamo wanahisa.

Kutokana na kukosa imani ya upatikanaji wa fedha zao, wateja hao wameandika barua wanayotarajia kuiwasilisha kwa mkuu wa Wilaya ya Temeke na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya hiyo ili wasaidiwe.

Hata hivyo, juzi Taasisi ya Taaluma ya Benki Tanzania (TIOB) iliwatoa wasiwasi wateja taasisi za fedha, ikiwamo Benki ya Yetu Microfinance kutokuwa na wasiwasi, kwani amana zao ziko salama zikisimamiwa na BoT.

Mkurugenzi Mtendaji wa TIOB, Patrick Mususa alitoa kauli hiyo kwenye sherehe ya kutimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo na akasisitiza kwamba “Benki Kuu ipo kwa ajili ya kulinda usalama wa wananchi, tuamini benki zinaaminika katika utendaji wake na ndiyo sehemu salama kuweka amana, kuchukua mikopo na kufanya miamala ya kununua bidhaa ndani na nje ya nchi.”

Akizungumzia kauli hiyo, Stewart alisema “Benki ya Yetu Microfinance hawaongei na sisi, suala hili linatupa wasiwasi. Inaonekana ni jambo ambalo halina kanuni ndani yake, ndiyo maana tunapata wasiwasi.”

Alisema zipo fununu kuwa benki hiyo inatafutiwa mwekezaji mwingine wa kuiendesha au kuunganishwa na benki nyingine, hivyo akabainisha kwamba wao wanachohitaji ni fedha zao ili waendelee na mipango yao binafsi.

“Tunachohitaji ni fedha zetu, hawako makini, kila mtu apewe cha kwake, mchakato wa kutafuta mtu mwingine wa kuiendesha hii benki utachukua muda na sisi tunahitaji kujikwamua kiuchumi,” amesisitiza Dyamvunye.