Matajiri wataka watozwe kodi
Muigizaji Simon Pegg ni miongoni mwa mamilionea waliandika barua Davos kutaka kutozwa kodi utajiri wao ulikithiri.
Muktasari:
- Katika barua yao wamesema wanashangaa wito wao wa awali wa utajiri wao uliokithiri kutozwa kodi na kuanzisha kodi ya asilimia mbili kwa matajiri zaidi haujasikilizwa.
Davos. Takriban mamilionea na mabilionea 270 duniani wameandika barua kwa viongozi wa Serikali na wanasiasa waongeze kodi ya utajiri wao, huku wengine wakitaka asilimia mbili zaidi ziongezwe kwa wenye utajiri zaidi.
Matajiri hao wameandika barua yenye saini zao kwa viongozi wa Serikali na wanasiasa wanaohudhuria Mkutano wa 54 wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) unaofanyika Davos nchini Uswisi.
Barua hiyo imewataka viongozi wa dunia waliopo Davos kwa ajili ya WEF kuongeza kodi kwenye utajiri wao uliokithiri huku wakionya kwamba ikiwa viongozi waliochaguliwa kidemokrasia hawatashughulikia ongezeko kubwa la ukosefu wa usawa wa kiuchumi, matokeo yake yatakuwa ni janga.
"Ombi letu ni rahisi: Matajiri zaidi katika jamii, utajiri wao utozwe kodi,” ilieleza barua hiyo yenye saini za matajiri 270 kutoka nchi 17 duniani.
"Hii haitabadilisha kiwango chetu cha maisha, wala kuwanyima watoto wetu, wala kudhuru ukuaji wa uchumi wa mataifa yetu. Lakini, itageuza utajiri wa kibinafsi uliokithiri na usio na tija kuwa uwekezaji kwa mustakabali wetu wa pamoja wa kidemokrasia."
Jukwaa hilo la uchumi lilianza Jumatatu ya Januari 15 na linamalizia Ijumaa ya Januari 19, 2024.
Katika barua yao walisema wanashangaa wito wao wa awali wa kutaka utajiri wao uliokithiri kutozwa kodi na ombi la kuongeza asilimia mbili ya kodi kwa matajiri zaidi kutofanyiwa kazi, wakisema wao hawataki mabadiliko makubwa, bali sera za kifedha ambazo zitazuia jamii kuzidi kuharibika.
"Ukosefu wa usawa umefikia hatua ya mwisho, na gharama yake kiuchumi, kijamii na kisaikolojia ni kubwa na zinakua kila siku. Kwa ufupi, tunahitaji hatua sasa," inasema barua hiyo, ikiongeza kuwa hisani na michango ya mara moja haitarekebisha suala la usawa wa kiuchumi.
"Si tu kwamba tunataka kutozwa kodi zaidi, lakini tunaamini lazima tutozwe kodi zaidi. Tungejivunia kuishi katika nchi ambazo hili linatarajiwa na kujivunia viongozi waliochaguliwa ambao wanajenga mustakabali bora," ilisema barua hiyo.
Watia saini wa barua hiyo ni pamoja na mtengenezaji wa filamu na mrithi wa Disney, Abigail Disney, waigizaji Simon Pegg na Brian Cox na Valerie Rockefeller wa familia ya Rockefeller ya Marekani.
"Tunahitaji Serikali zetu na viongozi wetu waongoze. Na kwa hivyo tunakuja kwako tena na ombi la dharura kwamba wachukue hatua. Kwa upande mmoja katika ngazi ya kitaifa, na kwa pamoja katika jukwaa la kimataifa," walisema.
Barua hiyo inakuja wakati kura ya maoni mpya iliyochapishwa Jumatano ya Januari 17, 2024 inaonyesha kuwa asilimia 74 ya watu matajiri wanaunga mkono kuongezwa kodi utajiri wao, wakati asilimia 75 wanaunga mkono kuanzishwa kwa kodi ya asilimia mbili kwa mabilionea, kama ilivyopendekezwa na Shirika la Kodi la Umoja wa Ulaya.
Kura ya maoni kwa niaba ya Mamilionea Wazalendo wasioegemea upande wowote, iliwahoji zaidi ya watu 2,300 kutoka nchi za kundi la G-20 ambao wanamiliki zaidi ya dola milioni moja katika mali zinazoweza kuwekezwa, bila kujumuisha nyumba zao, na kuwafanya kuwa na asilimia tano zaidi ya utajiri katika jamii.
Wengine waliohojiwa, asilimia 58 walisema wanaunga mkono kuanzishwa kwa kodi zaidi ya asilimia mbili kwa matajiri wenye fedha zaidi ya Dola milioni 10.
Ripoti ya Oxfam ilionyesha ukosefu wa usawa umezidi kuwa mbaya tangu 2020, na kuwa watu watano matajiri zaidi duniani wanaona utajiri wao ukiongezeka mara mbili huku asilimia 60 ya maskini zaidi duniani wakizidi kuwa maskini.