Tetemeko lingine laikumba Afghanstan, lajeruhi watu 100
Muktasari:
- Zikiwa zimepita siku nne tu tangu Afghanistan kukumbwa na tetemeko la ardhi na kusababisha vifo Zaidi ya 1,000, tetemeko lingine lenye ukubwa wa 6.3 limeikumba nchi hiyo na kujeruhi zaidi ya watu 100.
Afghanistan.
Tetemeko hilo jipya la kipimo cha 6.3 lilipiga mwendo wa saa 05:10 kwa saa za ndani leo Jumatano, kilomita 28 Kaskazini mwa jiji la Herat.
BBC imeripoti kuwa zaidi ya watu 100 waliojeruhiwa, wamepelekwa hospitalini, maofisa wa afya wamesema.
Athari zaidi bado hazijabainika, kwani wananchi wengi walikuwa wamelala nje baada ya nyumba zao kuharibiwa Jumamosi.
Mashirika ya misaada yamesema pia kuna uhaba wa blanketi, chakula na vifaa vingine.
Shahidi aliyeshuhudia eneo la kati la Herat, ambako baadhi ya nyumba bado zimesimama, alisema aliamka na kupiga kelele na kukimbia nje ya nyumba yake.
"Nilikuwa katika usingizi mzito kwa sababu sikuwa nimelala siku zilizopita," ameiambia BBC.
"Sijawahi kuhisi kifo," amesema, akiongeza kwamba alikimbia bila viatu hadi viunga vya jiji, ambapo wengi wamekuwa wakilala kwenye mahema tangu tetemeko la kwanza.
Tetemeko la ardhi la Jumamosi asubuhi lilipiga Zindajan, wilaya ya mashambani kilomita 40 kutoka Herat.
Picha kutoka vijijini zinaonyesha nyumba, ambazo hazikuweza kustahimili mitetemeko hiyo, zikiwa zimeharibiwa na kuwa vifusi.
Afghanistan hukumbwa na matetemeko ya ardhi mara kwa mara hususani katika safu ya milima ya Hindu Kush kwani iko karibu na makutano ya miamba ya Eurasia na India.