Kina Mdee ngoma nzito, wafungua kesi nyingine

Kina Mdee ngoma nzito, wafungua kesi nyingine

Muktasari:

  • Ni baada ya kurekebisha karoso za kisheria zilizoainishwa mahakamani

Dar es Salaam. Wabunge waliofukuzwa Chadema wameendeleza mapambano ya kisheria mahakamani kupigania uanachama na ubunge wao, baada ya kufungua tena shauri wakiomba ridhaa ya mahakama kufungua shauri la kupinga kuvuliwa uanachama.

Awali, Halima Mdee na wenzake 18 walifungua maombi kama hayo Mahakama Kuu Masjala Kuu dhidi ya Chadema, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Hata hivyo, maombi hayo yalitupiliwa mbali Juni 22, na Jaji John Mgetta kutokana na kasoro za kisheria, baada ya kukubaliana na hoja mbili kati ya sita za pingamizi zilizoibuliwa na Chadema kupitia jopo la mawakili lililoongozwa na wakili Peter Kibatala.

Baada ya uamuzi huo juzi, Mwananchi ilifanya jitihada za kumtafuta Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kuzungumzia suala hilo lakini hazikuzaa matunda.

Hata Katibu wa Bunge, Nenelwa Mwihambi alivyotafutwa ofisini kwake hakupatikana na ilielezwa alikuwa ndani ya ukumbi wa Bunge na
alipopigiwa simu baada ya kuharishwa kwa Bunge, alituma ujumbe wa maandishi akitaka kuandikiwa ujumbe, lakini hata alipoandikiwa hakuijibu.

Juzi, Chadema ilieleza imewasilisha barua kwa ofisi ya Bunge kukijulisha kuhusu uamuzi huo wa mahakama.

Siku moja baada ya maombi yao kutupwa, Mdee na wenzake juzi, Juni 23 walirudi mahakamani hapo na kufungua upya maombi hayo baada ya kurekebisha kasoro zilizoainishwa.

Mawakili wao, Aliko Mwamanenge, Ipilinga Panya na Edson Kilatu waliieleza Mwananchi jana kuwa shauri hilo jipya la ridhaa ya kufungua shauri la maombi ya mapitio ya Mahakama (kupinga uamuzi wa Chadema kuwavua uanachama) limesajiliwa kama shauri namba 27 la mwaka 2022.

Walisema sambamba na shauri hilo, pia walifungua shauri wakiomba amri ya mahakama kudumisha hali ilivyo sasa (kulinda hadhi ya ubunge wa wateja wao), ambalo limepewa usajili wa namba 16 la mwaka 2022.

Mawakili hao walieleza wamefanikiwa kufungua tena shauri hilo kwa kuwa walikuwa wamejiandaa na kuwaandaa wateja wao kwa uamuzi wowote wa mahakama.

Alifafanua baada ya kutoka mahakamani walirejea ofisini kufanya marekebisho ya kasoro zilizoainishwa na kwamba baada ya saa tatu walikuwa wamekamilisha, kisha akasafiri usiku huo kuwafuata wateja wake kwa ajili ya kusaini nyaraka hizo.

“Baada ya wateja wetu kusaini jana (juzi) asubuhi tuka-file (wakawasilisha nyaraka mahakamani) na mpaka saa moja tulikuwa tumemaliza ku-upload (kupakia nyaraka) maana siku hizi tuna-file online (kufungua kupitia mtandao),” alisema Panya na kuongeza:

“Mahakama baada ya kuzifanyia assessment nyaraka zetu tulikwenda tukalipia kisha tukapewa namba, hivyo mpaka saa mbili tulikuwa tumeshapata na namba na tukawajulisha wateja wetu wamwandikie Spika kumjulisha wameshafungua tena shauri na namba ni hiyo.”

Wakili Mwamanenge alisema licha ya kukamilisha mapema kufungua shauri hilo, hawakutaka kuweka wazi wakisubiri kwanza wapate hati ya wito kwa wajibu maombi ambayo ndiyo itaonyesha tarehe ya kutajwa na hata jaji atakayelisikiliza.

Hata hivyo, alisema mpaka jana jioni bado walikuwa hawajapata hati ya wito na wanaendelea kuisubiri kwa ajili ya kuwapelekea Chadema.

Ingawa walikuwa wanasoma taarifa nyingi na zisizo sahihi kwenye mitandao kuhusu uamuzi na hatima ya wateja wao, lakini walitulia kwa kuwa walikuwa wakijua wanachokifanya.