Marekani, Iran zakubaliana kusitisha mapigano, Hormuz kufunguliwa
Sehemu ya Mlango wa Hormuz. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Rais wa Marekani, Donald Trump, ametangaza kupitia mtandao wake wa Truth Social kwamba makubaliano na Iran yamekamilika.
Washington/Tehran. Marekani na Iran zimetangaza kufikia makubaliano ya awali ya kusitisha vita vilivyodumu kwa miezi kadhaa na kufungua tena Mlango wa Bahari wa Hormuz, hatua iliyopunguza hofu katika soko la mafuta duniani huku bei zikianza kushuka.
Makubaliano hayo, ambayo bado ni ya mfumo wa awali, yanatajwa kuwa hatua kubwa zaidi kuelekea kumaliza mgogoro uliozuka Februari mwaka huu baada ya mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, yaliyosababisha maelfu ya vifo na kuyumbisha masoko ya nishati duniani.
Rais wa Marekani, Donald Trump, ametangaza kupitia mtandao wake wa Truth Social kwamba makubaliano na Iran yamekamilika.
“Tumehitimisha makubaliano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran,” ameandika Trump Jumapili jioni kwa saa za Washington.
Kauli hiyo ilikuja muda mfupi baada ya Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, ambaye nchi yake imekuwa mpatanishi katika mazungumzo hayo, kutangaza kuwa pande hizo zimefikia mwafaka mapema leo Juni 15, 2026.
Kwa mujibu wa Sharif, makubaliano hayo yanataka kusitishwa mara moja na kwa kudumu kwa operesheni zote za kijeshi katika maeneo yote ya mgogoro, ikiwemo nchini Lebanon.
Makubaliano hayo yanatarajiwa kutiwa saini rasmi Ijumaa nchini Switzerland.
Hata hivyo, masharti kamili ya mkataba huo bado hayajawekwa wazi, huku hatma ya mpango wa nyuklia wa Iran ikitarajiwa kujadiliwa katika mazungumzo yatakayofuata.
Katika taarifa yake, Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran limesema vita na operesheni za kijeshi katika maeneo yote, ikiwemo Lebanon, zitakoma rasmi kuanzia usiku wa leo Jumatatu.
Licha ya hatua hiyo, Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, amesema jeshi la nchi hiyo litaendelea kuwepo katika maeneo ya kiusalama nchini Lebanon, Syria na Gaza kwa muda usiojulikana ili kulinda mipaka na makazi ya Waisraeli.
Katz amesema yeye pamoja na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, wamewasilisha msimamo huo kwa Trump na viongozi wengine wa Marekani.
“Iwapo Iran itaishambulia Israel kutokana na matukio yanayotokea Lebanon, tutaijibu kwa nguvu zote na kuonyesha wazi tofauti ya uwezo uliopo,” amesema Katz.
Makubaliano hayo yanatajwa kuwa hatua muhimu ya kupunguza mvutano katika Mashariki ya Kati, ingawa wachambuzi wanaonya kuwa mafanikio yake yatategemea utekelezaji wake na maendeleo ya mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.