Rais Ruto, Raila wazidi kuvurugana
Muktasari:
- Ni tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu, Ruto aahidi kufanya kazi na wote
Nairobi. Wakati kiongozi wa Muungano wa Azimio la Umoja, Raila Odinga ameendelea kudai Rais William Ruto hakushinda uchaguzi, wananchi wa Kaunti ya Kisii wamezuia mkutano wa Raila wakitaka apishe ziara ya Rais Ruto kwenye kaunti hiyo.
Mkutano wa Raila ni mwendelezo wa mikutano yake ya kupinga Serikali la Ruto, ulikuwa ufanyike jana kwenye uwanja wa Gusii na umeahirishwa hadi Ijumaa ya wiki hii.
Akizungumza kwenye mkutano uliofanyika Busia juzi na uliongozwa na Raila, aliyekuwa mgombea mwenzake wake, Martha Karua aliushutumu utalawa Rais Ruto kwa kushindwa kutimiza ahadi walizotoa kwenye kampeni.
“Serikali ambayo ‘hatuitambui’ inaongeza mzigo wa kodi kwa wananchi,” alisema Karua ambaye ni kiongozi wa chama cha NARC Kenya.
Pia, Karua alisema Serikali imekuwa ikikusanya kodi ya Sh173 bilioni kila mwezi katika kipindi cha miezi mitano iliyopita.
“Ruto lazima awaeleze Wakenya fedha hizo zimetumika vipi. Walitoa ahadi nyingi wakati wa kampeni ikiwamo kupunguza bei ya vyakula na bidhaa nyingine muhimu, hivyo bado havijatokea,” alisema Karua.
Aliitaka Serikali kuelezea matumizi ya Sh863 bilioni za kodi zilizokusanywa katika kipindi cha miezi mitano iliyopita.
Karua alidai kuwa utawala wa Kenya Kwanza umekazana kuwataka Wakenya walipe kodi wakati viongozi waandamizi serikalini wanafanya ubadhilifu wa fedha za kodi.
“Tunapambana kwa haki ya Wakenya. Nchi ina fedha za kutosha kulisha Wakenya, kuelimisha watoto na kutoa huduma za afya.
“Rushwa imeongezeka na wabunge wa Azimio wananunuliwa na Ikulu,” alidai Karua.
Hata hivyo, mwezi uliopita Katibu Mkuu Hazina, Chris Kiptoo alisema kodi iliyotolewa kati ya Julai na Novemba 2022 ilikuwa Sh789.5 billioni.
Kiptoo alisema kiwango hicho kimepungua Sh32.2 billioni kutimia lengo lililowekwa la makusanyo ya kodi kwa kipindi hicho.
Raila na kuibiwa kura
Kwa upande wake kiongozi wa Muungano wa Azimio la Umoja, Raila Odinga akihutubia kwenye mkutano huo aliendelea kumshutumu aliyekuwa mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati kwa kushindwa kutangaza matokeo ya urais ya majimbo 290 kama sheria inavyotaka.
“Azimio hatutavumilia ‘usaliti’,” alisema. Raila pia alidai yeye na kikosi chake wameapa kuchapisha matokeo mapya ya urais katika siku zijazo.
Aliishutumu IEBC kuwa ilishirikiana na wapinzani wake kumwibia kura.
Pia, Raila alimshabulia Rais Ruto kwa kile alichodai ‘kununua’ wabunge wa upinzani waunge mkono Serikali yake.
“...Tunajua wanapewa Sh50,000 kila mmoja kuunga mkono Serikali,” alidai Raila.
Siasa makanisani
Raila aliishutumu Serikali kwa kupeleka siasa makanisani kila wiki, badala ya kutimiza ahadi walizowapa Wakenya.
Alidai Ruto na timu yake walikuwa bado hawajajiandaa kuongoza nchi.
“Amekuwa kila mara akienda kanisani kujenga hisia kwamba alishinda uchaguzi.Anachofanya Ruto kuusafisha utawala wake makanisani badala ya kueleza namna gani ataboresha maisha,” alidai Raila.
Kalonzo na Katiba, rushwa
Kwa upande wake, kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka alisema mambo si shwari nchini.
“Mambo si shwari nchini baada ya ‘kuibiwa ushindi’ wetu,” alidai Kalonzo.
Alidai kodi kubwa iliyoongezwa inatumika kununua wabunge wa upinzani, wakati Rais akijiandaa kubadili Katiba.
“Nchi imekwenda mwelekeo mbaya. Imekwenda kwenye siasa za rushwa na wabunge wameamua kujiweka sokoni,” alidai Kalonzo.
Kisii wamgomea Raila
Wananchi wa Kaunti ya Kisii waligomea mkutano wa Raila na timu yake ya Muungano wa Azimio la Umoja, wakitaka kiongozi huyo apishe kwanza ziara ya Rais Ruto kwenye kaunti hiyo.
Wanachama wa UDA walimuonya Raila na timu yake dhidi ya kufanya mikutano yake ya kupinga Serikali katika Kaunti ya Kisii.
Viongozi hao walisema uongozi wa Azimio la Umoja unawapotosha wananchi na kuwatenganisha na Serikali.
Mkutano wa Raila ulikuwa ufanyike jana kwenye uwanja wa Gusii na umesogezwa hadi Ijumaa ya wiki hii.
Mwenyekiti wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) katika Kaunti ya Kisii, Kerosi Ondieki alithibitisha kuwa Raila ameahirisha mkutano wa Azimio la Umoja One Kenya katika eneo hilo
Ondieki alisema muungano huo ulifikia uamuzi wa kufanya maandalizi mazuri kabla ya mkutano wa hadhara wa Azimio la Umoja.
Mwenyekiti huyo pia alisema wameiomba sekretarieti ya Azimio la Umoja kumpa muda zaidi Gavana wa Kisii, Simba Arati kufanya mipango kabambe ya ziara ya Raila katika eneo hilo.
Uamuzi huo wa ODM unajiri baada ya baadhi ya wanasiasa washirika wa Rais Ruto kuonya uongozi wa Azimio dhidi ya kufanya mikutano yao katika eneo hilo.
Viongozi wa UDA wakiongozwa na aliyekuwa gavana wa Kisii, James Ongwae na aliyekuwa naibu gavana, Joash Maangi walimtaka Raila kufanya mikutano yake eneo la Luo-Nyanza na kuepuka kuwapotosha Wakisii dhidi ya Serikali ya sasa.
“Sisi kama viongozi wa Gusii tunakataa jaribio hili na kulishutumu kabisa iwezekanavyo. Raila Odinga lazima atuache kama Omogusii, ili tuamue mustakabali wetu wa kisiasa ambao kwa sasa uko na William Ruto,” alisema Maangi.
Kwa upande wake, James Ongwae aliwaomba majemedari wa Azimio kumkubali Ruto kama Rais, ili kumpa muda wa kutosha kutekeleza ahadi zake kwa Wakenya.
“Ninawasihi na kuwasihi watu wetu kutokubali chochote kinachokusudiwa kuweka jamii yetu kuwa ya waasi na kuhatarisha eneo letu la Gusii kutopokea miradi ya kimaendeleo iliyopangwa na Rais Ruto,” alisema Ongwae.
Ongwae alisema kuwa watu wa jamii ya Gusii wako tayari kumpokea Rais Ruto ambaye anatarajiwa kupamba hafla ya kurejea nyumbani kwa Waziri wa Elimu, Ezekiel Machogu.
Ruto kufanya kazi na wote
Wakati Raila akiendelea kulalamika kuhusu kuibiwa kura na kutoitambua Serikali iliyopo madarakani, kwa upande wake Rais Ruto alisema alikutana na viongozi waliochaguliwa kupitia upinzani ambao waliapa kuunga mkono utawala wake.
Pia, Ruto alisema yupo tayari kufanya kazi na viongozi wote bila kujali misimamo yao kisiasa.
Akizungumza mjini Nakuru, Ruto alisema nia yake ni kuunganisha nchi baada ya kipindi kikali cha kisiasa.
Akijibu shutuma za Azimio ambao wamekuwa wakimtuhumu kwa kuvamia upinzani na kuudhoofisha kwa kuwavuna viongozi wake, Ruto alisema hataomba ruhusa ya mtu yeyote au ridhaa ya kushirikiana na viongozi wote kwa malengo ya maendeleo.
Ruto alitangaza kuwa kupitia ushirikiano huo pekee ndiyo Kenya inaweza kupiga hatua kimaendeleo.