Russia yafanya shambulizi kubwa Ukraine

Muktasari:

  • Inadaiwa kuwa wakazi wa Jiji la Kyiv ambao ni Mji Mkuu wa Ukraine, waliamshwa na milipuko kadhaa alfajiri ya leo Jumamosi Novemba 25,2023 ambayo ilisikika kwa zaidi ya saa sita, kabla ya ulinzi wa anga kuimarishwa tena.

Dar es Salaa. Russia imefanya shambulizi kubwa zaidi la ndege zisizo na rubani dhidi ya Kyiv tangu kuanza kwa mzozo baina yake na Ukraine February mwaka jana, Meya wa jiji hilo amesema.

Inadaiwa kuwa wakazi wa jiji hilo waliamshwa na milipuko kadhaa alfajiri ya leo Jumamosi Novemba 25,2023 ambayo ilisikika kwa zaidi ya saa sita, kabla ya ulinzi wa anga jiji hilo kuimarishwa tena.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Uingereza (BBC), maofisa wa Ukraine wamesema zaidi ya ndege 75 za Shahed zinazodaiwa kutengenezwa Iran, zilifyatuliwa risasi katika mji mkuu huo, na kati ya hizo, 74 ziliangushwa.

Hakujaripotiwa kifo chochote katika shambulio hilo, lakini takriban watu watano wanadaiwa kujeruhiwa, akiwemo mtoto wa miaka 11, Meya wa Kyiv, Vitaliy Klitschko amesema na kuongeza kuwa: “Shule ya awali (chekechea) ni miongoni mwa majengo yaliyoharibiwa.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameyataja mashambulizi hayo kuwa ni kitendo cha ugaidi wa makusudi na kusema kuwa nchi yake itaendelea kufanya kazi ya kutafuta uungwaji mkono duniani, katika kile alichosema “kujilinda dhidi ya ugaidi.”

Rais huyo amaendelea kupata uungwaji mkono kutoka mataifa ya Magharibi huku majadiliano kuhusu Ukraine kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya yakiendelea.

Rais Zelensky pia amebainisha kuwa shambulio hilo lilikuja siku ambayo Ukraine ilikuwa ikifanya maadhimisho ya janga la njaa lijulikalo kama Holodomor ya 1932-1933; linalodaiwa kusababishwa na aliyekuwa kiongozi wa Soviet ya wakati huo, Joseph Stalin; ambayo iliua mamilioni ya watu.

Wakati majira ya baridi yakiendelea, ilihofiwa kuwa Russia ingerudia mbinu yake ya kulenga miundombinu ya nishati ya Ukraine. Huku nyumba 16,000 zikiachwa bila umeme katika eneo la kati la Kyiv.

Inadaiwa kuwa mkakati wa Moscow wa mwaka jana ulikuwa kuinyima Ukraine umeme na maji huduma ambazo zilikuwa zikihitajika sana.  Hata hivyo inaelezwa kuwa mamlaka nchini humo zilifanikiwa kufanya ukarabati wa haraka wa mabomba na njia za umeme zilizokuwa zimeharibiwa.


Imeandikwa na Victor Tullo kwa msaada wa mashirika.