Tabia hatarishi kwa maisha ya Watanzania;nyingi ni hatari kiafya
Watu wengi wamekuwa wakila bila kufuata maadili ya afya, hivyo kuwafanya baadhi yao kuwa na afya mbaya.Picha ya Maktaba
Muktasari:
- Wapo wanaodhani afya ni kula chakula kingi, kama ni ugali basi uwe mkubwa mithili ya mlima. Ukweli ni kwamba mwili haujengwi na wingi wa chakula kingi tena cha aina moja, bali unajengwa na ulaji wa vyakula vya aina tofauti hata kama ni vichache.Wataalamu wa lishe wanatueleza kuwa kila mlo anaokula mwanadamu unapaswa kuwa mchanganyiko.
Yanaonekana ni mambo ya kawaida, ama ni kwa mazoea au kwa kutojua lakini yana athari kubwa kwa afya na maisha kwa jumla.
Kwa siku kadhaa kuanzia leo, safu hii itaangazia baadhi ya tabia na mienendo ya Watanzania ambayo wataalamu wanasema ni hatari kwa maisha yetu.
Ulaji usiofaa wa vyakula
Watanzania wengi tunakosea kula kwa kutozingatia kanuni za ulaji bora. Kwa mfano, mtaalamu wa lishe, Pazi Mwinyimvua anasema kuwa ulaji bora ni ule unaozingatia kanuni kadhaa muhimu kama vile kula kwa kiasi, kula vyakula vya asili, kula kwa wakati uleule kila siku, kula mboga za majani, kuepuka kula vyakula vya kukaanga mara kwa mara, kupunguza matumizi ya chumvi na sukari katika vyakula na kunywa maji ya kutosha.
“ Ulaji bora pia ni pamoja na mtu kuwa na tahadhari juu ya unywaji wa pombe, soda na juisi za viwandani, chai, kahawa na uvutaji sigara, anasema na kuongeza kuwa ulaji wa vyakula hivi huchangia watu kupatwa na maradhi ya Kisukari. Kuhusu unywaji wa maji, wengi hatunywi maji kiasi kinachotakiwa kwa mujibu wa matakwa ya kilishe. ‘’ Kunywa maji ya kutosha kuna manufaa mengi ikiwamo kuuwezesha mwili kufanya kazi barabara, kukua vizuri, kusaga chakula vizuri, kujikinga na maradhi, kupoza mwili, mwili kutoa sumu mwilini hasa kwa njia ya mkojo...’’ anaongeza kutaja umuhimu wa kunywa maji.
Kwa wale wanaokunywa maji nao wanakosea kwa kufanya hivyo punde tu baada ya kula. Wanalishe wanatueleza kuwa muda mwafaka wa kunywa maji ni kabla ya kula au nusu saa baada ya kula chakula.
Ama unywaji wa maji baridi ambao hupendelewa na watu wengi, nao sio tabia ya kuiendekeza kama anavyosema Dk Samuel Shitta: ‘’ Maji baridi kama ukinywa sana yana madhara machache kama vile kupata vikohozi na vidonda ya koo. Pia maji baridi hasa baada ya kumaliza kula kama wanavyofanya watu wengi kunachangia kugandisha mafuta ya chakula ulichokula, hivyo kulifanya zoezi la usagishaji chakula kuwa taratibu mno.
Wataalamu wanasema hali hiyo inaweza kumsababishia mtu kukosa choo, na kuwa kama tabia itakuwa endelevu upo uwezekano wa mnywaji baadaye kupata saratani ya utumbo, ugonjwa wa moyo na mwishowe kifo.
Kuhusu kipimo cha matumizi ya maji kwa siku na muda wa kunywa, mwandishi na mtaalamu wa mazoezi ya viungo, Fredy Macha anasema mwanadamu anapaswa kunywa bilauri, glasi au vikombe nane vya maji kila siku.
“ Maji hayo usinywe tu wakati wa kula au yote kwa wakati mmoja, yasambazwe katikati ya siku kwa kunywa unapoamka, kabla ya kula, nusu saa baada ya kula. Unapokunywa maji ya kutosha unalipumzisha ini na kulisaidia kuchuja, kusafisha uchafu, takataka’’anasema.
Kula chakula kingi kupita kiasi
Aidha, wapo wanaodhani afya ni kula chakula kingi, kama ni ugali basi uwe mkubwa mithili ya mlima. Mwili haujengwi na wingi wa chakula kingi tena cha aina moja, bali unajengwa na ulaji wa vyakula vya aina mbalimbali hata kama ni vichache.
Huu ndio mlo kamili maarufu Kiingereza kwa jina la Balanced Diet. Wataalamu wa lishe wanatueleza kuwa kila mlo anaokula mwanadamu unapaswa kuhusisha mafungu ya vyakula ambayo ni wanga, protini, vitamin, nyuzinyuzi, madini, mafuta na maji ya kunywa.
