Rais Museveni awaomba radhi Wakenya

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Kenya, Rais anaruhusiwa kugombea mihula miwili tu ya vipindi vya miaka mitano, na kwa sababu hiyo hangeweza kugombea muhula wa tatu isipokuwa katiba ibadilishwe kwanza.

Kampala. Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amewaomba radhi wananchi wa Kenya kutokana na andiko lililochapishwa na Jenerali wa Jeshi la Uganda, Muhokozi Kainerugaba la kumlaumu Rais mstaafu Uhuru  Kenyatta kwa kutogombea muhula wa tatu wa uongozi wa nchi hiyo.

Kupitia ujumbe wake aliouchapisha katika mtandao wa kijamii Jenerali Kainerugamba aliandika

“Shinda yangu pekee na kakangu mkubwa ni kwamba hakugombea muhula wa tatu. Tungeshinda kwa urahisi,” ulisomeka sehemu ya ujumbe huo.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Kenya, Rais anaruhusiwa kugombea mihula miwili tu ya vipindi vya miaka mitano, na kwa sababu hiyo hangeweza kugombea muhula wa tatu isipokuwa katiba ibadilishwe kwanza.

Leo Jumatano Oktoba 5, 2022 kupitia ukurasa wake wa Twitter Rais Museveni aliwapongeza Wakenya kwa kufanya uchaguzi wa amani ambapo William Ruto alitangazwa kuwa mshindi wa urais.

Kupitia taarifa hiyo, Rais Museveni aliwaomba wananchi wa Kenya radhi kufuatia ujumbe uliochapishwa na kiongozi huyo mkuu wa jeshi kupitia mtandao wa kijamii kuhusu uchaguzi wa nchi hiyo.

Amesema si vyema kwa  mtumishi wa umma au raia kwa namna yeyote kuingilia uchaguzi  wa nchi nyingine.

Rais Museveni amesema jukwaa pekee  halali la muingiliano baina ya nchi moja na nyingine ni kupitia Umoja  wa Afrika, au kupitia Jumuiya ya Umoja wa Afrika Mashariki hiyo kilichofanywa na kiongozi huyo wa jeshi kimeleta taswira mbaya kwa utumishi wa umma.

“Hata hivyo, kuna michango mingine mingi mizuri ambayo Mkuu huyu wa jeshi ametoa na bado anaweza kuitoa. huu ni muda wa kuangalia yale mema na kuachana na yale mabaya, niwape pole ndugu zetu Kenya na wananchi wa Uganda waliokerwa na maafisa wao kuingilia mambo ya ndugu yao,”ilisomeka taarifa hiyo.

Rais Museveni amesema anatambua Jenerali Muhoozi ni mwanamajumui wa Afrika lakini alipaswa kutumia njia sahihi za wanamajumui ikiwemo Jukwaa la Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika.