Mwanafunzi akutwa ameuawa kichakani

Adah Nyambura kwenye picha ndogo enzi za uhai wake, picha kubwa baba yake, Mtiri

What you need to know:

  • Baba mzazi wa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara ambaye mwili wake umepatikana kichakani karibu na chuo hicho, afichua mateso aliyoyapata binti yake kabla hajauawa.

Meru. Baba mzazi wa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara ambaye mwili wake umepatikana kichakani karibu na chuo hicho, afichua mateso aliyoyapata binti yake kabla hajauawa.

Miriti amesema uchunguzi wa mwili uliofanywa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Narok, umeonyesha binti yake Adah Nyambura, alibakwa, kisha kuchomwa na pasi baadaye kuuawa.

Akizungumza nyumbani kwake Mikunduri, Tigania Mashariki katika Kaunti ya Meru, Miriti alisema Ijumaa iliyopita, binti yake huyo alimpigia simu kumwambia angerejea nyumbani Jumatatu au Jumanne wiki hii.

Baada ya simu hiyo, Miriti  amesema hakuwa na wasiwasi kwani tayari waliishakubaliana siku angerudi nyumbani japo pia alikuwa amemfahamisha baba yake kuwa jioni hiyo, angehudhuria sherehe na marafiki zake.

Hata hivyo, baba huyo amesema kuwa siku ya Jumamosi alipojaribu kumpigia simu hakupokea. Mkewe, Isabella Karimi, naye alijaribu bila mafanikio na jambo hilo liliwatia wasiwasi kwa sababu binti yao hawezi kuacha kupokea simu za mama yake.

Kilicholeta mshtuko na wasiwasi ni pale simu ya binti yao ilizimwa na kwamba siku ya Jumapili wakiwa kanisani, alipigiwa simu na ofisa wa polisi kumjulisha kupatikana kwa mwili wa binti yake.

“Alinivunja moyo. Sikuweza kuelewa alichokuwa anazungumza. Nilichosikia ni kwamba mwili umepatikana umetupwa mahali fulani. Nilisafiri hadi Narok bila kumwambia mke wangu kilichotokea kwa sababu nilikuwa na hofu kumwambia,” amesema Miriti.

Baada ya kuutazama mwili wa marehemu katika chumba cha kuhifadhia maiti, baba huyo alisema kuwa, kwa msaada wa maafisa wa toka ofisi ya DCI, alifuatilia dakika za mwisho za binti yake akijaribu kujua alikuwa  na nani kabla hajafariki.

"Nilienda kwenye klabu ambapo walifanya sherehe na nikaonyeshwa picha na video zao wakifurahi. Alionekana mwenye furaha sana na sikuweza kufikiria mwili wake ungekuwa umelazwa katika chumba cha kuhifadhia maiti,” alikumbuka.

Pia aliambiwa alikuwa na mwanaume mmoja na wenzake lakini muda wa kuondoka ulipofika muda wa saa tatu asubuhi, mpenzi wake alichukua simu yake na kumuacha klabuni hapo.

Alienda nyumbani Jumamosi asubuhi na hiyo ilikuwa mara ya mwisho kuonekana akiwa hai.

Mwanamume aliyechukua simu yake yuko kizuizini akihojiwa na polisi lakini taarifa alizopata Miriti zilipingana na maelezo ya mwanaume huyo aliyoyatoa polisi kwamba alitoweka Jumapili asubuhi.

Hoja kadhaa zimeibuka kuhusu mahali ambapo Adah alikuwa kati ya Jumamosi asubuhi na Jumapili aliporipotiwa kutoweka.

“Pia tulienda eneo la tukio ambapo mwili wake ulipatikana kwenye kichaka. Maafisa waliniambia mwili wake ulikuwa nusu uchi na hakuwa na viatu hivyo muuaji lazima alitekeleza maujai sehemu nyingine na kisha kuutupa mwili hapo. Lakini pia majeraha ya kuchomwa na pasi yanadhihirisha wazi kuwa mauaji yalitokea chumbani," alisema.

“Wameniibia mzaliwa wangu wa kwanza ambaye nilikuwa na mipango mikubwa kwake. Alikuwa rafiki yangu na hangenificha chochote… mama yake amechanganyikiwa sana haongei,” alisema huku akitokwa na machozi.

Alifichua kuwa baada ya kuzungumza Ijumaa, alishauriana na mkuu wa shule ya sekondari na kupanga jinsi Adah ambaye alikuwa mwanafunzi wa Shahada ya Elimu (Hisabati na Biashara) angefundisha shuleni hapo kabla ya kuripoti shuleni Septemba.

“Nilimjulisha mipango hiyo na alifurahi kwamba angeanza mazoezi yake ya vitendo mapema. Nilimtumia pesa nikitarajia kwamba angerudi nyumbani. Lakini yote hayo yamepita. Ni uchungu sana nilienda kuchukua mwili wake,

Baba alisema. Mtoto wake mwingine yuko Darasa la Saba.

Baada ya uchunguzi, polisi walimruhusu kuuhamisha mwili huo na umehifadhiwa katika mochwari ya Meru ukisubiri kuzikwa Mei 10.

"Ninatoa wito kwa polisi kuharakisha uchunguzi kwa sababu tunataka kujua ni nani aliyemuua binti yetu. Ingawa hii haitamrudisha lakini haki lazima itendeke. Pia tunaomba Mungu atupe nguvu za kukubali ukweli huu…”


Imeandaliwa na Pelagia Daniel