Rais Ramaphosa atangaza umeme janga la kitaifa, upinzani wapinga
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa akizungumza wakati wa hotuba yake ya hali ya taifa 2023 huko Cape Town, Afrika Kusini, Februari 9, 2023
Muktasari:
- Kutokana na uhaba mkubwa wa umeme ulioikumba nchi hiyo kwa miaka kadhaa sasa akisema unaleta tishio kwa uchumi na kijamii huku upinzani ukimjia juu.
Cape Town. Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ametangaza janga la kitaifa kutokana na uhaba wa umeme nchini humo, akisema unaleta tishio taifa hilo lililoendelea zaidi kiviwanda barani Afrika.
Katika hotuba yake ya kila mwaka aliyoitoa bungeni siku ya Alhamisi, Ramaphosa alikiri kuwa wako kwenye mzozo mkubwa wa kinishati huku akiulaumu ufisadi.
Katika hotuba hiyo ilishuhudiwa upinzani mkubwa dhidi ya wabunge wa Chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) waliovuruga shughuli kwa zaidi ya dakika 45 huku wengine wakijaribu kupanda jukwaani.
Pia chama cha upinzani cha Democratic Alliance, kilisema kitapinga tamko la "hali ya maafa" mahakamani, kikidai chama cha Ramaphosa kilitoa kanuni zisizo na maana na kutumia vibaya michakato ya ununuzi wakati wa janga hilo.
Kwa mujibu wa Reuters, Ramaphosa aliweka wazi kwamba uhaba wa umeme umekuwa ukiendelea kwa miaka mingi, ikiwa ni matokeo ya ucheleweshaji wa ujenzi wa vituo vipya vya nishati ya makaa ya mawe.
Pia amesema ufisadi katika kandarasi za usambazaji wa makaa ya mawe, hujuma za uhalifu na kushindwa kurahisisha udhibiti ili kuwawezesha watoa huduma binafsi kuleta nishati mbadala kwa haraka haraka.
"Mgogoro umeendelea kubadilika na kuathiri kila sehemu ya jamii. Ni lazima tuchukue hatua ili kupunguza athari za mgogoro huo kwa wakulima, kwa wafanyabiashara wadogo, kwenye miundombinu yetu ya maji na mtandao wetu wa usafiri," amesema Ramaphosa.
Kukatika kwa umeme kunatarajiwa kupunguza ukuaji wa uchumi katika taifa hilo hadi 0.3% tu kwa mwaka huu.