Spare; Kitabu cha Prince Harry kitakacholeta balaa

Muktasari:

  • Prince Harry (wa sita kwa kiti cha enzi cha ufalme wa Uingereza), ameandika kitabu kinachosubiriwa duniani kote tangu kilipotangazwa kwa mara ya kwanza mwaka jana. Kitabu hicho kilichopewa jina la ‘Spare’ kitazinduliwa Januari 10, mwakani.

Prince Harry (wa sita kwa kiti cha enzi cha ufalme wa Uingereza), ameandika kitabu kinachosubiriwa duniani kote tangu kilipotangazwa kwa mara ya kwanza mwaka jana. Kitabu hicho kilichopewa jina la ‘Spare’ kitazinduliwa Januari 10, mwakani.

Katika taarifa iliyotolewa Alhamisi iliyopita, wachapishaji wa kitabu hicho, Penguin Random House, ilieleza kuwa kitabu hicho kina kumbukumbu za kifo cha ‘kutatanisha’ cha mwaka 1997 cha mama wa Prince Harry, Princess Diana na picha iliyofuata ya Harry na kaka yake wakitembea nyuma ya jeneza la mama yao huku ulimwengu ukiwatazama kwa huzuni na hofu. “Wakati Princess Diana anazikwa, mabilioni ya watu walikuwa wakijaribu kuwaza kile watoto wake walichokuwa wakiwaza na kuhisi na maisha yao ya baadaye,” taarifa hiyo inasomeka kwa sehemu na kuongeza, “Mwishowe, hii ndiyo hadithi ya Harry”.

Wafuatiliaji wa masuala ya ufalme wa Uingereza na umma kwa ujumla wamesikia sana habari za kitabu hicho tangu kilipotangazwa kwa mara ya kwanza Julai mwaka jana. Saa chache tu baada ya tangazo la juzi Alhamisi, ‘Spare’ kilikuwa katika orodha ya vitabu kumi bora kwa wauzaji bora wa vitabu mtandao duniani Amazon.

Prince Harry tayari ameweka wazi nia ya kujadili maisha yake ya kibinafsi wakati yeye na mkewe mzaliwa wa Marekani, Meghan, walipohojiwa na mtangazaji wa televisheni maarufu wa Marekani, Oprah Winfrey, Machi mwaka jana.

Wanandoa hao walizungumza juu ya kutokuwa na furaha kwa Meghan na maisha yake mapya huko Uingereza, ubaguzi wa rangi unaodaiwa kukithiri ndani ya familia ya kifalme, hofu ya Harry kwamba maisha ya mkewe yanaweza kuhatarishwa ikiwa wangebaki katika nchi yake ya asili.

Mwaka 1992 Princess Diana alifanya kazi na mwandishi Andrew Morton kuandika kitabu chake kilicholeta mtafaruku katika ufalme wa Uingereza kinachoitwa ‘Diana: Her True Story’ ambacho ndani yake alielezea kwa kirefu ndoa kati yake na Mfalme Charles III isivyokuwa ya furaha na yenye misukosuko mingi.

Harry na Meghan walijiuzulu kutoka katika wadhifa wake wa kifalme mwaka 2020 na kuhamia Marekani. Wamezindua mipango mingi pamoja, ikiwamo uzalishaji wa Netflix na Shirika lisilo la faida la Archewell Foundation.

Tangu Prince Harry na Meghan Markle walipotoka katika familia ya kifalme, wenzi hao wamekuwa wakijifurahisha nyumbani kwao Montecito, California na watoto wao Archie na Lilibet Diana Mountbatten-Windsor katika nyumba mpya waliyoinunua kwa Dola milioni 14.7 (sawa na Sh34.1 bilioni).

Lilibet Diana ni mjukuu wa 11 wa hayati Malkia Elizabeth II na ni wa nane katika safu ya kurithi kiti cha enzi cha Ufalme wa Uingereza.

Nyumba hiyo ya kifahari ambayo imejengwa kwenye eneo lenye ukubwa wa futi za mraba 18,671 ina vyumba tisa na bafu 16. Huduma zinazopatikana katika nyumba hiyo ni vyumba vya maktaba, mazoezi, chumba cha michezo na ukumbi mdogo wa muziki. Kwa nje kuna nyumba ya wageni yenye vyumba viwili vya kulala na bafu.

