Bilionea Laizer achangia Sh10 milioni mfuko wa elimu Simanjiro

Friday January 14 2022
Bilionea pc
By Joseph Lyimo

Simanjiro. Mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite katika mji mdogo wa Mirerani, wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Saniniu Laizer amechangia Sh10 milioni kwa ajili ya kutunisha mfuko wa elimu wa wilaya hiyo.

Mfuko huo wa elimu umeanzishwa na mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Dk Suleiman Serera kwa lengo la kupambana na changamoto mbalimbali zinazowakabili kwenye sekta hiyo.

Akizungumza kwenye kikao cha wadau wa elimu wa Simanjiro, Laizer amesema amechangia fedha hizo kwa ajili ya kuboresha elimu katika wilaya hiyo.

"Watoto wa jamii ya wafugaji hapa Simanjiro, hivi sasa wana mwamko mkubwa wa kupata elimu, hivyo namuunga mkono mkuu wetu wa wilaya katika kuhakikisha wanafunzi wanasoma inavyopaswa," amesema Laizer.

Kwa upande wake, mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Dk Suleiman Serera amesema mfuko wa elimu wa wilaya utakuwa endelevu kwa lengo la kuboresha elimu.

 "Tunapokuwa na mfuko wa elimu wa wilaya tunaweza kuwalipa mishahara hata walimu 100 wa kujitolea wa masomo ya sayansi ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi wetu," amesema Dk Serera.

Advertisement

Mbunge wa jimbo la Simanjiro,  Christopher Ole Sendeka naye aliunga mkono mfuko huo wa elimu wa wilaya kwa kuchangia Sh5 milioni.

"Pamoja na kuunga mkono mfuko huo kwa kiasi hicho nitachangia pia Sh3 milioni kwa ajili ya ujenzi wa choo cha shule ya msingi Ngorika na Sh3 milioni kwa ajili ya nyumba ya mwalimu shule ya Lengungumwa, kata ya Ngorika," amesema Ole Sendeka.

Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM mkoa wa Manyara, Kiria Laizer naye amechangia mfuko huo wa elimu wa wilaya ya Simanjiro kwa kutoa Sh5 milioni.

Advertisement