Askofu Shoo: Corona ipo chukueni tahadhari
Askofu Fredrick Shoo akizindua kitabu chenye mkakati wa mawasiliano ya viongozi wa dini kuhusiana na ugonjwa wa covid 19 ambapo kitabu hicho kitawawezesha kuendelea na majukumu yao na kuongeza usalama wa waumini. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ,Askofu Fredrick Shoo amewakumbusha Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.
Moshi. Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ,Askofu Fredrick Shoo amewakumbusha Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.
Ameeleza hayo leo Jumatano Juni 30, 2021 katika mkutano wa viongozi mbalimbali wa dini waliokutana mjini Moshi.
Katika mkutano huo ulifanyika uzinduzi wa kitabu cha mkakati wa mawasiliano ya viongozi wa dini kuhusu ugonjwa huo sambamba na kuweka mikakati ya kuongeza usalama wa waumini.
Amesema ni muhimu kila mmoja kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo kwa sababu watu wanaishi kwa mazoea na kusahau kama upo.
"Sasa hivi inaonekana watu wamesahau, wamepuuza kuchukua tahadhari juu ya wimbi hili la tatu la corona na hii italeta hatari kubwa sana," amesema Askofu Shoo
Amebainisha kuwa katika nyumba za ibada unatakiwa umakini katika utoaji wa sakramenti ili kuepuka kugusana mikono.
"Umakini unahitajika katika utoaji wa sakramenti ili kupunguza kugusana mikono na pia kuhakikisha vifaa vya ibada vinasafishwa ipasavyo ili kupunguza kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19.”
"Tutaendelea kuweka tahadhari kwenye nyumba zetu za ibada na kuelimisha watu, kuchukua tahadhari zinazoelekezwa na wataalam wa afya ili katika nyumba zetu za ibada pasiwe sehemu ya maambukizi," amesema Askofu Shoo huku akitaka idadi ya ibada kuongezwa ili waumini wakae mbalimbali.