Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Trump adai Putin anataka wakutane, maandalizi yanaendelea

Muktasari:

  • Tangu kutangaza operesheni zake za kijeshi nchini Ukraine, Russia imetwaa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Ukraine ikiwemo Donetsk, Luhansk, Kherson, Pokrovisk na Crimea iliyotwaliwa mwaka 2014.

Florida. Rais mteule wa Marekani, Donald Trump amesema maandalizi ya kikao chake na rais wa Russia, Vladimir Putin yameanza kufanyika huku akisema kiongozi huyo anataka kukutana naye.

Trump alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na vyombo vya habari katika makazi yake yaliyopo Mar-a-Lago nchini humo, huku akigoma kuweka wazi ni wapi yatafanyikia mazungumzo hayo.

“Anahitaji (Putin) kukutana na mimi na tumeshaanza kuweka mipango sawa,” amesema Trump.

Trump, ambaye anatarajia kuingia ofisini Januari 20, mwaka huu amekuwa mkosoaji mkubwa wa Rais wa sasa wa Marekani, Joe Biden kuhusiana na namna anavyoshughulikia vita hiyo.

Pia, amekuwa akilaani kitendo cha Marekani kuipatia Ukraine misaada ya kijeshi na silaha, huku wakati wa kampeni zake za urais akiahidi kwamba akichaguliwa kuongoza taifa hilo atamaliza vita ya Russia na Ukraine.

Pia, alimueleza kiongozi wa Ukraine, Volodymyr Zelensky kama “mfanyabiashara mzuri duniani,” kutokana na uwezo wake wa kuyashawishi mataifa ya magharibi kumpatia misaada ya kijeshi na kiuchumi.

Pamoja na kuwa hakuanika mbinu atakayoitumia kiongozi huyo kumaliza vita hiyo, vyombo vya habari vimeripoti kuwa mpango wa Trump ni kumaliza vita hiyo katika hatua iliyofikia.

Kutokana na kauli hiyo ya Trump, mteule wake nchini Ukraine, Keith Kellogg, alisema lengo lake ni kuhakikisha vita kati ya Russia na Ukraine inamalizwa ndani ya siku 100 baada ya kuapishwa.

Pia, alimkosoa Biden kwa kutochukua hatua yoyote tangu mwaka 2022 Russia ilipoanzisha ilichokiita operesheni zake za kijeshi nchini Ukraine.

Mazungumzo kati ya Russia na Ukraine ya mwaka 2022, yaligonga mwamba baada ya pande zote kutokubaliana baada ya kutuhumiana kwamba kila upande umeweka masharti yasiyotekelezeka.

Kwa mujibu wa Putin, wawakilishi wa Ukraine katika mazungumzo hayo walikuwa wameshakubaliana na baadhi ya masharti yake, ghafla wakageuka na kuamua kususia mazungumzo hayo.

Hata hivyo, baadaye Victor Nuland ambaye ni Ofisa Mwandamizi Mstaafu katika Ikulu ya Marekani, alianika kuwa Ukraine ilijiondoa katika mazungumzo hayo ya mwaka 2022, baada ya kushauriwa na mataifa ya magharibi kuwa isikubaliane na masharti hayo ya Russia.

Kuhusu suala hilo, Shirika la Habari la Russia, TASS lilimnukuu Msemaji wa Ikulu ya Russia ya Kremlin, Dmitry Peskov akisema kuwa Russia haijapokea mwaliko rasmi wa mazungumzo kutoka nchini Marekani kuhusiana na mzozo kati ya nchi hiyo na Ukraine.

Pescov alisema: “Huenda ikawa ni kweli ngoja tusubirie akiingia Ikulu” huku akisisitiza kuwa ni jambo ambalo rais Putin angetamani kulifanya ni mazungumzo yenye lengo la mzozo huo.

Japo alisema Kremlin haijapokea taarifa wala mwaliko wowote kuhusiana na mazungumzo hayo kutoka Marekani, masharti ya taifa hilo hayajabadilika ikiwemo Ukraine kutojiunga katika Jumuiya ya Kujilinda ya Nato.

Pia, inaitaka Ukraine kuondoa vikosi vyake eneo la Kursk nchini Russia, Zelenskyy kuitisha uchaguzi utakaomuweka madarakani kihalali kwa kile ambacho Putin alidai kiongozi huyo yuko madarakani kwa sheria ya Kijeshi (Martial Law).

Pia, Russia inaitaka Ukraine kuachana na mpango wa urutubishaji wa nyuklia sambamba na kutumia silaha za Marekani na mataifa ya magharibi kushambulia maeneo ya Russia.

Tangu kutangaza operesheni zake za kijeshi nchini Ukraine, Russia imetwaa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Ukraine ikiwemo Donetsk, Luhansk, Kherson, Pokrovisk na Crimea iliyotwaliwa mwaka 2014.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.