Alipoulizwa na Oprah Winfrey, ni neno gani atatumia kuelezea maisha yake mapya ya Pwani ya Magharibi mwa Marekani, Meghan alisema ‘amani’, akielezea zaidi kuwa sehemu bora ya maisha yake ni kuishi maisha halisi ya amani ya moyo. Aliongeza, “Hili ni la msingi sana, na linatosheleza. Tumejishusha kufanya mambo ya msingi.”

Katika mahojiano hayo pia Meghan alisema kuna wakati maisha yalimsonga na kuwa magumu sana katika familia ya kifalme kiasi kwamba ‘hakutaka tena kuendelea kubaki hai’.

Jambo baya Zaidi, alisema, ni kwamba hakupata msaada hata alipouomba.

Alisema kibaya zaidi ilikuwa wakati mtu mmoja wa familia hiyo alipomuuliza Harry jinsi mtoto watakayemzaa atakuwa na ngozi nyeusi.

Kwa upande wake, Prince Harry alisema baba yake, Prince Charles hakupokea simu zake alipogundua kwamba alikuwa na mpango wa kujiondoa kutoka familia ya kifalme. Wawili hao walizungumza masuala mbalimbali, ikiwamo ubaguzi wa rangi, uhusiano wao na vyombo vya habari, afya ya akili na mambo katika familia ya kifalme. Pia walitangaza ujio wa mtoto wao wa kike.

Meghan alisema alianza kuhisi upweke sana wakati alipowekewa vikwazo dhidi ya mambo aliyotaka kuyafanya maishani mwake.

Alisema wakati fulani alishindwa kwenda kazini kwa miezi kadhaa kwa sababu ya vikwazo hivyo.

Alipoulizwa iwapo aliwahi kufikiria kuhusu kujidhuru au kuwa na mawazo kama hayo, alisema hilo lilikuwa jambo la wazi kabisa.

“Lilikuwa ni jambo bayana na la kutisha sana. Sikujua msaada ningeupata wapi, hali ilianza kuwa mbaya mara baada ya ndoa yetu Mei 2018.

“Familia ya ufalme ilikuwa na wasiwasi kuhusu ngozi ya mwanangu. Niligundua sikuwa nikichungwa bali pia walikuwa tayari kusema uongo ili kuwakinga baadhi ya watu wa familia ya kifalme na siyo mimi na Harry.”

Akiungana na mkewe, Harry alizungumzia uhusiano wake na watu wengine wa familia ya kifalme, akiwamo bibi yake, Malkia ulikuwa mzuri sana na wawili hao huzungumza kila mara, lakini uhusiano kati yake na baba yake, Prince Charles ulivurugika.Harry alisema ataendelea kumpenda baba yake, lakini alisikitishwa na kile anachokiita kuumizwa sana kunakomhusisha kaka yake, Prince William na sasa wako mbalimbali.

Baada ya familia ya Kifalme kusitisha ufadhili wao kwa Harry na Meghan, tajiri mmoja wa Marekani, Tyler Perry aliwapa hifadhi ya makao na ulinzi katika eneo la California mwaka jana.

Perry ni mtengenezaji filamu mashuhuri, mchekeshaji, mwigizaji, mzalishaji wa vipindi na mtunzi, kazi ambazo ndiyo chanzo cha utajiri wake.

Ingawa Perry hajawahi kutoa sababu ya kumsaidia Harry na Meghan, Harry alisema:

“Wasiwasi mkubwa ulikuwa ni kwamba wakati tuko Canada katika nyumba ya mtu mwingine, niliarifiwa ulinzi utaondolewa ndani ya kipindi kifupi, (kwa sababu ya Uviko-19) nikafikiria mipaka inaweza kufungwa, ulinzi wetu utaondolewa na hakuna anayejua mipaka ikifungwa itafunguliwa lini.”

Harry amefanya kama Edward VIII, aliyeachana na ufalme wa Uingereza kwa sababu ya mwanamke Mmarekani, Wallis Simpson Alhamisi ya Desemba 10, 1936, aliyefanya hivyo Jumanne ya Machi 31, 2020 kwa sababu ya mwanamke Mmarekani, Meghan.

Wafuatiliaji wa mambo wanasema kitabu hicho ni bomu kwa ufalme wa Uingereza.

Fuatilia sehemu ya mwisho kesho