Wanaharakati wahoji mawaziri kutumia Sh16.5 bilioni kupanda miti

Muktasari:

  • Wanaharakati kutoka kundi la linalojiita ‘Operesheni Linda Jamii,’ limekosoa hatua iliyochukuliwa na Serikali ya Kenya, ya kuwatumia Mawaziri kuongoza shughuli ya upandaji miti nchini humo, wakidai hatua hiyo ni sehemu ya matumizi mabaya ya fedha za umma.

Dar es Salaam. Wanaharakati nchini Kenya wameikosoa Serikali ya nchi hiyo kwa kutumia Ksh1 bilioni (inakaribia Sh16.5 bilioni), kwa ajili ya kuwatuma mawaziri kuongoza kampeni ya upandaji miti, wakisema hayo ni moja ya matumizi mabaya ya fedha za umma.

Mtandao wa Taifa leo umeripoti kuwa Kiongozi wa wanaharakati hao wanatokea katika kundi linalojiita ‘Operesheni Linda Jamii,’ Profesa Fred Ogola, amesema badala ya kutumia Mawaziri 22 pamoja na maofisa wengine wakuu kuongoza shughuli hiyo, viongozi wa mikoa, wangetumika.

“Kwa mtazamo wangu kama mtaalamu wa masuala ya kiuchumi, naona kwamba huo ni ubadhirifu wa pesa za umma kwa Serikali kukodisha helikopta kwa ajili ya mawaziri kwenda kwenye kaunti mbalimbali kuongoza shughuli ya upandaji miti,” amesema Profesa Ogola na kuongeza;

“Inagharimu kati ya KSh150, 000 (Sh2, 486, 816) na KSh170, 000 (Sh2, 818, 391), kukodisha helikopta kwa saa moja. Kwa hivyo inakadiriwa kuwa mpaka Jumatatu, Novemba 13, 2023, Serikali imetumia zaidi ya KSh1 bilioni kusafirisha mawaziri huku na kule.”

Siku ya Jumatatu ilitengwa na Serikali kama Siku ya Kitaifa ya upandaji miti na hivyo kutangazwa kuwa siku ya mapumziko.

Inaelezwa kuwa Serikali ilifanya hivyo ili kuhakikisha kwa jumla ya miti 500 milioni ingepandwa siku ya Jumatatu pekee kama sehemu ya kufanikisha lengo la kupanda angalau miti 15 bilioni ndani ya miaka 10 ijayo (mpaka 2032).

Profesa Ogola alisema kuwa ajenda ya upandaji wa miti imesukumiwa Serikali ya Kenya na mashirika ya kimataifa ya kifedha kama vile; Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) na Benki ya Dunia (WB).

“Sisi kama Operation Linda Jamii tunahimiza Rais William Ruto kukoma kuingiza masharti ya IMF na Benki ya Dunia katika Sera ya Bajeti ya Serikali (BPS) kwani baadhi ya sera hizo zinaumiza Wakenya,” akasema.

Profesa Ogola aliorodhesha hatua kadha ambazo Serikali inaweza kuchukua kuwapunguzia Wakenya mzigo wa kupanda kwa gharama ya maisha.

Miongozi mwa hatua hizo ni kupunguzwa kwa viwango aina mbalimbali za ushuru, kuondolewa kwa Mamlaka ya Kusimamia Nishati na Mafuta (EPRA), kupunguzwa kwa bajeti ya Serikali, kupunguza madeni ya kitaifa, kuimarishwa kwa vita dhidi ya ufisadi na kutekelezwa kwa miradi ambayo itaweka pesa mfukoni mwa wananchi moja kwa moja.

“Aidha, tungependa Serikali kuiga mfano wa mipango ya usimamizi wa kiuchumi unaokumbatiwa na mataifa kama Singapore, Korea Kaskazini na Malaysia. Nchi hizi zilikuwa katika kiwango sawa cha ukuaji wa kiuchumi na Kenya katika miaka ya 1970, lakini wakati huu zimepiku taifa letu kimaendeleo,” amesema.