Serikali ya Kenya yapinduliwa Agosti-6

Rais Daniel arap Moi

Muktasari:

  • Katika toleo lililopita tuliona namna ambavyo wapanga njama za mapinduzi hawakuwa na tarehe maalumu ya kufanya mapinduzi hayo lakini baada ya uvumi kusambaa kwamba Wakikuyu walikuwa wakipanga njama za kumpindua Rais Daniel arap Moi na kumsimika Mwai Kibaki, uliwalazimisha kuharakisha tarehe hiyo iwe Agosti mosi mwaka 1982.


Katika toleo lililopita tuliona namna ambavyo wapanga njama za mapinduzi hawakuwa na tarehe maalumu ya kufanya mapinduzi hayo lakini baada ya uvumi kusambaa kwamba Wakikuyu walikuwa wakipanga njama za kumpindua Rais Daniel arap Moi na kumsimika Mwai Kibaki, uliwalazimisha kuharakisha tarehe hiyo iwe Agosti mosi mwaka 1982.


Baada ya Rais Daniel arap Moi kuingia kwenye mgogoro wa kisiasa na wanasiasa wengi wa Kenya pamoja na kuharamisha vyama vingi vya siasa kwa kubadili Katiba ya nchi hivyo kujikuta kwenye mgogoro kati yake na baadhi ya wasomi wa nchini mwake, zilianza kusikika tetesi za mapinduzi ya kijeshi kuuondoa madarakani utawala wake.

Uvumi huo ulidokeza kuwa mapinduzi yalipangwa kufanyika wiki ya mwisho ya Julai 1982 lakini kwa kuwa sehemu ya habari zilizosambaa zilibainika kuwa za uongo, basi na uvumi huo haukutiliwa maanani.

Private Hezekiah Ochuka alipanga mkutano wa siri mwishoni mwa Julai 1982 karibu na Shamba la Umoja kujadili utekelezaji wa mpango wa kuipindua Serikali ya Rais Moi.

Katika mkutano mmoja kulikuwa na mjadala mkali wa nani angekuwa mwenyekiti wa kikundi kilichojiita Baraza la Ukombozi wa Watu (PRC) wa Kenya ili achukue nafasi ya urais baada ya mapinduzi. Yeye alisisitiza kwamba ni lazima awe mwenyekiti wa kikundi hicho.

Wengine waliotamani kuupata wadhifa huo ni wawili ambao ni Joseph Ogidi Obuon na Pancres Oteyo.

Kwa upande wake, Obuon alisema yeye ndiye anastahili kuwa mwenyekiti kwa sababu aliingiza wafuasi wengi katika kikundi hicho. Ochuka alitishia kwamba wanajeshi wote aliowasajili kwenye kikundi hicho wangeachana na mpango wa kuipindua Serikali iwapo hatochaguliwa kuwa mwenyekiti.

Obuon na Ochuka walikuwa na mabishano makali ambayo nusura yaangukie kwenye vita kuhusu uenyekiti hadi Oteyo aliponasa na kumshauri Obuon kumwachia Ochuka uenyekiti lakini wangemuua baada ya mapinduzi.

Ochuka alikuwa mwanajeshi mjanja kwa hiyo alijua kilichojificha nyuma ya akili za Obuon na Oteyo. Mara moja alihakikisha anaungwa mkono. Aliungwa mkono na rafiki wa zamani wa kisiasa wa Obuon na inaaminika kuwa rafiki huyo wa zamani hata alimpa shilingi milioni mbili na gari. Pia, alifanikiwa kuiba baadhi ya vifaa vya mawasiliano vya kijeshi ambavyo alikuwa ameviweka katika nyumba binafsi jijini Nairobi iliyokuwa kilomita chache kutoka katikati mwa jiji hilo kubwa ukanda wa Afrika Mashariki.

Mwishoni mwa Julai 1982, Ochuka alifanya mkutano wa siri katika uwanja vya mpira uliokuwapo karibu na Umoja Estate na kutoa maelezo jinsi mapinduzi yanapaswa kutekelezwa. Katika mkutano huo, Ochuka aliwaambia waliohudhuria kuwa anaungwa mkono na Uganda, Tanzania na Sudan ambao wapo tayari kutuma wanajeshi wao mipakani ili kukabiliana na upinzani wowote utakaojitokeza.

Alienda mbali zaidi na kudai kwamba alikuwa na baraka za Urusi ambayo ingetuma meli ya Kisovieti pwani ya Kenya ili kuongoza mapambano dhidi ya uvamizi wowote kutoka nje.

Mapinduzi hayo yalipangwa kufanyika wakati idadi kubwa ya vitengo vya jeshi vikiwa mbali na Nairobi kwenye mazoezi yaliyokuwa yakifanyika katika mji wa Lodwar.

Ilipotimu saa tisa alfajiri ya Agosti mosi mwaka 1982, Ochuka na wenzake walianza kwa kukiteka Kituo cha Jeshi la Anga (KAF) cha Eastleigh nje kidogo ya Jiji la Nairobi, baadaye kidogo kituo kingine cha jeshi hilo, Embakasi.

Kabla ya saa 12 asubuhi Private Ochuka na Sajenti Pancras Oteyo Okumu ambaye alikuwa mjumbe wa PRC, walivamia kituo cha redio cha Sauti ya Kenya (VoK) katikati mwa Jiji la Nairobi.

Alfajiri ya siku hiyo Ochuka alikuwa na shughuli nyingi akimsaka mtangazaji maarufu wa redio Leonard Mambo Mbotela ili akatangaze mapinduzi hayo. Aliamini kuwa ingeaminika ameipindua Serikali ikiwa angesikia redioni.

