Machifu wamlilia hayati Magufuli
Muktasari:
- Umoja wa machifu Tanzania (UMT) na viongozi wa mila kutoka makabila mbalimbali Tanzania umesema utamkumbuka hayati John Magufuli kwa namna alivyoongoza nchi kwa uzalendo, uthubutu, utendaji kazi na maamuzi katika kutekeleza jambo alilolikusudia.
Moshi. Umoja wa Machifu Tanzani (UMT) umesema utamkumbuka akiyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dk John Magufuli, kwa uzalendo, uthubutu na maamuzi yake.
Akitoa taarifa Machi 22, 2021, Mwenyekiti wa UMT, Frank Marialle amesema, machifu wamepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha aliyekuwa kiongozi mkuu wa nchi na kwamba, ataendelea kuishi kwenye mioyo yao kutokana na mambo makubwa aliyoyafanya kwa Taifa.
"Tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha ya Hayati Magufuli kwa uongozi, uzalendo,uthubutu, utendaji na maamuzi yake, ambayo yalikuwa ni leo leo, hapakuwa na njoo kesho katika kipindi cha uongozi wake" amesema Marialle
"Tunatoa pole kwa Rais mpya wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Mama Janeth Magufuli, watoto, Watanzania wote na Waafrika wote popote walipo duniani"
Aidha umoja huo umeiomba Serikali kuyaendeleza yale yote mema yaliyodhamiriwa na hayati Magufuli, na kwamba wao kama viongozi wa Kimila wataendelea kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa Rais mpya na viongozi wote wa Serikali katika kulijenga taifa.
Akizungumza Chifu wa Kigoma, Isambe Gilbert amesema hayati Magufuli ni mmoja wa viongozi waliofanya kazi kwa kushirikiana na viongozi wa kimila katika kuhakikisha Taifa linasonga mbele kimaendeleo.
Naye Mwenyekiti wa Malegwanani Tanzanua Joseph Laizer amesema kifo cha Magufuli ni pigo kubwa kwa taifa na kwamba wataendelea kuyaenzi yale yote mazuri yaliyokuwa yakifanywa na kiongozi huyo.
"Tumepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha kiongozi huyu, hakika Magufuli alishatutoa mahali pagumu na sasa ameondoka, tuiombe Serikali iendeleze yale yote mema yaliyokuwa yakifanywa ili kuliwezesha taifa kufika pale lilipo kusudiwa" amesema Laizer.