Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

PENTAGON: Mhimili wa mamlaka ya kijeshi Marekani -1

Muktasari:

  • Katika siku ya kawaida ya kazi, takribani watu 23,000 huwa ndani ya Pentagon wakitekeleza majukumu mbalimbali.



Kabla ya satelaiti, mifumo ya kidijitali na vita vya mtandaoni kubadili sura ya mikakati ya kijeshi duniani, kulikuwa na jengo la kipekee lenye pande tano lililokuwa likiinuka taratibu kutoka maeneo ya mabwawa ya Arlington, Jimbo la Virginia nchini Marekani.

Wakati huo halikuvutia hisia za wengi, lakini lilijengwa kuwa moja ya vituo muhimu zaidi vya uongozi wa kijeshi duniani.

Ujenzi huo ulianza mwaka 1941. Wakati huo Jeshi la Marekani lilikuwa limetawanyika kwenye majengo 17 tofauti ndani ya Jiji la Washington D.C na maeneo ya jirani.

Mfumo huo ulisababisha changamoto nyingi za kiutendaji. Maofisa wakuu wa kijeshi hawakuwasiliana kwa urahisi wala kukutana kwa haraka bila kupitia mtandao mgumu wa ofisi zilizopangishwa kwenye maeneo mbalimbali.

Mifumo ya zamani ya mawasiliano ya simu na majengo ambayo kimsingi hayakuwahi kubuniwa kwa ajili ya shughuli za kijeshi, iliibua changamoto kubwa.

Kadri vita vilivyozidi kutanda barani Ulaya na katika ukanda wa Pasifiki, viongozi wa jeshi walitambua kwamba, mazingira ya vita vya kisasa yalihitaji jambo ambalo jeshi la Marekani halikuwa nalo awali; yaani makao makuu ya pamoja yaliyounganishwa kikamilifu, yenye uwezo wa kuratibu na kuelekeza nguvu zote za kijeshi za taifa kutoka sehemu moja.

Brigedia Jenerali Brehon Somervell, aliyekuwa mkuu wa kitengo cha ujenzi cha Jeshi la Marekani, aliandaa mchoro wa awali wa jengo hilo Julai 1941. Kilichoanza kama wazo lililochorwa kwenye karatasi kilikuja kuwa moja ya majengo makubwa na yenye ushawishi mkubwa zaidi duniani katika masuala ya ulinzi na usalama.

Jengo lenye kuhudumia takriban watumishi 23,000 wa kijeshi na kiraia, likiwa na eneo linalofikia futi za mraba milioni 6.5 na mtandao wa korido wenye urefu wa takribani kilometa 28.

Jambo la kuvutia zaidi si ukubwa wa jengo pekee, bali lilibuniwa kwa ustadi wa hali ya juu kiasi kwamba mtu angeweza kutembea kutoka sehemu yoyote ndani yake kwenda nyingine kwa muda usiozidi dakika saba.


Kwa nini umbo la pande tano?

Ubunifu wa pande tano na pembe tano ulitokana na haja ya kutatua changamoto ya kijiografia na kupanga eneo la ujenzi.

Eneo la awali lililotengwa kwa ajili ya makao mapya ya Idara ya Vita ya Marekani lilikuwa limezungukwa na barabara tano zilizopangwa kwa namna iliyofanana kwa kiasi kikubwa na umbo la pentagoni (pembe tano).

Kutokana na hilo, wasanifu majengo waliopewa jukumu la kubuni mradi huo, wakiongozwa na msanifu majengo wa kijeshi la Marekani, George Bergstrom na baadaye chini ya usimamizi wa David Witmer, walichagua mpangilio wa sakafu wenye pande tano ili kutumia kwa ufanisi ardhi iliyokuwapo na kuendana na mipaka ya eneo husika.

Kadiri michoro na tathmini za kitaalamu zilivyoendelea, ilibainika kuwa umbo hilo halikuwa tu suluhisho la changamoto ya eneo, bali pia kuwa na faida kubwa za kihandisi na kiutendaji.

Mpangilio wa jengo wenye pande tano zinazozungukana pamoja na korido zilizounganishwa kwa ustadi, ulirahisisha usafiri wa ndani ya jengo.

Badala ya kutegemea lifti kwa shughuli za kila siku, watumishi walitembea kwa urahisi kati ya ghorofa tano na sehemu mbalimbali za jengo kwa kutumia njia zilizopangwa kwa ufanisi mkubwa.

Mfumo huo ulipunguza msongamano, ukaongeza kasi ya mawasiliano na kurahisisha uratibu wa shughuli za kila siku.

Ujenzi rasmi wa Pentagon ulianza Septemba 11, 1941, tarehe ambayo miongo kadhaa baadaye ilibeba kumbukumbu nzito katika historia ya Marekani. Kwa mshangao wa wengi, mradi huo mkubwa ulikamilika Januari 15, 1943 baada ya kipindi cha miezi 19 pekee.

Wakati likikamilika, Pentagon lilikuwa jengo kubwa zaidi la ofisi duniani. Takribani tani 680,000 za mchanga na kokoto zilizochimbwa kutoka Mto Potomac zilitumika. Zaidi ya wafanyakazi 15,000 walishiriki katika mradi huo, wakifanya kazi kwa zamu mchana na usiku bila kusimama.

Hakuna mradi mwingine wa ujenzi katika historia ya Marekani uliowahi kukamilishwa kwa mchanganyiko wa kasi, ukubwa na kiwango cha uratibu kama ule wa Pentagon.


Uhalisia wa kiutendaji

Pembe zote tano za jengo hilo, kila moja imepewa alama za herufi A hadi E, zikianzia kwenye ua wa ndani wa jengo kuelekea sehemu za nje. Wakati huohuo, korido zimepewa namba kuanzia 1 hadi 10.

