Waziri Mkuu Majaliwa aagiza vifungashio bidhaa kuandikwa Kiswahili

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Dar es Salaam. Serikali imeagiza kampuni zote zinazozalisha bidhaa hapa nchini kuhakikisha vifungashio vyake vinakuwa na maelezo kwa lugha ya Kiswahili pamoja na bidhaa zote zinazoingia nchini.
Akizungumza wakati wa hafla ya utoaji Tuzo za Safal- Cornell ya Fasihi ya Kiafrika, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza kampuni zote zinazozalisha bidhaa kuhakikisha wanaweka maelezo kwa lugha ya Kiswahili.
Amesema kuwa mbali na hayo pia mamlaka husika zihakikishe mabango mbalimbali ya matangazo barabarani yawe kwa Kiswahili.
Aidha, Waziri Mkuuu Majaliwa ameipongeza Kampuni ya Alaf kutokana na mchango wake kwa kutumia sehemu ya faida kuwekeza kwenye lugha ya Kiswahili.
Amesema ni hatua kubwa kwa Chuo Kikuu cha Dar es salaam kutoa ufadhiri kwa wanafunzi wanaotaka kusoma Kiswahili kutoka nchi za nje.
Miongoni mwa nchi zilizonufaika na ufadhiri huo ni Burundi, Misri, na Italia.
Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mohammed Mchengerwa amesema tuzo hizo za Kiswahili zimekuwa chachu kuhamasisha matumizi ya Kiswahili ndani na nje ya nchi.
Amesema kuwa kupitia tuzo hizo tayari kuna viongozi kwenye kampuni hizo wameanza kujifunza lugha ya Kiswahili.
Hata hivyo amesema licha ya maendeleo hayo, kasi ya uendelezahi Kiswahili haiendani na matwaka ya viongozi wanavyopenda kulingana na changamoto mbalimbali.
Amesisitiza kuwa, “Malengo ya Serikali ni kuisogeza Kiswahili kutoka kuwa lugha ya 10 duniani hadi kufikia nafasi ya pili. Tayari ipo mkakati wa kujenga chuo cha Kiswahili ambapo zimetegwa ekari 100.”
Mkurugenzi Mkuu wa Safal Group, Anders Lindgren ameipongeza Tanzania kuwa ndiyo nchi pekee inayozungumza lugha ya Kiswahili kwa usanifu duniani.
“Tutaendelea kushirikiana na serikali katika kuhakikisha maendeleo ya Kiswahili yanafikiwa,” amesema.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa(Bakita), Consolata Mushi amesema baraza hilo kwa kushirikiana na Baraza la Kiswahili la Zanzibar (Bakiza) wametekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Waziri Mkuu pamoja na Makamu wa Rais.
Amesema miongoni mwa maagizo yaliyotolewa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango wakati wa maadhimisho ya siku ya Kiswahili Duniani, ni pamoja na kubidhaisha Kiswahili, ambapo tayari Kiswahili kinafundishwa kwenye ofisi za ubalozi kama vile China, Korea na Italia.