Israel yatoa masharti vita Gaza

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema nchi yake haitakubali usitishwaji wa vita Gaza, iwapo mpango huo hautahusisha kuachiliwa kwa mateka.

DW imeripoti kuwa Netanyahu ameweka wazi msimamo huo baada ya kukutana na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Antony Blinken ambaye taifa lake linataka vita visitishwe ili misaada ifike Gaza.

Netanyahu amesema aliweka wazi kuwa wataendelea kusonga mbele kwa nguvu zote, na kwamba wanakataa usitishwaji wowote wa mapigano ambao hautajumuisha kuwachiwa kwa mateka wao.

Maofisa wa Israel wanakadiria kuwa karibu watu 249 walitekwa katika mashambulizi ya Oktoba saba na wanashikiliwa mateka Gaza.

Pia Umoja wa Mataifa umekuwa ukitoa wito wa usitishwaji wa mapigano ili kuruhusu upelekaji wa misaada ya kibinadamu.

Awali Blinken alikutana na Rais wa Israel, Isaac Herzog mjini Tel Aviv, akisisitiza kuwa Israel ina haki ya kujilinda, wakati akizungumzia haja ya kuongeza kwa kiasi kikubwa na haraka msaada endelevu katika Ukanda wa Gaza.

Blinken vilevile alisisitiza kuhusu ulinzi wa raia wa Gaza ambao wamenaswa katika makabiliano hayo yaliyochochewa na Hamas, akisisitiza kuwa kila kitu kifanywe kuwalinda na kupeleka msaada kwa wale wanaouhitaji kwa dharura na ambao kwa njia yoyote ile hawahusiki na matukio ya Oktoba saba.

Alipoulizwa kuhusu hotuba ya kiongozi mkuu wa Hezbollah Sayyed Hassan Nasrallah, Blinken alisisitiza kuwa Marekani imedhamiria kuhakikisha kuwa hakuna upande wa pili na wa tatu katika mzozo huo.

Alisema Marekani iko katika hali ya tahadhari kubwa katika upande wa kaskazini, kujibu tukio lolote linaloweza kutokekea kwa sasa na katika siku zijazo kuhusiana na Lebanon, Hezbollah au Iran. Nasrallah alionya kuwa vita kati ya Israel na Hamas vinaweza kugeuka kuwa mzozo wa kikanda kama mashambulizi yataendelea Gaza.