Katikati ya Pentagon kuna ua wenye ukubwa wa takribani ekari tano ambao kwa miaka mingi umekuwa chanzo cha simulizi, uvumi na nadharia mbalimbali.

Wakati wa vita baridi, wachambuzi wa kijasusi wa Umoja wa Kisovieti walifuatilia kwa karibu picha za satelaiti za eneo hilo ili kuelewa siri za makao makuu ya kijeshi ya Marekani.

Leo hii, Pentagon ni makao ya Ofisi ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Kamati ya Wakuu wa Majeshi ya Pamoja na pia ni ofisi kuu ya viongozi wakuu wa matawi yote ya Jeshi la Marekani.

Kwa maana halisi, Pentagon ni kitovu kinachosimamia na kuelekeza matumizi ya nguvu za kijeshi za Marekani katika maeneo mbalimbali duniani. Ni kituo cha kimkakati ambacho ndani yake hukusanyika taarifa, mamlaka, utaalamu na uamuzi unaoweza kuathiri mwelekeo wa operesheni za kijeshi katika sehemu nyingi za dunia.


Walio nyuma ya kuta

Ingawa mara nyingi Pentagon hutajwa kwa ukubwa wake, mifumo yake ya usalama au nafasi yake katika uongozi wa kijeshi wa Marekani, ukweli ni kwamba nguvu yake halisi imo kwa maelfu ya watu wanaofanya kazi ndani yake kila siku.

Katika siku ya kawaida ya kazi, takribani watu 23,000 huwa ndani ya Pentagon wakitekeleza majukumu mbalimbali. Kati yao, karibu 3,000 ni maofisa wa jeshi walioko katika utumishi wa moja kwa moja, huku idadi iliyobaki ikijumuisha watumishi wa umma, wataalamu wa kandarasi, washauri wa kiufundi na wafanyakazi wa huduma za usaidizi.

Ndani ya jengo hilo kuna mazingira yanayofanana na mji mdogo unaojitegemea. Kuna migahawa na sehemu nyingi za chakula zinazohudumia maelfu ya watu kila siku.

Hata hivyo, kazi kubwa inayofanyika ndani ya Pentagon ni ambayo haionekani kwa umma moja kwa moja. Asili ya majukumu yake mengi ni ya siri na ya ulinzi mkubwa wa taarifa. Nyaraka za mipango ya kimkakati huwekwa katika viwango vya juu vya usiri.

Kwa mtazamo mmoja, Pentagon inaweza kuelezwa kama mashine kubwa ya kimkakati inayobadilisha taarifa kuwa uamuzi ambao huwa matokeo yanayoathiri siasa, usalama na mahusiano ya kimataifa katika sehemu mbalimbali za dunia.


Uongozi wa kijeshi kimataifa

Kinachofanya Pentagon kuwa ya kipekee ikilinganishwa na majengo mengine makubwa ya serikali, si ukubwa wake wala umaarufu wake, bali nafasi yake kama kitovu cha mtandao mpana wa mamlaka ya kijeshi unaounganisha maeneo mbalimbali duniani.

Kupitia mifumo ya mawasiliano yenye usalama wa hali ya juu, Pentagon imeunganishwa moja kwa moja na karibu kila kambi kubwa ya kijeshi ya Marekani duniani.

Kuanzia Kituo cha Anga cha Ramstein nchini Ujerumani hadi Camp Humphreys nchini Korea Kusini; kutoka Diego Garcia katikati ya Bahari ya Hindi hadi Guantanamo Bay nchini Cuba; taarifa, maelekezo na tathmini za kiusalama husafiri kila sekunde kupitia mtandao huo wa kimataifa.

Pindi hali ya dharura inapojitokeza, iwe ni kurushwa kwa kombora hasimu lililogunduliwa na satelaiti za ulinzi au janga kubwa la kibinadamu linalohitaji msaada wa haraka wa vifaa na usafiri wa kijeshi, vituo vya operesheni vya Pentagon vina uwezo wa kubadilishwa na kupangwa upya ndani ya muda mfupi ili kukabiliana na dharura inayohitajika.

Kituo hicho hufanya kazi saa 24 kwa siku bila kusimama. Maofisa waliopo humo huwa kazini wakati wote, tayari kuwasiliana na vikosi vya nyuklia, kupeleka maagizo kwa makamanda waliopo katika maeneo mbalimbali ya operesheni na kuandaa mikutano ya video yenye usalama wa hali ya juu na washirika wa Marekani walioko upande mwingine wa dunia ndani ya muda wa dakika chache.

Kwa lugha ya wataalamu wa mikakati ya kijeshi, kituo hicho ni kile kinachoitwa “Command and Control Node” au kitovu cha amri na udhibiti.

Tangu kukamilika kwake mwaka 1943, jukumu la Pentagon limeendelea kubadilika sambamba na mabadiliko ya mazingira ya usalama duniani.

Kila mgogoro uliibua mahitaji mapya. Kila kipindi cha vita kilisababisha marekebisho katika muundo wa ndani wa Pentagon. Teknolojia mpya ziliongezwa, mifumo mipya ya mawasiliano ikawekwa na aina mpya za vitisho zikaanza kushughulikiwa.

Hivyo, historia ya Pentagon si ya jengo pekee; ni ya namna mamlaka, taarifa, teknolojia na watu vinavyounganishwa katika sehemu moja ili kuunda uwezo wa kufanya uamuzi unaoweza kubadili mkondo wa matukio duniani.


Pentagon ikiwa na umuhimu mkubwa kiasi hicho, swali muhimu linaibuka: Inalindwaje dhidi ya wingi wa vitisho vinavyoikabili kila siku? Fuatilia toleo lijalo.