Wapinzani wasusia uchaguzi mkuu Madagascar

Muktasari:

  • Viongozi wa upinzani wakiwemo marais wawili wa zamani Ravalomanana na Hery Rajaonarimampianina, wamekuwa wakifanya maandamano kudai uhuru na uwazi katika mikakati ya kuandaa uchaguzi huo.

Madagascar. Wapigakura milioni 11 nchini Madagascar, leo Alhamisi watamchagua Rais, katika uchaguzi uliosusiwa na wagombea wa upinzani, huku kukiwa na hali ya wasiwasi nchini humo.

RFI imeripoti kuwa vituo vya kupigia kura vimefunguliwa tangu saa 12 asubuhi saa za Madagascar na kwamba Rais aliyeko madarakani Andry Rajoelina, ni miongoni mwa wagombea 13 wanaowania kiti hicho, japo inadaiwa wagombea 11 wa upinzani wamejitoa katika kinyang’anyiro hicho.

Imeelezwa kuwa, siyo tu kwamba wamegoma lakini pia wamekuwa wakiwataka raia wa nchi hiyo kususia upigaji kura wakidai kumekuwa na mikakati ya kuupendelea Rais aliyepo madarakani.

Ikumbukwe kuwa, Rais Rajoelina aliingia madarakani mwaka 2009 baada ya mapinduzi yaliyomuondoa madarakani Marc Ravalomanana, japo (Rajoelina) hakuwania muhula uliofuata, hata hivyo, alirejea madarakani mwaka 2018 na amekuwa akiweka bayana matumaini yake ya kushinda uchaguzi unaofanyika leo.

Tangu Oktoba mwaka huu, viongozi wa upinzani wakiwemo marais wawili wa zamani Ravalomanana na Hery Rajaonarimampianina, wamekuwa wakifanya maandamano kupinga kile walichodai ni kutokuwepo kwa suala la uhuru na uwazi katika mikakati ya kuandaa uchaguzi huo.

Jana polisi nchini humo, walipiga marufuku ya watu kutoka nje nyakati za usiku katika Mji Mkuu wa nchi hiyo Antananarivo, ambapo marufuku hiyo ilikuwa ni kwa siku moja kabla ya uchaguzi wa urais.

Marufuku hiyo ilichochewa na maandamano ya zaidi ya mwezi mmoja yaliyofanyika katika mitaa ya Antananarivo yaliyoitishwa na upinzani.

Gavana wa Mji Mkuu, Jenerali Angelo Ravelonarivo, ameshutumu vitendo vya hujuma vilivyofanyika jana

"Kutokana na vitendo mbalimbali vya hujuma vilivyotokea nitatoa uamuzi hivi karibuni wa kutaganzwa sheria ya kutotoka nje kutoka saa 9:00 usiku hadi saa 4:00 usiku (Alfajiri)," alitangaza jana wakati wa mkutano na waandishi wa habari.

Akirejea kuchomwa kwa kituo cha kupigia kura na kuharibiwa kwa vifaa mbalimbali vya uchaguzi, gavana huyo ameonya dhidi ya vitendo vinavyoweza kusababisha watu kukamatwa katika kipindi hiki cha uchaguzi.

Wagombea 13 wanawania kiti cha urais, akiwemo rais anayemaliza muda wake Andry Rajoelina, mwenye umri wa miaka 49. Wagombea 10 wa upinzani walikusanyika kwa pamoja, wakiwemo marais wa zamani Hery Rajaonarimampianina na Marc Ravalomanana na kuwataka wapigakura  kutoshiriki.

"Tunakataa uchaguzi huu na tunatoa wito kwa watu wote wa Madascar kuzingatia kuwa uchaguzi huu haupo," alitangaza mgombea na mpinzani Andrianinarivelo, kwa niaba ya wagombea urais 10.

"Tunatoa wito kwa kila mtu kutopiga kura," amesisitiza mgombea Roland Ratsiraka.