11 mbaroni wakituhumiwa kutuma ujumbe ‘tuma ile pesa kwa namba hii’

Muktasari:

Watu 11, mbaroni Kwa tuhuma za utapeli kwa njia ya mtandao,Ni wale wanaotuma ujumbe mfupi wa 'Ile pesa tuma Kwa namba hii'

Moshi. Jeshi la Polisi Mkoani Kilimanjaro linawashikilia watu 11 Kwa tuhuma za utapeli kwa njia ya mitandao.


Watuhumiwa hao ni wale ambao wanadaiwa hutuma ujumbe mfupi Kwa njia ya simu, 'Ile pesa tuma kwa namba hii', ambapo wamekamatwa na simu za kiganjani 19 pamoja na fedha Sh700,000 ambazo wanadaiwa kuwatapeli watu mbalimbali kupitia ujumbe wa simu.

Akitoa taarifa hiyo leo Januari 13,2023   Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema watu hao walikamatwa Januari 9, mwaka huu katika eneo la Matindigani Pasua, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Amesema watu  hao 11 walikamatwa wakiwa chumbani wakitapeli watu kwa njia ya mtandao kwa kuwatumia ujumbe mfupi wa maandishi kuwa ‘Ile pesa tuma kwa namba hii’.


Kamanda Maigwa amesema baada ya watuhumiwa kufanyiwa upekuzi walikutwa na simu za aina tofauti tofauti 19 kati ya simu hizo, nane ni simu janja na 11 simu ndogo (Viswaswadu).

Amesema kuwa baadhi ya simu hizo zimekutwa zikiwa na ujumbe  mbalimbali zinazosomeka ‘tuma kwa namba hii ambapo pia walikutwa na fedha taslimu ambazo walikuwa tayari wametapeli.


"Watuhumiwa hao pia  wamekutwa na pesa taslimu 700,000 ambazo ni pesa walizokuwa wameshatapeli watu na walikuwa wanasubiri wengine watume pesa kisha zinapotumwa zinatolewa haraka kwa mawakala wa mitandao husika," amesema kamanda Maigwa.


Aidha Kamanda Maigwa amesema upelelezi wa kina wa shauri hilo unaendelea na baada ya kukamilika watuhumiwa hao watafikishwa kahakamani ili kujibu tuhuma zinazowakabili huku akiwataka wananchi kutoa taarifa wanapowabaini matapeli.