Chongolo kuwafikisha kwa Rais Samia ‘viongozi wa hovyo’

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo

Muktasari:

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo ameonyesha kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi wa Maji wa Wona-Marangu-Amboni, unaotarajiwa kugharimu Sh 2.9Bilioni hadi kukamilika.

Rombo. Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo ameonyesha kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi wa Maji wa Wona-Marangu-Amboni, unaotarajiwa kugharimu Sh 2.9 bilioni hadi kukamilika.

 Chongolo amesema fedha za mradi huo ambao unaanzia Marangu hadi Rombo, tayari zimewekwa kwenye bajeti lakini utoaji wa fedha hizo kwenda kwenye mradi umekuwa ni changamoto.

Mradi wa maji wona marangu Amboni, ambao unatekelezwa na mkandarasi  Best One Limited, unahusisha ujenzi wa chanzo, mabomba yenye urefu wa kilometa 22 na tanki la maji la lita laki moja

Mkandarasi wa mradi huo alisaini mkataba Februari mwaka huu na mradi unapaswa kukamikika agust 23 lakini mpaka sasa ujenzi wa tanki umefikia asilimia 30 huku wa Chanzo ukifikia asilimia 40.

Chongolo akizungumza leo Ijumaa Agusti 5,2022 na wananchi wa Tarakea Wilaya ya Rombo,  amewaahidi wananchi kufikisha taarifa kwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hasani kumweleza uwepo wa watu hovyo ambao wanamchonganisha na wananchi na Serikali.

Chongolo amesema ni lazima kuwa na watu ambao wakikubaliana fedha zinatengwa kwa ajili ya mradi fulani ziende kwenye huo mradi na utekelezwe ili uweze kuleta matokeo na miongoni mwa miradi hiyo ni mradi huo wa maji ambao  hauridhishi kwa kasi yake ya utekelezaji.

Amesema atakwenda kukabana mashati kuhakikisha mradi huo ambao unaonekana kusuasua, unakamilika na wananchi wanaondokana na changamoto ya upatikanaji wa maji.

Ameeleza hawapo tayari kuona miradi kwenye makaratasi na badala yake wanataka miradi halisia na kuwaomba kusimamia miradi yote inayoletwa na Serikali ili itekelezwe kwa wakati.

"Ruwasa ni lazima watupe tafsiri ya utatuzi wa changamoto ya mradi huu, kama amepewa mkandarasi, changamoto ni fedha basi zishuke, na mimi ndio kazi yangu nikiondoka hapa naondoka na taarifa yangu kwapani Mwenyekiti si ndio amenituma nije na yeye ndio Rais wa Tanzania,” amehoji Chongolo

"Wala simchongei mtu naenda kusema kuna watu wako wa hovyo wanakuchonganisha na wananchi," amesema Chongolo.

Amesema, "Rais ameahidi mradi na kuagiza fedha ziwekwe kwenye bajeti na zimewekwa lakini watu kutoa fedha tu na kupeleka zikatekeleze mradi wanapiga miguu miwili kushoto miguu miwili kulia, hatuwezi kwenda na mambo ya namna hiyo."

"Mkuu wa wilaya wewe pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya nyie njooni chini ili kuhakikisha fedha hizo zitakapofika kasi ya mradi inaridhisha na kuleta matokeo yaliyokusudiwa kutolewa na ndio kazi yako" amesema Chongolo.

 "Mkuu wa mkoa kazi yako wewe ni kuniambia fedha imeingia au imechelewa ukinijulisha mimi katibu mkuu kazi yangu ni kushikana mashati huko juu watuambie kama tumeweka mradi kwenye bajeti fedha ipo mnataka nani ashuke ili alete hiyo fedha huku, hatupo tayari kugombanishwa na wananchi," amesema 

Amesema wao ndio wasaidizi wa Mwenyekiti wa CCM Taifa na yeye ni msaidizi mkuu na hayupo tayari kuona mambo ya hovyo na yasiyofaa yakifanyika hivyo ni lazima wakabane mashati kuleta matokeo yaliyokusudiwa.

"Mtumishi au kiongozi aliyepewa dhamana kama yeye anasimamia mafungu kushushwa huku chini ahakikishe anatekeleza hilo kwa vitendo hatutakuwa tayari kuona mambo hayaendi na yeye yuko pale amepiga nne," amesema

Naye Kaimu mkurugenzi wa mamlaka ya maji Rombo (ROMBOWSSA) Martin Kinabo amesema mradi huo ukikamilika utakuwa una uwezo wa kuzalisha maji mita  za ujazo 4,000 kwa siku na utanufaisha zaidi ya vijiji 39 na wananchi 56,000.

"Wilaya ya Rombo kwa sasa wanapata maji kwa asilimia 57 na kutokana na upungufu huo wananchi wanapata maji kwa mgao ambapo ukanda wa chini wanapata maji saa 4 kwa wiki, lakini kukamilika kwa mradi huu na mingine inayotekelezwa Rombo, upatikanaji wa maji utaimarika" amesema.

Chongolo yupo katika ziara ya kikazi mkoani Kilimanjaro, ambapo anahimiza na kusimamia Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2020 – 2025 na kuangalia uhai wa chama.