Athari ya ulaji wa chakula kingi anaitaja mwanalishe Pazi kwa kusema: “ Kuweka chakula kingi katika sahani kunamfanya mtu kushindwa kudhibiti mhemko wake wa kula sana, kwa hiyo sio ulaji bora… hivyo huchangia kwa haraka safari ya kupata maradhi ya kisukari.’’ Aidha, upo utaratibu mbovu kwa watu wengi kupenda kula aina moja ya chakula katika muda fulani siku zote. Kwa mfano, Watanzania wengi wana mazoea ya kula ugali mchana na wali nyakati za usiku.
Kilishe kuna vyakula kedekede vinavyofanya kazi sawa na ugali kama vile viazi, mihogo, ndizi na vyakula vingine jamii ya nafaka.
Hata ulaji wa mbogamboga nao ni tatizo kwa watu wengi. Mboga za majani zinanasibishwa na hali duni ya kipato, ni chakula cha wasionacho. Wenye nacho wanakula nyama. Huu ni mtazamo tenge kuhusu ulaji wa vyakula vya mbogamboga, ambavyo wataalamu wanatueleza kuwa ni muhimu kwa uimara wa afya zetu.
Kutopenda kula ugali wa dona
Mazoea mengine ni kwa walaji wa ugali. Walaji wengi hawataki kula unga usiokobolewa, maarufu kwa jina la dona. Wanapenda ugali uliokobolewa ambao kimsingi hauna virutubisho vingi kama ugali wa dona.
Japo kila aina ya unga wa ugali una faida na hasara zake, wataalamu wengi wanashauri matumizi ya unga wa dona hata kama unaonekana mbaya katika macho ya walio wengi.
‘’Kwa mtu anaweza kutumia unga usiokobolewa (dona) ni muhimu kwake kufanya hivyo kwa sababu faida zake ni nyingi... unga usiokobolewa una kiasi kikubwa cha mafuta, protini, madini, vitamini, na nyuzinyuzi (fibre), kwa hiyo, unaimarisha zaidi lishe ya mlaji, ‘’anashauri Pazi.
Vyakula vya kufungasha
Kuna vyakula maarufu Kiingereza kwa jina la ‘Fast Food.’ Watanzania wengi hasa vijana mijini ni waathirika wa tabia ya ulaji wa vyakula hivi hatarishi. Vyakula hivi ni kama viazi vya kukaanga (chips), kuku wa kukaanga, keki, pizza na biskuti.
Ukweli ni kwamba uvivu wa kupika na ulimbukeni unawafanya vijana wengi kutonunua vyakula halisi. Wanataka vyakula vya haraka haraka vilivyotengenezwa tayari bila ya kujali afya zao.
Madhara ya kutopenda kupika ni kuwepo kwa idadi kubwa ya vijana, wakiwemo wanawake wasiojua kupika hata mapishi mepesi . Ziko ndoa zinazovunjika kwa kuwa mke hajui kupika hata wali wa maji!
Ulaji mwingi wa nyama
Ulaji mwingine hatari ni ule unaohusu nyama hasa kuku wa kisasa, tabia iliyowakumba watu wengi mijini. Kimsingi wataalamu wanasema nyama (ukiondoa ya samaki) sio nzuri kwa afya zetu.
Kwa mfano, Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Saratani linasema nyama zina kemikali aina ya Amino ambazo ni chanzo cha maradhi ya saratani.
...walaji wa nyama wa kila mara wanajiweka katika hatari ya kupatwa na ugonjwa wa saratani ya matiti na figo. Utafiti mwingine uliofanyika Chuo Kikuu cha Harvard cha nchini Marekani, ulibainisha ya kwamba walaji wakubwa wa nyama ya ng’ombe, kondoo, mbuzi, na nguruwe, wako katika hatari ya kukumbwa na ugonjwa wa saratani ya matiti hasa wanawake, ‘’anasema Esbon Kagya akinukuliwa na gazeti la Rai la Oktoba 4 2012.
Kuna kasumba pia ya baadhi ya watu kwenda kununua vyakula katika maduka makubwa (super market) licha ya ukweli kuwa vyakula halisi vinapatikana katika masoko ya kawaida.
Wapo wanaofikiri kwenda katika maduka haya na kununua bidhaa zilizofungashwa ndio usasa. Kwa Watanzania wengi bado hatujafikia mazingira ya kununua bidhaa kama vile mboga katika maduka ya aina hii. Kwa nini ukanunue nyanya iliyohifadhiwa mwezi mzima dukani, wakati masoko yamesheheni nyanya kutoka shambani?
Vyakula vya mafuta
Mitaani kuna matumizi makubwa ya vyakula vyenye mafuta mengi hasa yatokanayo na wanyama. Mafuta mengi hasa kwa vyakula vya kukaanga kama vile chips, ni hatari kwa afya kama anavyosema mtaalamu wa Lishe Halima Chamosi kuwa mafuta hayo yana lehemu ambayo ni chanzo cha magonjwa mengi kama vile ugonjwa wa moyo na kibofu.
Ikibidi kutumia mafuta kama kiungo muhimu katika vyakula , Chamosi anashauri matumizi ya mafuta yatokanayo na mimea au nafaka kama vile pamba, alizeti, chikichi na aina nyingine ya mimea.