Kutokana na hilo, Mambo Mbotela akawa mmoja wa Wakenya waliojikuta katikati ya sakata hilo mapema asubuhi ya siku hiyo baada ya kufuatwa nyumbani kwake na wanajeshi hao, wakamchukua kwa lazima kwenda kituo cha redio na kumlazimisha atangaze kuwa Serikali ya Rais Moi imepinduliwa na jeshi.

Walipomfikisha studio alikalishwa kwenye kiti kisha Ochuka akachukua karatasi na kalamu akaandika tangazo kisha akamwamuru Mbotela kutangaza alichokiandika.

“Hamjambo wananchi wa Kenya? Mimi ni Leonard Mambo Mbotela. Hii ni Sauti ya Kenya. Nawafahamisha kwamba Serikali ya Mzee Daniel arap Moi imepinduliwa. Na hapa nilipo niko na Bwana Hezekiah Ochuka na viongozi wengine. Kwa hiyo anasema ya kwamba mtulie majumbani. Kila mtu atulie nyumbani. Mahabusu wote wafunguliwe na kuanzia sasa polisi wote ni raia. Wananchi wasitangetange. Mtulie nyumbani. Na mengi mtafahamishwa baadaye,” alisoma Mbotela.

Vichekesho zaidi vilionekana pale wanajeshi walipofika kwenye studio za utangazaji zilizopo kando mwa Barabara ya Harry Thuku. Katika hali ya kawaida, mapinduzi yangeambatana na muziki wa kijeshi uliochaguliwa kwa uangalifu. Ochuka na timu yake hawakuwa na muziki wowote wa kijeshi.

Ulifika wakati wakamlazimisha mtangazaji aweke mziki wa jeshi ili wananchi wausikie. Yeye akawaambia hajui ataupata wapi muziki huo. Lakini akawaambia kuna wimbo wa Tabu Ley. Lakini badala yake wakachagua nyimbo za Reggae za Bob Marley na Jimmy Cliff.

Wakati wote huo Mambo Mbotela alikuwa chini ya ulinzi wa Private Hezekiah Ochuka na Sajenti Pancras Oteyo Okumu ambao ndio walikikamata kituo hicho cha redio.

Baada ya Mambo Mbotela kutangaza kuwa Private Ochuka ametwaa madaraka ya nchi, Ochuka aliwaambia wafuasi wake: “Nimekuwa Rais...ulimwengu wote utasoma na kusikia habari zangu. Nimeweka historia.”

Ochuka aliamini kwamba mambo yangekwenda kama alivyopanga. Aliendelea kuwaambia waasi wenzake kuwa nchi za Uganda, Tanzania, Sudan na Urusi zilikuwa zinaunga mkono mapinduzi hayo na kwamba misaada ya kijeshi ingeletwa kwa ajili yao ili kuisimika Serikali mpya.

Muda mfupi baada ya tangazo hilo kusomwa redioni, akiwa bado chini ya ulinzi wa wanajeshi waasi, Mambo Mbotela alitangaza tena kwamba Jiji la Nairobi limegeuka kuwa uwanja wa vita kwa hiyo watu mnatakiwa kutulia majumbani mwenu.

Kisha Ochuka akamwambia Mambo Mbotela kuwakusanya wananchi ili wajiunge katika harakati za kuikomboa Kenya kutoka kwenye mikono ya dhuluma ya Moi.

Wakati huohuo, vikosi vya waasi vilivamia Chuo Kikuu cha Nairobi, na kuwataka wanafunzi wajiunge nao kwenye mpango wao.

Saa moja asubuhi Wakenya walipoamka na kusikiliza muziki wa Jimmy Cliff na Bob Marley na kufuatiwa na tangazo la mapinduzi ya kijeshi lililorudiwa mara kadhaa kwenye kituo cha redio badala ya taarifa ya habari kama ilivyokuwa imezoeleka.

Mambo Mbotela aliendelea kuwatangazia Wakenya hivi kuwa “ninapozungumza nanyi sasa, nchi yetu iko chini ya udhibiti kamili na thabiti wa majeshi yetu. Hatua zote za uangalifu kadiri iwezekanavyo zimechukuliwa ili mapinduzi yasiwe na umwagaji damu.”

Dakika 10 baadaye Mbotela alitangaza tena: “Katika kipindi cha miezi sita tumeshuhudia kwa karaha kuanzishwa kwa mfumo wa chama kimoja bila ridhaa ya wananchi na raia wakikamatwa ovyo na kuwekwa kizuizini bila hatia wala kushtakiwa, kudhibitiwa kwa vyombo vya habari, vitisho kwa watu binafsi na ukiukwaji wa jumla wa mambo ya msingi ya haki za binadamu.”

Muda mfupi baadaye akatoa tangazo jingine akisema “Serikali imekuwapo tu kutisha watu. Ufisadi, ukabila na upendeleo wa viongozi umefanya maisha yasivumilike katika jamii yetu. Uchumi wa nchi hii umedorora kutokana na kukithiri kwa rushwa na ufisadi.”

“Majeshi yetu yametii wito wa wananchi kuikomboa nchi yetu kwa mara nyingine tena kutoka mikononi mwa uonevu na unyonyaji ili kurejesha uhuru, utu na haki za kijamii kwa watu,” alisikika Mambo Mbotela redioni.

Wakati wote huo akisoma matangazo hayo, Mbotela alikuwa chini ya ulinzi mkali wa wanajesh hao waasi.

Je, nini kiliendelea? Usikose toleo lijalo.