35 wafariki baada ya kutumbukia kisimani India

Wananchi wakiwa wamekizunguka kisima ambacho watu 35 wamefariki baada ya kutumbukia nchini India

Muktasari:

  • Watu 35 wamefarikidunia baada ya kutumbukia kisimani katika jimbo la Madhya Pradesh nchini India walipokua wakisali.

India. Takribani watu 35 wameuawa baada ya kutumbukia kwenye kisima walipokuwa wakisali katika hekalu moja katika jimbo la kati la India la Madhya Pradesh.

Wengine 14 wameokolewa na mtu mmoja bado hajapatikana katika ajali hiyo iliyotokea katika mji wa Indore jana Alhamisi.

Polisi walisema waathiriwa walikuwa wamesimama kwenye juu kisima hicho ndipo kilipoporomoka baada ya kulemewa na uzito.

Waziri Mkuu Narendra Modi amesema ameumizwa na ajali hiyo.

Kisa hicho kilitokea wakati wa hafla ya maombi iliyoandaliwa katika hekalu la Beleshwar Mahadev Jhulelal kwenye hafla ya sherehe ya Kihindu ya Ram Navami.

Umati mkubwa wa waumini walikuwa wamesimama kwenye zege iliyofunika kisima ambacho kiliporomoka kwa uzito wao na kuwatumbukiza watu wengi kwenye kisima chenye kina cha futi 40.

Vyombo vya habari vya eneo hilo vimeripoti kwamba hekalu hilo lilijengwa baada ya kisima hicho kufunikwa takriban miongo minne iliyopita.

Afisa mkuu Illayaraja, amekiambia kituo cha habari cha ANI kuwa watu 18 walilazwa hospitali baada ya kuokolewa na watu wawili wameruhusiwa. Aliongeza kuwa msako bado unaendelea ili kumpata mtu aliyetoweka.

Timu ya wafanyakazi 75, ikiwa ni pamoja na wale wa serikali na vikosi vya kitaifa vya kukabiliana na maafa wanashiriki katika juhudi za uokoaji.

Waziri Mkuu Shivraj Chouhan ametangaza fidia ya rupia 500,000 (Sh14 milioni) kwa jamaa wa marehemu.