Niger yasimamishwa uanachama Umoja wa Afrika
Muktasari:
- Umoja wa Afrika (AU) umeisimamisha Niger katika jumuiya hiyo, kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya mwezi uliopita katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Ethiopia. Umoja wa Afrika (AU) umeisimamisha Niger katika jumuiya hiyo, kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya mwezi uliopita katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Uamuzi huo uliotangazwa leo Jumanne Agosti 22, 2023 umekuja baada ya mkutano wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika kutoa uamuzi huo katika mji mkuu wa Ethiopia wa Addis Ababa.
Miongoni mwa sababu zilizotajwa za mkutano huo ni pamoja na nchi kadhaa za Magharibi kukata misaada kwa Niger kutokana na mapinduzi ya Julai 26 yaliyompindua Rais Mohamed Bazoum ambaye amekuwa kizuizini nyumbani kwake tangu mapinduzi hayo.
Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (Ecowas) pia iliweka vikwazo na wiki iliyopita iliidhinisha kuanza uingiliaji wa kijeshi kupitia kikosi cha kikanda ambacho tayari kimeanzishwa.
Ecowas ilisema matumizi ya nguvu itakuwa suluhisho la mwisho baada ya njia za kidiplomasia ambazo zilishindwa kufua dafu.
Jana Jumatatu, Ecowas ilikataa pendekezo la Serikali ya kijeshi ya Niger kufanya uchaguzi ndani ya miaka mitatu.
Hata hivyo, AU ilisema inapitia mpango wa utekelezaji wa Ecowas na kutoa wito kwa nchi wanachama wake na jumuiya ya kimataifa kutochukua hatua yoyote ya kuhalalisha Serikali ya kijeshi ya Niger.
"Tunachunguza uamuzi wa Ecowas wa kuandaa vikosi kwa ajili ya kutumwa nchini Niger, na Tume ya Afrika itatathmini athari zake," ilisema taarifa hiyo.
"Tunakataa vikali uingiliaji wowote wa nje wa chama au nchi yoyote katika masuala ya Afrika, ikiwa ni pamoja na makampuni ya kijeshi ya kibinafsi,” imeeleza.