Mbunge ataka sheria kudhibiti wanaochafua hewa kwenye ndege

Mbunge wa Rangwe, Lilian Gogo aliibua kicheko katika Bunge la Kenya juzi alipopendekeza kuwa itungwe sheria ya kudhibiti abiria wanaotoa ushuzi kwenye ndege na kusababisha usumbufu kwa abiria wengine.
Mbunge huyo alishauri abiria hao wapewe tembe za kupunguza asidi ili kuwazuia kutoa hewa hiyo mbaya, kwa mujibu wa Gazeti la Taifa Leo.
Akichangia mjadala kuhusu muswada wa Sheria ya Kudhibiti Makosa ambayo hutendwa na abiria kwenye ndege, Gogo alisema kujamba katika ndege ni usumbufu ambao mara nyingi hupuuzwa.
“Pamoja na masuala mengine ambayo yanaweza kuhatarisha usalama au kusababisha usumbufu kwa abiria, ushuzi pia ni chanzo cha usumbufu japo hupuuzwa. Kuna abiria ambao hutoa harufu inayokera zaidi baada ya kujamba,” akasema Gogo.
Mbunge huyo aliongeza kuwa ushuzi pia husababisha machungu kwa abiria wanaosafiri kwenye ndege.
“Inapaswa kuwapo sheria inayodhibiti chakula wanachopewa abiria katika ndege kando na mikakati ya tiba ambayo inaweza kupunguza kiwango cha gesi mbaya ambayo mtu anaweza kutoa kwenye ndege,” Gogo alilalamika.
Mbunge huyo alitoa mifano ya ndege ambazo husafiri kutoka Kisumu kwenda Nairobi akisema ndiko abiria hujamba kila mara bila kujizuia.
“Hii ndio maana napendekeza kuwa mashirika ya ndege yanayohudumu katika ruti hiyo yawape abiri dawa za kupunguza asidi ili kuzuia kero hili,” Dk Gogo akakariri.
“Sheria iwepo ya kulazimisha mashirika ya ndege kununua dawa kama vile ‘eno’ na kuwapa abiria wao ambao huenda wakapata matatizo ya tumbo kwa kula chakula nyingi kupita kiasi,” akaongeza.
Spika wa muda wa Bunge, Chris Omulele aliunga mkono pendekezo la Dk Gogo akisema tabia ya kujamba imekithiri zaidi na baadhi ya abiria hulazimika kuvumilia usumbufu wakiwa safarini.
Dk Gogo pia anapendekeza sheria kuanzishwa na mashirika ya ndege kwa ajili ya kudhibiti kiwango cha pombe ambayo abiria hupewa.
Alisema baadhi ya abiria ambao hudhihirisha tabia mbaya katika ndege wamebainika kuwa ni walevi baada ya kubugia pombe kupita kiasi.
“Kwa nini isiwepo sheria ya kudhibiti kiwango cha pombe ambayo inaruhusiwa kunywewa na abiria kwani baadhi yao hunywa pombe nyingi wanayopewa.
Wabunge waliochangia mjadala huo walisema mabadiliko yanapasa kufanywa na jumuiya ya mataifa kuhusu usalama wa abiria katika ndege, ikiwamo kuimarishwa kwa mafunzo yanayotolewa kwa wahudumu wa ndege.
“Wanafaa kufunzwa mbinu bora za kuwadhibiti abiria wanaonyesha mienendo mibaya safarini,” akasema Mbunge wa Kimilili, Chris Wamalwa.
Alishauri wahudumu kufunzwa kwamba abiria hawafai kuruhusiwa kubugia pombe kupita kiasi.