Mafua yakwamisha mkutano wa Papa Francis

Muktasari:

  • Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amelazimika kuahirisha mkutano wake na waumini kutokana na kuugua mafua.

Dar es Salaam. Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amelazimika kuahirisha mkutano wake na waumini kutokana na kuugua mafua.

Papa (86) kwa kawaida hufanya mikutano na maofisa wa Vatican pamoja na waumini siku ya Jumamosi, lakini safari hii haukufanyika.

Taarifa kutoka Vatican zinasema, mkutano huo uliokuwa ufanyike jana, Novemba 25, 2023 umeahirishwa kutokana na hali yake ya kiafya na alilazimika kwenda hospitali kwa matibabu.

Tovuti ya Vatican News imesema Papa alipofika Hospitali ya Roma ya Gemelli iliyopo kisiwani Tiberia, alifanyiwa uchunguzi wa CT scan kwenye mapafu.

“Vipimo vilitoa matokeo kwamba hakuna matatizo ya mapafu. Sasa amerudi katika makazi yake ya Vatican ya Casa Santa Marta.

“Alipokuwa na umri wa miaka 21, Papa Francis alipata ‘pleurisy’, kuvimba kwa tishu zinazozunguka pafu, ambayo ilisababisha kufanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe na sehemu ndogo ya pafu lake la juu la kulia,” imeeleza taarifa hiyo.

Roma, pamoja na sehemu kubwa ya Italia, kwa sasa joto limepungua katika siku za hivi karibuni, hali inayopelekea kuongezeka kwa magonjwa ya msimu ikiwamo mafua.