Kama una tatizo hili, usile ndizi mbivu

Ndizi mbivu inapochanganywa na maziwa humfanya mtu aongezeke uzito kwa haraka kwa sababu maziwa hutoa protini na ndizi hutoa sukari.

Wataalamu wanaeleza kuwa machanganyiko huo husababisha mlaji anenepe.

Mtaalamu wa Lishe kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili(MNH), Scholastica Mlinda anasema licha ya ndizi kuwa na faida nyingi mwilini, ni hatari kwa watu wenye matatizo ya figo.

“Watu wenye matatizo ya figo hawatakiwa kutumia ndizi mbivu kwa kuwa ni hatari kwao,” anasema Mlinda.

Mtaalamu huyo anasema ndizi ina madini ya potasiam ambayo ni hatari kwa watu wenye matatizo hayo.

Hata hivyo, anasema madini ya potasium kwa watu wasio na matatizo ya figo inatajwa kusaidia kujenga misuli na kumfanya mtu aweze kuwa hodari katika tendo la ndoa.

“Tunda hili husaidia kushusha presha, kulinda afya ya moyo, kuboresha mfumo wa mkojo na kinga ya mwili na afya ya macho.”

Mtaalamu huyo anasema ulaji wa ndizi mbivu hupunguza makali ya vidonda vya tumbo na ni chanzo kikubwa cha vitamin B ambayo husaidia kuongeza stamina wakati wa kufanya kazi nzito.

“Ndizi humeng’enywa kwa urahisi hivyo mtu mdhaifu anaweza kula ndizi mbivu tano hadi sita kwa siku tofauti na milo mingine na zote zikamengenywa na kuingia mwilini husababisha kuongeza nguvu.”

Licha ya faida hizo, ndizi mbivu ina sifa ya kuwa na nishati, wanga na ina virutubisho kama vitamini A,B na C.

Pia, ina manganizi, potasium, madini ya foliki, riboflavin, niacin na madini ya chuma.

Ndizi husaidia kupunguza uwezekano wa kupata ugonjwa ya pumu, hivyo ulaji wa ndizi mbivu moja kila siku kwa mtoto wadogo unaweza kupunguza hatari ya kupata ugonjwa huo. Faida nyingine ya ndizi mbivu, husaidia kulegeza mishipa ya damu na kupunguza tatizo la shinikizo la damu.

Makala haya yameandikwa na mwandishi wa gazeti hili Hadija Jumanne