Mahakama yaamuru Rais wa zamani Afrika Kusini arudi jela

Muktasari:

  • Mahakama ya Juu ya Rufani (SCA) nchini Afrika Kusini imeitupa rufaa ya Rais wa zamani wa nchi hiyo, Jacob Zuma na kuamuru arejeshwe gerezani.


Cape Town. Mahakama ya Juu ya Rufani (SCA) nchini Afrika Kusini imeitupa rufaa ya Rais wa zamani wa nchi hiyo, Jacob Zuma na kuamuru arejeshwe gerezani.

 Zuma ambaye alihukumiwa kifungo cha miezi 18 jela kwa kuidharau mahakama, alikata rufaa ya kuomba kuachiwa huru kwa msamaha wa matibabu ambayo hata hivyo imegonga mwamba.

Hukumu iliyotolewa jana Jumatatu Novemba 21, 2022 ilisema Zuma lazima arudi gerezani kuendelea na kifungo kwa kuwa kumpa msamaha wa matibabu ni kinyume na sheria.

Zuma (80) aliyeondoka madarakani Februari 2018, alitolewa gerezani baada ya miezi miwili kwa maelezo ya kusumbuliwa na maradhi.

Idara ya huduma za marekebisho nchini humo ilitoa taarifa ikithibitisha kuwa rais huyo wa zamani atamalizia kifungo chake nyumbani baada ya kufanyiwa upasuaji.

Hata hivyo, jana Jumatatu, Mahakama ya Juu ya Rufani imesema msamaha wa matibabu kwa Zuma ni kinyume cha sheria na anatakiwa kurudi gerezani kumalizia kifungo chake.

Mahakama hiyo ilisema maofisa wa magereza ndiyo wenye mamlaka ya kuamua siku alizotumia Zuma nje ya gereza kama zitahesabika kwenye kifungo chake hicho au la.

Zuma anatumikia kifungo hicho kwenye gereza la Estcourt lililopo KwaZulu-Natal. Hatua iliyobaki ni kwa Zuma ni kukata rufaa kwenye Mahakama ya Katiba.

Mahakama ya Katiba ndiyo ilimuhukumu Zuma kifungo hicho baada kumkuta na hatia ya kudharau baada ya kushindwa kuitikia wito wa Tume ya Uchunguzi ya Zondo iliyokuwa chini ya Jaji Raymond Zondo ikichunguza tuhuma za ufisadi za Zuma.

Hoja za mawakili wa Zuma kwamba kiongozi huyo wa zamani anahitaji matibabu ambazo hazipo gerezani hazikufua dafu na wamesema watakwenda Mahakama ya Katiba.

Zuma aliwahi kutumikia kifungo cha miaka 10 jela katika gereza la Roben island kutokana na ushiriki wake kwenye harakati za ukombozi dhidi ya utawala wa mfumo wa kibaguzi.

Tuhuma zake

Zuma anatuhumiwa kujihusisha na masuala ya rushwa miaka 20 iliyopita.

Pia, anakabiliwa na mashitaka 16 ya ulaghai, rushwa na ulanguzi unaohusiana na ununuzi wa ndege za kivita, boti za doria na vifaa vya kijeshi kutoka kampuni tano za silaha za Ulaya kwa randi bilioni 30 sawa na dola bilioni tano za kimarekani.

Marais wa Afrika waliofungwa

Zuma aliyejiuzulu mwaka 2018 anaingia kwenye orodha ya idadi ya marais na viongozi wakuu wa nchi waliowahi kufungwa jela kwa makosa mbalimbali mara baada ya kumaliza muda wao madarakani ama kujizulu wadhifa huo wa urais.

Makosa mengi wanayofungwa nao viongozi wa mataifa mengi yanahusishwa na masuala ya ufisadi, mauaji au matumizi mabaya ya madaraka.

Zaidi ya viongozi wakuu 40 kutoka nchi za Afrika wamewahi kuonja jela kwa sababu mbalimbali zilizohusiana na nafasi ya ama urais, umakamu wa rais ama waziri mkuu.

Kesi za Zuma

2005: Alishtakiwa kwa kumbaka rafiki wa familia yake kabla ya kuondolewa mashtaka mwaka 2006.

2005: Alishtakiwa na ufisadi uliohusisha mamilioni ya fedha za ununuzi wa silaha 1999, lakini mashtaka hayo yakaondolewa muda mchache kabla ya kuwa rais 2009.

2016: Mahakama iliagiza ashtakiwe na mashataka 18 ya ufisadi kuhusu kashfa hiyo - alikata rufaa, lakini mwaka 2017 alishindwa kubatilisha uamuzi.

2016: Mahakama iliamuru alikwenda kinyume na kiapo alichokula kwa kutumia fedha za Serikali kurekebisha nyumba yake ya kibinafsi huko Nkandla - alilipa fedha alizotumia.

2017: Mlinzi wa umma alisema anapaswa kuteuwa jopo ili kuchunguza madai alijipatia faida kutokana na ushirikiano na familia ya kitajiri ya Gupta - alikana madai hayo kama Gupta walivyofanya.

2018: Zuma aliidhinisha madai ya kuibia Serikali.

2018: Mamlaka ya kitaifa ya kuwashtaki washukiwa ilithibitisha Zuma atakabiliwa na mashtaka 12 ya ulaghai.