Mtoto wa Museveni aibua tena kauli tata uvamizi Nairobi

Muktasari:

  • Mtoto wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni, Muhoozi Kainerugaba amesisitiza kauli yake ambayo amewahi kuitoa siku za nyuma kwamba atauvamia mji mkuu wa Kenya, Nairobi jambo linalochochea mzozo wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.

Dar es Salaam. Kauli ya Mtoto wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni, Muhoozi Kainerugaba la jeshi la nchi hiyo kuuteka mji mkuu wa Kenya (Nairobi) imeibua hisia upya ya mzozo wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.

Kauli hiyo ameitoa jana Januari 20 kupitia ujumbe wake wa Twitter, akisema hajali athari zitakazotokea na kuongeza kuwa baba yake anaweza kumfukuza kutoka jeshini.

"Nitaiteka Nairobi hakika, huo ni mji wangu. Mkenya yoyote akijaribu kunizuia atakuwa supu, atakua kinywaji kwenye chakula cha jioni. Baba yangu anaweza kunifukuza tena akitaka," ameandika Muhoozi.

Muhoozi ameongeza kuwa yeye ndiye atakayekuwa rais wa Uganda baada ya baba yake ambaye amekua madarakani tangu 1986.

Muhoozi amewataka wakenya kumuomba radhi yeye na familia yake kwa madai ya kupigwa.

Ameongeza kuwa alipata vipigo kwa sababu alikuwa mtoto wa Museveni kipindi ambacho baba yake alikuwa anapambana dhidi ya serikali kuchukua kiti cha urais.

"Wakenya wanahitaji kuniomba msamaha kwa vipigo vyote, nikiwa mvulana mdogo, nilipata kwa sababu nilikuwa mtoto wa Museveni mwanzoni mwa miaka ya 1980."

Hapo awali, Uganda iliyapinga maneno ya Muhoozi ya kupendekeza jeshi la nchi hiyo kutumia wiki mbili tu kuiteka Nairobi.

Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Jumanne, Oktoba 4, 2022 kupitia Wizara ya Mambo ya Nje, nchi hiyo jirani ilisema hawafanyi sera kupitia mitandao ya kijamii.

"Wizara ya Mambo ya Nje inapenda kufafanua kwamba Serikali ya Jamhuri ya Uganda haitekelezi Sera yake ya Mambo ya Nje na majukumu mengine rasmi kwenye mitandao ya kijamii."

Wakati mjadala mkali uliosababishwa na maandishi yenye utata ya Muhoozi katika mtandao wa Twitter ukishika kasi, Uganda imesema wanathamini ujirani wa kindugu dhidi ya majirani zao Kenya.