Profesa anayepiga pesa kwa kuchomelea vyuma
Muktasari:
- Msomi mwenzake, Profesa Yusuf Jubril, ameeleza kuwa jamii inafikiri mtu akiwa na kiwango kama hicho cha elimu kuna majukumu fulani siyo yake.
Nigeria. Profesa Kabir Abu Bilal, wa chuo kikuu kimoja nchini Nigeria, ameamua kujiajiri kwa kuchomelea vyuma licha ya kuwa ni mtumishi wa taasisi hiyo ya elimu iliyopo Kaskazini mwa Jiji la Zaria nchini humo.
Profesa Bilal ameieleza BBC Swahili kwamba haoni aibu kufanya kazi ya uchomeleaji licha ya kuwa ni profesa.
"Ninapata pesa zaidi kutokana na uchomaji vyuma," amesema Profesa Bilal.
Mwalimu huyo mwenye umri wa miaka 50 anafundisha na kusimamia wanafunzi wa utafiti katika kitivo cha uhandisi katika Chuo Kikuu cha Ahmadu Bello, ambacho ni chuo kikuu kikubwa zaidi nchini Nigeria.
Amefanya kazi chuo kikuu kwa miaka 18 sasa na kuchapisha vitabu kadhaa vya fizikia na uhandisi wa umeme.
Msomi mwenzake, Profesa Yusuf Jubril, ameeleza kuwa jamii inafikiri mtu akiwa na kiwango kama hicho cha elimu kuna majukumu fulani siyo yake.
"Anachofanya si cha kufedhehesha bali ni cha kupongezwa, na natumai wengine watajifunza kutoka kwake," amesema Profesa Jubril.
Prof Bilal anasisitiza kwamba watu hasa wahitimu, wanahitaji kuwa wazi zaidi kuhusu jinsi wanavyoendesha maisha yao.
"Elimu isimzuie mtu kufanya kazi za namna hii, nashangaa kuna watu wenye shahada za kwanza wanaona kazi kama hii ni udhalilishaji," amesema Profesa Bilal.
Alifungua karakana hiyo mwaka 2022 mwaka mmoja baada ya kupandishwa cheo na kuwa profesa.
Imeandaliwa na Mwandishi Wetu kwa msaada wa BBC.