Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Viwanda hatari vinavyotumia watoto kuzalisha nguo Bangladesh

Watoto wakishona nguo katika kiwanda kilichopo kwenye makazi mjini Dhaka.

Muktasari:

  • Ni vichafu, viko ndani ya makazi ya watu na hufanya kazi kwa ujira mdogo
  • 60: Asilimia ya viwanda vya kisasa vya Bangladesh vimeajiri wanawake
  • Sh105,000: Mshahara uliopitishwa na Serikali kwa watumishi wa viwanda vya nguo

Dhaka, Bangladesh

Mazingira ya uzalishaji katika viwanda vingi kwenye nchi maskini si mazuri sana. Uzalishaji katika sehemu nyingi hufanyika katika mazingira yanayohatarisha usalama wa maisha ya wafanyakazi.

Nchi ya Bangladesh yenye watu zaidi ya milioni 168, ina viwanda vingi vinavyozalisha bidhaa kwa ajili ya mataifa yaliyoendelea, lakini uzalishaji wake unafanyika katika mazingira hatari, dhalili na mabaya.

Kuna zaidi ya viwanda 700 katika taifa hilo lililopo kusini mwa Asia vilivyopo ndani ya nyumba za makazi, vinavyowatumia watoto wa kike na kiume kuzalisha bidhaa za aina mbalimbali, hususan nguo na mikanda.

Uchunguzi uliofanywa na mpigapicha Claudio Montesano katika eneo la Keraniganj jijini Dhaka na picha zake kuchapishwa kwenye mtandao wa Dailymail, zinaonyesha watoto wanavyofanyishwa kazi ngumu za ushonaji wa nguo.

Kwa mujibu wa mpigapicha huyo, katika viwanda hivyo ambavyo vingi havijakaguliwa na kuthibitishwa na Serikali, maelfu ya wafanyakazi hao watoto hutekeleza majukumu yao katika hali ngumu kwa ujira wa kati ya Sh17,500 hadi Sh40,000 kwa mwezi, lakini wanalazimika kufanya kazi kwa siku saba, huku wakiwa na nusu siku kwa ajili ya mapumziko.

Montesano anasema watoto hao ambao hufanyishwa kazi ya ushonaji wa nguo zinazosafirishwa katika masoko ya Ulaya na Marekani huvitumia viwanda hivyo pia kama makazi yao kwa sababu hula, kuoga na kulala sehemu hizo.

Mbaya zaidi ni kuwa, ndani ya majengo vilipo viwanda hivyo hakuna milango ya dharura wala mahali pa kutumia kutokea ndani inapotokea  hatari yoyote.

Pia hayana mpangilio wowote wa usalama wala vizima moto, wakati matumizi ya shughuli zake huambatana na nguo. Vilevile,  majengo hayo yamezingirwa na mifereji michafu na ni machakavu ndani na nje.   

Katika mojawapo wa jengo lililopo jirani na Kiwanda cha Rana Plaza kilichoteketea kwa moto mwaka 2013 na kuua watu 1,100 kuna kiwanda cha nguo ambacho watoto hufanya kazi za ushonaji kwa muda mrefu bila kupumzika.

Wakati kiwanda hicho kinazalisha nguo kwa ajili ya soko la ndani na nchi jirani, pia husafirisha nguo maarufu kwenye masoko ya mataifa yaliyoendelea kwa kutumia mbinu ambazo kampuni zinazopokea mizigo haziwezi kubaini mapema unakotoka.

Ndani ya chumba kimoja kuna  kiwanda chenye vyerehani hadi 15. Watoto wasioenda shule hupewa kazi ya kushona, kutia nakshi katika mavazi yaliyo tayari kupelekwa sokoni pamoja na usafishaji wa mashine.   

“Ndani ya viwanda hivi, wafanyakazi hufanya kazi kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa 12 jioni na kuwa na nusu siku ya mapumziko katika wiki moja baada ya kazi ngumu inayoambatana na vumbi jingi.  Wafanyakazi katika viwanda hivi hulala au kukodi vyumba jirani na viwanda hivi,” anasema mpigapicha huyo.

Wengi wa watoto wanaofanyakazi katika viwanda hivyo ni wale wanaotoka vijijini kukimbilia mjini kwa ajili ya kusaka ajira, wakiwa na matumaini ya kupata maisha bora. Hata hivyo, watoto hao huishia kusota bila kutimiza lengo la kuwa na maisha mazuri.

Baadhi ya wakazi wa Dhaka wanasema nguo zinazozalishwa katika viwanda hivyo huuzwa kwa bei ndogo kuliko zile zinazotengenezwa katika viwanda vikubwa vinavyokaguliwa mara kwa mara.

Serikali inasemaje?

Zaidi ya asilimia 80 ya viwanda vinavyozalisha nguo kwa ajili ya soko la nje vimekaguliwa na viko salama.

Mkaguzi Mkuu wa Viwanda wa nchi hiyo, Syed Ahmed anasema viwanda 1,475 vilikaguliwa kama sehemu ya mkakati wa Serikali kuhakikisha maeneo ya uzalishaji viwandani yako salama.

Hata hivyo, mkaguzi huyo anasema asilimia 81 ya majengo ya viwanda hivyo, vingi vikiwa katikati ya jiji viko yako salama, huku 37 kati ya vilivyokaguliwa vililazimika kufungwa kutokana na kuhatarisha usalama wa watumiaji.

Ahmed anasema viwanda 209 vimeonywa kuwa vinaweza kufungiwa iwapo havitachukua hatua ya kuboresha mazingira, usafi na miundombinu.

Kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef), Bangladesh ina zaidi ya watoto milioni moja wenye umri wa kati ya miaka 10 hadi 14 wanaotumikishwa viwandani.

 Sekta ya viwanda, hususan vya nguo nchini humo ni ya pili kwa usafirishaji nje bidhaa hizo ikitanguliwa na China. Hata hivyo nchi hiyo ina rekodi mbaya ya usalama kuliko mataifa yote yanayozalisha nguo. Mwaka 2013 zaidi ya watu 1,100 walikufa katika tukio la ajali mbaya ya viwandani.

Viwanda vya nguo nchini humo huchangia kwa asilimia kubwa katika pato la nchi hiyo, ikiingiza Sh52 trilioni kwa mwaka na kuchangia ajira ya watu milioni nne, wengi wao wakiwa wanawake.