Biden aunga mkono Afrika kuwa mwanachama G20

Muktasari:

Biden awaunga mkono Umoja wa Afrika kuwa mwanachama wa kudumu wa G20, na kuahidi kutoa kiasi cha $165million ambazo ni sawa na Sh379 bilioni, kusaidia uchaguzi na utawala bora barani Afrika mwaka ujao, baada ya kukutana na viongozi wa nchi ambazo zitafanya uchaguzi hivi karibuni.

Dar es Salaam. Rais wa Marekani, Joe Biden ametangaza kuunga mkono Umoja wa Afrika kujiunga na kundi la mataifa yenye uchumi mkubwa duniani (G20), huku wakitaka kujenga uhusiano imara na mataifa ya Afrika.

Akizungumza katika hafla ya mkutano wa Viongozi wa Marekani na Afrika jana Desemba 15, Biden amesema, “Uongozi wa Arika na uvumbuzi ni muhimu katika kushughulikia baadhi ya changamoto kubwa duniani.”

Kwa mujibu wa televisheni ya Aljazeera, mkutano huo umefanyika nchini Marekani, jijini Washngton, kuanzia Desemba 13 hadi 15, huku ukiwa umehudhuriwa na viongozi 49 kutoka Afrika,  akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania.

Biden ametaka kujenga upya uhusiano wa Marekani nje ya nchi baada ya miaka minne ya sera ya mambo ya nje ya rais wa zamani wa wa nchi hiyo, Donald Trump ya ‘Amerika Kwanza’ ambayo ilishuhudia nchi hiyo ikijiondoa katika mashirika na makubaliano ya kimataifa.

Hata hivyo, msukumo wa utawala wa Biden kuwekeza barani Afrika, unakuja dhidi ya hali ya ushindani wa kimataifa na China na Russia, ambayo imewekeza katika eneo hilo kwa kiwango ambacho kimeishinda Marekani katika miaka ya hivi karibuni.

Wakati mkutano huo ulikua ukimalizika, mazungumzo ya Alhamisi Desemba 15, 2022 yalikuwa maalum kwa majadiliano ya hali ya juu kuhusu Marekani kushirikiana na dira ya kimkakati ya Umoja wa Afrika kwa bara hilo.

Hiyo ni pamoja na usalama wa chakula, suala ambalo limezua wasiwasi wa kimataifa huku kukiwa na ongezeko la bei za vyakula linalohusishwa na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Kuongezaka kwa Umoja wa Afrika kwenye G20 kutayapa mataifa ya Afrika kauli katika masuala muhimu ya ulimwengu yakiwamo mabadiliko ya tabia nchi Uviko-19.

Wakati huo huo, Rais Biden amesema kwamba hivi karibuni atafanya ziara katika nchi zinazopatikana Kusini mwa Jangwa la Sahara na atatuma washauri wake wengi wakuu katika bara hilo, akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje, Antony Blinken, Katibu wa Hazina Janet Yellen na Katibu wa Biashara Gina Raimondo.

"Ninatazamia kuwaona katika nchi zenu," Biden amesema, bila kutoa maelezo zaidi juu ya ziara hiyo au lini itafanyika.

Kama ikitokea akafanya ziara hiyo Biden atakuwa rais wa kwanza wa Marekani kuzuru tangu Rais Barrack Obama aje Afrika.