Adaiwa kumuua mkewe kisha kuzunguka na mwili baa pombe

Muktasari:

  • Mwanaume adaiwa kumuua mkewe kutokana na ugomvi wa kifamilia kisha kuzunguka na mwili baa akinywa pombe. 

Dar es Salaam. Polisi wa kaunti ya Kericho nchini Kenya wako katika uchunguzi wa tukio la mwanaume mmoja kutoka eneo hilo aliyedaiwa kumuua mkewe, kisha kuzunguka na mwili huo baa akinywa pombe.

Tovuti ya NTV ya nchini humo imesema mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 46 anadaiwa kutekeleza mauaji hayo kwa kumchoma kisu kutokana na ugomvi wa kifamilia.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ndogo ya Belgut, Charles Kibati amesema kuwa mwanaume huyo ambaye ni fundi, alitenda kosa hilo Jumapili usiku kabla ya kuanza kuzunguka na mwili wa marehemu.

Kibati amesema alipofika nyumbani muda mfupi baadaye ugomvi ulizuka ambapo marehemu alitoa kisu na kutaka kumchoma mumewe, lakini mwanaume huyo  alikwepa na kumshika mkewe  kisha kumgeukia na kumuua.

“Baada ya kumuua, aliuchukua mwili wake akauweka kwenye siti ya gari, akaendesha hadi kituo kimoja cha biashara, akaliegesha na kwenda kwenye klabu ya usiku iliyopo karibu na kituo hicho.

“Hata hivyo, watu waliokuwa wakiendelea na starehe klabuni hapo walipata wasiwasi baada ya kuona madoa ya damu kwenye fulana yake ambapo walimtaka awapeleke alipoegesha gari,” amesema.

Ameendelea kusema, “watu hao waligundua maiti ya mwanamke ambaye baadaye alitambuliwa kuwa ni mkewe.

“Mwili ulikuwa ukivuja damu na ulikuwa na majeraha kichwani, mdomoni na machoni,” amebainisha.

Inaelezwa kuwa tukio hilo liliripotiwa polisi ambapo askari walikwenda eneo  la tukio, kisha kumkamata.

Aidha mwili huo ulitolewa na kupelekwa mochwari ya Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kericho huku gari likivutwa hadi Kituo cha Polisi cha Sosiot anaposhikiliwa.