Milionea Zimbabwe kuzikwa na dola

Muktasari:
Marafiki wa milionea Genius Kadungure, aliyejulikana kwa jina la Ginimbi katika mitandao ya kijamii, wamesema watamzika kwa kuweka mifuko ya dola ndani ya kaburi, vyombo vya habari vimeripoti.
Dar es Salaam. Marafiki wa milionea Genius Kadungure, aliyejulikana kwa jina la Ginimbi katika mitandao ya kijamii, wamesema watamzika kwa kuweka mifuko ya dola ndani ya kaburi, vyombo vya habari vimeripoti.
Mfanyabiashara huyo aliyeishi maisha ya kifahari aliacha maagizo kuwa katika mazishi yake watu wote wavae nguo nyeupe, kwa mujibu wa gazeti la Herald.
Ginimbi alifariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea Jumapili jijini Harare, akiwa na mwanamitindo Mitchelle Amuli, ambaye ni maarufu kwa jina la Moana.
Wakati marafiki wakijiandaa kumzika mwenzao pamoja na utajiri wake, familia ya Moana inaomba isaidiwe na wasamaria wema kufanikisha mazishi.
Familia hiyo imeahirisha mazishi yake kwa wiki mbili kusubiri matokeo ya vipimo vya DNA na kuchangisha fedha zinazotakiwa kwa ajili ya shughuli hiyo ya mazishi, tovuti ya Zim Morning Post imeripoti.
Matajiri wa Zimbabwe wamekuwa wakitoa ahadi za kufanikisha mazishi hayo.
Naibu waziri, Tino Machakaire ameahidi kununua jeneza la chapa ya versace kwa ajili ya Ginimbi, Temba Mliswa (mbunge) ameahidi kutoa wanyama ili wachinjwe kwa ajili ya chakula, wakati mwanasiasa Acie Lumumba ameahidi kutoa lita 1,000 za dizeli, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Zimbabwe.
Ginimbi na Moana walikuwa wakitoka katika sherehe ya watu wote kuvalia nguo nyeupe wakati gari lao lilipogonga gari jingine na kuacha njia kabla ya kugonga mti na kulipuka.
Haijaweza kufahamika kama familia ya Ginimbi imeweza kufuatilia mali za mtoto wao.
Kuna habari kwamba jumba lake la Domboshava lilifungwa kwa muda baada ya taarifa za kifo wakati familia ikijaribu kufanya utafiti wa mali zake.
Kuna habari kuwa mfanyabiashara mwanamke, Zodwa Mkandla alikuwa ni sehemu ya wamiliki wa jumba hilo.
Zim Morning Post imeandika kuwa: “Zodwa ameshaanza kujitangaza kuwa ndiye mke aliyesalia na ndiye mmiliki wa mali”.
Kwa mujibu wa nyaraka za mahakamani, jumba hilo, ambalo Ginimbi alikuwa anadai analimiki, linamilikiwa pamoja na Zodwa.
Katika kesi hiyo, Zodwa anadai kupoteza umiliki wa jumba hilo kutokana na mmoja wa wanasheria wake, anayejulikana kama Justice Jasi kulichukua. Justice anatuhumiwa kutotenda haki licha ya imani iliyowekwa kwake.