Upinzani kuandamanana kupinga matokeo Uchaguzi Zimbabwe
Kiongozi wa chama cha upinzani cha CCC nchini Zimbabwe, Nelson Chamisa
Muktasari:
- Chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe kimeitisha maandamano ya nchi nzima leo Ijumaa kutaka marudio ya uchaguzi kikisema uchaguzi uliofanyika hivi karibuni na kumpa ushindi Rais Emmerson Mnangagwa haukuwa huru na haki.
Zimbabwe. Chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe kimeitisha maandamano ya nchi nzima leo Ijumaa kutaka marudio ya uchaguzi kikisema uchaguzi uliofanyika hivi karibuni na kumpa ushindi Rais Emmerson Mnangagwa haukuwa huru na haki.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku moja baada ya Rais Mnangagwa kusema uchaguzi huo ulikuwa halali na kuonya kuwa kutakuwa na msako mkali dhidi ya yeyote anayeeneza machafuko.
"Ninaonya yeyote ambaye ataleta machafuko, tuko tayari kukabiliana naye. Yeyote anayehubiri matamshi ya chuki atawajibika kwa matamshi yake, magereza yetu hayajajaa," alisema Mnangagwa
Mnamo Jumamosi wiki iliyopita, tume ya uchaguzi nchini humo, ilisema Mnangagwa amepata takribani asilimia 53 ya kura, na kumwacha kiongozi wa chama cha wananchi (CCC) Nelson Chamisa katika nafasi ya pili kwa asilimia 44.
Licha ya Chama tawala cha Rais Mnangagwa cha ZANU-PF kutajwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa bunge lakini kilipungukiwa na theluthi mbili ya wingi wa kura zinazohitajika kubadilisha katiba.
Wachambuzi wametilia shaka uchaguzi huo ambao ulitawaliwa na mapungufu kadhaa ikiwemo kukamatwa kwa wasimamizi katika vituo vya kupigia kura.
Chama tawala Zanu-PF kimesema hakukuwa na kasoro zozote na Rais Mnangagwa amemtaka yeyote mwenye malalamiko kwenda mahakamani.
Chama hicho cha upinzani kimeitisha maandamano katika majimbo 10 nchini humo na kuwataka wanaharakati kuzindua kampeni mtandaoni na kushiriki kutoa ushahidi wa kasoro zilizojotokeza wakati wa upigaji kura.
"Tunawahimiza watu wawe na amani, Maandamano haya ni ya wananchi,” amesema msemaji wa CCC, Promise Mkwananzi.
Chama hicho kinazitaka nchi nyingine za Afrika kuingilia kati na kusuluhisha mzozo wake na chama tawala, lakini wachambuzi wanasema uwezekano wake wa kutengua matokeo ya uchaguzi kupitia mahakama ni mdogo kutokana na mfumo kuonekana kuwa unadhibitiwa na chama tawala.
Kwa mujibu wa katibu ya nchini humo, chama cha CCC kina siku saba za kukata rufaa mahakamani tangu tume ya uchaguzi ilipotangaza matokeo hayo.
Imeandaliwa na Albetina Menas