El Chapo atuma ujumbe kwa Rais Mexico akiomba...

Muktasari:

  • El Chapo Guzman amuomba Rais wa Mexico kuingilia kati, mateso ya kisaikolojia anayopata katika Gereza la Marekani, ambapo anatumikia kifungo cha maisha jela nchini humo.

Dar es Salaam. Mlanguzi wa dawa za kulevya Joaquin "El Chapo" Guzman ameomba msaada kwa Rais wa Mexico kutokana na madai ya mateso ya kisaikolojia anayopata katika Gereza la Marekani.

"Katika miaka sita ambayo Joaquin amekuwa nchini Marekani, hajaona jua," alisema Jose Refugio Rodriguez, mwakilishi wa kisheria wa Mexico.

Kwa mujibu wa kituo cha habari ‘Mexico News Daily’ wameeleza kwamba ujumbe huo, unaofafanuliwa kama "SOS," ulipitishwa kupitia mmoja wa mawakili wa Guzman nchini Marekani pamoja na familia yake.

Rodriguez ambaye ni wakili wake ameeleza kwamba, Guzman anaruhusiwa tu kutoka nje mara tatu kwa wiki kwenye eneo dogo ambako hapati jua na ana matembezi machache kuliko wafungwa wengine.

"Anateswa kisaikolojia na ukosefu wa jua pia ni mbaya kwa afya ya kimwili,’’ amefafanua.

Guzman amemuomba Rais Andres Manuel Lopez Obrador kushughulikia madai ya ukiukaji wa taratibu wakati wa kurudishwa kwake mwaka 2017 chini ya serikali ya zamani, Rodriguez aliongeza.

Ubalozi wa Mexico mjini Washington ulithibitisha kwenye ukurasa wao wa Twitter Jumanne ya Februari 17, kwamba ulipokea barua pepe kutoka kwa Rodríguez Januari 10.

Bila kurejelea yaliyomo kwenye barua pepe hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Mexico, Marcelo Ebrard alipuuza maombi hayo kwa serikali kwa ajili ya mlanguzi huyo wa dawa za kulevya.

"Anatumikia kifungo huko, ana kifungo," aliwaambia waandishi wa habari. "Kwa hivyo, kusema ukweli sioni uwezekano wowote kwake, lakini nitawasiliana na ofisi ya mwendesha mashtaka."

El Chapo anatumikia kifungo cha maisha jela nchini Marekani baada ya kukutwa na hatia mwaka 2019 kwa makosa ya ulanguzi wa dawa za kulevya, utakatishaji fedha na makosa yanayohusiana na silaha.

Mmoja wa wanawe, Ovidio Guzman, alikamatwa na vikosi vya usalama vya Mexico mwezi huu katika operesheni iliyosababisha vifo vya watu 29 na kusababisha ufyatulianaji wa risasi katika uwanja wa ndege katika mji wa Culiacan.