Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yajibu azimio la kamati Bunge la Ulaya kuhusu msaada wa Tanzania

Muonekano wa ndani katika Bunge la Ulaya. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Azimio hilo lilipitishwa Mei 3, 2026 katika kikao cha pamoja cha kamati hizo, ambapo wabunge 81 waliunga mkono mapendekezo hayo, mmoja alipinga na wanne hawakuwa na msimamo.

Dar es Salaam. Wakati Kamati za Mambo ya Nje na Maendeleo za Bunge la Ulaya zikipitisha mapendekezo kusimamisha msaada wa maendeleo wa euro 156 milioni (Sh440 bilioni) kwa Tanzania, Serikali imefafanua kuhusu hatua hiyo.

Wabunge hao walipitisha azimio hilo kwa kura Mei 3, 2026 mjini Brussels, Ubelgiji katika kikao cha pamoja cha kamati hizo, ambapo wabunge 81 waliunga mkono mapendekezo hayo, mmoja alipinga na wanne hawakuwa na msimamo.

Mapendekezo hayo ya sasa, yanatarajiwa kuwasilishwa katika hatua zinazofuata za mchakato wa maamuzi ndani ya Bunge la Ulaya kuhusu utekelezaji wa mpango huo wa maendeleo kwa Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa za kamati hizo, hatua hiyo imechochewa na wasiwasi kuhusu hali ya haki za binadamu, utawala bora, uhuru wa maoni na maendeleo ya demokrasia nchini Tanzania.

Kufuatia hatua hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania imetoa taarifa kwa umma kufafanua suala hilo, ikisema ni sehemu ya taratibu za ndani za Bunge la Ulaya katika kufanya uamuzi. Lakini hatua ya mwisho haijafikiwa

“Katika hatua hii, ni Kamati ya Mambo ya Nje na Kamati ya Maendeleo pekee ndizo zilizojadili na kupigia kura mapendekezo yanayohusu Tanzania,” taarifa hiyo imeeleza.

Imesema mchakato huo bado haujakamilika kwani mapendekezo yaliyopitishwa ngazi ya kamati yanapaswa kuwasilishwa kwenye kikao cha Bunge zima la Ulaya, linalojumuisha zaidi ya wabunge 700, kwa ajili ya mjadala na uamuzi.

 “Ni muhimu kufahamu kwamba uhusiano kati ya Umoja wa Ulaya na nchi washirika wake, ikiwemo Tanzania, unaendeshwa kupitia Tume ya Ulaya, ambayo ndiyo chombo cha utendaji cha Umoja wa Ulaya,” taarifa hiyo imeeleza.

 Serikali imesema kama ilivyo katika mifumo mingi ya Bunge, mapendekezo yanayopitishwa na kamati za Bunge au na Bunge lenyewe huwasilishwa kwa taasisi husika za kiutendaji kwa ajili ya kuzingatiwa na kufanyiwa kazi kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Hivyo, taarifa hiyo ya Serikali imeeleza kuwa na mapendekezo yaliyopitishwa na kamati za Bunge hayapaswi kutafsiriwa kuwa ni uamuzi wa moja kwa moja unaobainisha mustakabali wa mahusiano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya.

“Suala hili bado liko ndani ya taratibu za Umoja wa Ulaya na halijafikia hatua ya mwisho ya maamuzi. Wizara inapenda kuuhakikishia umma kwamba uhusiano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya unaendelea kuwa imara na unazidi kustawi katika maeneo mbalimbali yenye masilahi ya pamoja,” taarifa hiyo imeeleza.

Pamoja na hayo, taarifa hiyo imeeleza kuwa Tanzania na Umoja wa Ulaya zinafurahia ushirikiano wa muda mrefu uliojengwa kupitia mazungumzo, ushirikiano na kuheshimiana, unaoungwa mkono na mifumo imara ya mashauriano iliyoanzishwa vyema.

“Serikali ya Tanzania inaendelea kuwa na dhamira ya kuimarisha zaidi ushirikiano wake wa muda mrefu na Umoja wa Ulaya kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili na kwa ajili ya kufanikisha malengo ya pamoja ya maendeleo,” taarifa hiyo imeeleza.


Mapendekezo ya wabunge

Mwaka jana, Tume ya Ulaya ilisimamisha kiasi cha euro 156 milioni (Sh440 bilioni) kufuatia shinikizo na malalamiko kutoka Bunge la Ulaya na ikaahidi kufanya marekebisho katika namna fedha hizo zitakavyotolewa.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge wa Bunge la Ulaya (MEPs), akiwemo Barry Andrews ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo, wanaamini kuwa Tume hiyo haijashughulikia ipasavyo changamoto zilizobainishwa.

Tume ya Ulaya imependekeza usimamizi wa fedha hizo uondolewe chini ya udhibiti wa moja kwa moja wa Serikali.

Rasimu ya azimio linalokosoa pendekezo la Tume ya Ulaya lilipata uungwaji mkono kutoka vyama mbalimbali katika Kamati za Maendeleo na Mambo ya Nje.

Bunge zima la Ulaya linatarajiwa kupigia kura azimio hilo mwezi huu, ingawa haliwezi kuilazimisha Tume ya Ulaya kubadili msimamo wake.

"Tume ya Ulaya na Huduma ya Nje ya Umoja wa Ulaya (EEAS) zimeshindwa kuonyesha kwa ufanisi kwamba zimeyashughulikia masuala halisi yaliyokuwa yameibuliwa kuhusu Tanzania," inaeleza rasimu hiyo.

Hata hivyo, Mei mwaka huu, Tanzania iliahirisha ziara rasmi iliyokuwa imepangwa kufanywa na wabunge wa Bunge la Ulaya (MEPs) kutoka Kamati Ndogo ya Haki za Binadamu, hatua iliyozua malalamiko kutoka kwa Mounir Satouri, mmoja wa wabunge wa kundi la Green katika Bunge la Ulaya.

"Tunasikitishwa na ukosefu wa utayari wa mamlaka za Tanzania kushiriki mazungumzo ya dhati na yenye nia njema, hasa katika mazingira ya kuzorota kwa hali ya haki za binadamu na hatua za kukandamiza upinzani wa kidemokrasia," alisema Satouri.