Uchunguzi wa afya zetu
Kilele cha kupuuzia mambo kwa Watanzania kinajionyesha kwa jinsi tunavyodharau kupima hata hali ya afya zetu. Jiulize wewe unayesoma makala haya umeshakwenda kupima afya yako tangu kuanza mwaka huu unaofikia ukingoni?
Kwa kawaida wataalamu wa tiba wanasema tunapaswa kufanya uchunguzi wa afya zetu hata kama tunafikiri hatuna maradhi yanayotusonga. Kiwango kidogo cha upimaji wa afya ni angalau mara moja kwa mwaka.
Unywaji wa vinywaji vyenye kemikali
Soda na juisi za viwandani ni hatari kwa maisha yako. Kuna wanaofikiri unywaji wa soda na juisi za kufungasa ndiyo maisha ya kisasa, kila mlo hawakosi kuwa na moja ya vinywaji hivyo. Hawajui kama wanahatarisha maisha yao kuelekea kupata ugonjwa wa Kisukari.
Mizani madukani
Watanzania wengi wanatumia maduka kununua bidhaa mbalimbali, vikiwamo vyakula, lakini je, maduka hayo ni salama kwa afya zetu? Tuangalie matumizi ya mizani.
Katika maduka mengi kifaa kikubwa cha kupimia ni mizani. Kifaa hicho kinatumika kupima kila bidhaa bila ya kujali usafi na usalama wa kinachopimwa. Maharage, karanga, unga, sukari, vyote vinapimwa kwa kutumia mizani moja.
Kuna uwezekano mkubwa wa mizani kusambaza vijidudu na vimelea vya magonjwa kutoka bidhaa moja hadi nyingine hasa kwa bidhaa zinazoliwa moja kwa moja bila ya kupikwa kama sukari. Katika maduka mengi bidhaa nyingi za nafaka hukaa muda mwingi, huku mazingira ya kuzihifadhi yakiwa hatarishi.
Unywaji pombe na kuvuta sigara
Bila shaka haya ni maradhi ya wengi nchini, licha ya kuwa vitu hivi vimeshathibitika kitaalamu kuwa na athari kwa mwanadamu. Ukweli ni kuwa pombe na sigara havina umuhimu kwa mwanadamu hata kama wapiga debe wake wanatushawishi tuvitumie kwa kivipachika majina ya kuvutia.
Kwa mfano, sigara inayoelezwa kuwa na aina zaidi ya 4000 za kemikali hatarishi kwa binadamu husababisha madhara karibu kila sehemu ya mwili wa mtu.
Mtandao wa Wikipedia wa lugha ya Kiswahili, unataja maeneo 16 yanayoweza kuathirika kwa mtu kutumia sigara.
Baadhi ya maeneo hayo mwilini ni pamoja na moyo (ugonjwa wa moyo), tumbo (vidonda vya tumbo), saratani ya ulimi, saratani ya figo, koo, mfuko wa uzazi na nyinginezo.
Kutojali muda wa matumizi ya bidhaa
Baadhi yetu hatuna tabia ya kuangalia tarehe za ukomo wa matumizi ya bidhaa mbalimbali tunazonunua hasa zile zinazofungashwa.
Wauzaji hawana habari na hata wanunuzi hatutaki kujali usalama wa bidhaa kwa kujua kipindi cha ukomo wa matumizi yake. Uzoefu unonyesha maduka mengi yanauza bidhaa nyingi zilizopitwa na wakati.
Tujenge tabia ya kujua muda wa matumizi ya bidhaa, na tuachane na bidhaa zisizokuwa na maelezo ya muda wa matumizi yake hata kama zinapendeza machoni.
Kusafisha haja kwa karatasi
Kwa nini ujisafishe kwa kutumia karatasi unapokwenda haja kubwa au ndogo? Kwa dharura inawezekana, lakini sio hata katika mazingira ambayo maji ni bwerere.
Katika ofisi nyingi mijini, makaratasi yamekuwa ndio mtindo wa maisha ya watu, hawataki kutumia maji hata kama vyoo vina mifumo ya kujisafisha kwa kutumia maji.
Uchafu hotelini, migahawani
Ni kama wenye hoteli na migahawa wameungana kuhakikisha wateja wao tunadhurika. Ni jambo dogo kwa walio wengi lakini lina athari kiafya.
Nazungumzia tabia ya uwekaji wa sukari, chumvi, ndimu, au pilipili juu ya meza bila ya kufunika.
Kwa mujibu wa utafiti nilioufanya migahawa mingi ipo katika mazingira hatarishi na bado wahusika wanashindwa kuhifadhi vyakula hivi vinavyopendwa na walaji wengi.
Mara nyingi utawakuta nzi wamepiga kambi katika vifaa vinavyotumika kuwekea vitu hivi mezani. Sambamba na hili, wafanyabiashara wengi wa vyakula wameshtadi kuuza bidhaa zao katika mazingira hatarishi ya kutovifunika.
Hivi ndivyo ilivyo kwa wauza samaki mitaani, wauza mahindi, juisi na aina nyingine ya vyakula. Imeshakuwa mazoea na wala walaji hawajali afya zao kwa kununua vyakula visivyofunikwa.