Marekani, Iran zaanza kushambuliana tena, bei ya mafuta yapaa
Mvutano kati ya Marekani na Iran umeingia hatua mpya baada ya jeshi la Marekani kutangaza kushambulia zaidi ya maeneo 80 ya kijeshi nchini Iran, likisema hatua hiyo ni jibu la mashambulizi dhidi ya meli tatu za mafuta katika Mlango wa Hormuz, huku Tehran ikijibu kwa kushambulia vituo vya kijeshi vya Marekani nchini Bahrain na Kuwait.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Reuters, Marekani na Iran zimeanza kushambuliana tena leo Jumatano Julai 8, 2026, baada ya kipindi kifupi cha utulivu uliotokana na makubaliano ya muda ya kupunguza mapigano.
Mashambulizi hayo yameongeza hofu ya kusambaratika kwa makubaliano ya muda yaliyokuwa yakilenga kupunguza mapigano kati ya mataifa hayo mawili, hali iliyotikisa masoko ya dunia na kusababisha bei ya mafuta kupanda kwa zaidi ya asilimia tano.
Bei ya mafuta ghafi ilikuwa imeshuka hadi takribani Sh203,000 kwa pipa baada ya hali ya usalama kuimarika katika Mlango wa Hormuz. Hata hivyo, mashambulizi mapya yaliyohusishwa na Iran yameibua hofu ya usumbufu wa usafirishaji na bei kupanda hadi karibu Sh214,000 kwa pipa.
Hilo ni ongezeko la takribani asilimia 5.4, likionyesha jinsi mivutano katika Hormuz, ambako hupita karibu asilimia 20 ya mafuta yanayouzwa duniani, inavyoathiri haraka soko la nishati na matarajio ya mfumuko wa bei duniani.
Kwa mujibu wa Jeshi la Marekani (CENTCOM), mashambulizi hayo yalilenga mifumo ya ulinzi wa anga, vituo vya uongozi, rada za pwani, makombora ya kupambana na meli pamoja na zaidi ya boti 60 za Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC), kwa lengo la kudhoofisha uwezo wa Tehran kutishia usafirishaji wa kimataifa kupitia Mlango wa Hormuz.
Iran, kupitia Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi (IRGC), ilisema ilijibu kwa kurusha makombora na ndege zisizo na rubani kuelekea vituo vya jeshi la Marekani nchini Bahrain na Kuwait, ikidai mashambulizi ya Washington yalikiuka makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyokuwa yamefikiwa awali.
Mashambulizi hayo yamechochea ongezeko la bei ya mafuta ya Brent na WTI kutokana na hofu ya kuvurugika kwa usafirishaji wa mafuta kupitia Mlango wa Hormuz, ambao ni njia muhimu ya biashara ya nishati duniani.