Kivumbi kutimka majimboni, kata

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani nchini, viongozi wa serikali baada ya mkutano wake na viongozi wa vyama hivyo uliofanyika ikulu jijini Dar es Salaam Januari 3 mwaka huu. Picha na Ericky Boniphace


Muktasari:

  • Madiwani waliojisahau matumbo moto, Wapinzani watangaza mikakati patashika nguo kuchanika.

Dar/mikoani. Ni mtifuano majimboni. Hivi ndivyo unavyoweza kuelezea kile kinachotarajiwa kutokea katika majimbo na kata mbalimbali kutokana na ruksa iliyotolewa ya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa iliyokuwa imezuiwa kwa miaka sita mfululizo.

 Januari 3 mwaka huu Rais Samia Suluhu Hassan alitangaza kuruhusu vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara akisema ni haki yao isipokuwa wazingatie sheria, kanuni, taratibu, mila na desturi za Watanzania.

Uamuzi huo ulipongezwa na wadau mbalimbali akiwemo Balozi wa Marekani ambaye kupitia ukurasa wake wa Twitter aliandika, “Hongera kwa Rais Samia, vyama vya siasa na wananchi wa Tanzania kwa kuondoa zuio kwa mikutano ya hadhara ya kisiasa. Namna nzuri ya kuuanza mwaka 2023.”

Kuruhusiwa kwa mikutano hiyo iliyozuiwa na Rais wa awamu ya tano, John Magufuli, kumewaweka matumbo joto wabunge na madiwani ambao hawakuwa na kawaida ama ya kufanya mikutano au kuonja joto la upinzani kwa muda mrefu.

Wachambuzi wa masuala kisiasa wanasema wabunge na madiwani waliopo watakuwa na kazi ya kushawishi wananchi waendelee kuwaamini na kujibu mapigo ya hoja zitakazokuwa zikiibuliwa na washindani wao kwenye mikutano ya hadhara, kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya kisiasa.

Baadhi ya wanasiasa wa upinzani wameleeza jinsi walivyojiandaa kuingia mitaani kwa ajili ya mikutano huku wengine wakisambaza picha za bendera zilizoandaliwa kwa ajili hiyo.

Mikutano hiyo kwa sehemu kubwa ndiyo iliyowapa umaarufu wapinzani kwa kuibua hoja mbalimbali zilizoifanya Serikali ama kuzifanyia kazi, kuzikanusha au kuzitolea ufafanuzi.

Presha kila mahali

Kutokana na ruksa hiyo na maandalizi yaliyopo, Mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk George Kahangwa alisema “kutakuwa na presha kubwa.”

“Na jambo jema presha ipo na hata tulipoamua kuwepo kwa vyama vingi sababu ni hiyohiyo, kuwa waliopo ofisini wasibweteke kwa sababu kuna chombo cha kuwamulika na ushindani una manufaa kwa nchi,” alisema.

Dk Kahangwa ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema presha hiyo inatokana na “msukumo kwa walioko ofisini kuwa watakosolewa, wataonyeshwa wanapokosea na wakicheza uchaguzi unapokuja wanaweza kuondoka.”

Alisema presha hiyo haitaishia kwenye kata na majimbo pekee, bali hata baadhi ya taasisi kama Bunge na Jeshi la Polisi kutokana na mambo mbalimbali yatakayokuwa yanaibuliwa kama ilivyowahi kushuhudiwa huko nyuma.

Aliongeza, “tutashuhudia baadhi ya ‘makaburi’ yakifukuliwa kama haki za binadamu, kuendelea kuongezeka kwa deni la Taifa, vyombo vya habari na kwa kifupi ni presha kila mahali,” alisisitiza.

Hata hivyo, mtazamo wa Dk Kahangwa unatofautiana na wa mchambuzi mwingine, Bubelwa Kaiza aliyesema vyama vinahitaji mwaka mmoja au zaidi kwa ajili ya kujipanga kufanya mikutano ya hadhara.

Kwa mujibu wa Kaiza, vyama vinahitaji kujiweka sawa, kuangalia uongozi wake, mtandao wake, rasilimali na mifumo ya kiutawala.

“Kuna vitu vingi vya kufanya kabla hata mikutano haijaanza. Kwa hiyo kama wanakimbilia kwenye mikutano ya hadhara, hawajui wanafanya nini kwenye siasa. Chama serious (makini) kitaangalia uwezo wake wa ndani, mazingira ya nje, viongozi wake, mwitikio wa wananchi, mifumo ya teknolojia,” alisema Kaiza.

Alisema vyama haviwezi kufanya yote hayo chini ya mwaka mmoja, hivyo anaona vikifanya hivyo sasa havitatoa ushindani mkubwa kwa CCM hivi karibuni hadi hapo watakapojipanga na kuweka mikakati imara ya kuwashawishi wananchi.

Mikakati yawekwa

Baadhi ya viongozi wa upinzani, hasa mikoa ya Kanda ya Ziwa wametamba kuanza mikakati ya mikutano ya hadhara ndani ya wiki mbili kwa lengo la kujiimarisha ili kushinda chaguzi zijazo huku wenzao wa CCM wakiwemo wabunge wakisema wako tayari kuwakabili, kuhimili na kujibu vishindo.

Tayari aliyekuwa Meya wa Ubungo na Kinondoni kupitia Chadema, Boniface Jacob ametangaza kuanza maandalizi ya mkutano wake wa hadhara utaofanyika Jumamosi hii Kimara Mwisho.

Jacob ameanza kutengeneza bendera ambazo atazitumia akisema atafanya mikutano jimbo la Ubungo ambalo mwaka 2020 aligombea ubunge na kushindwa na Profesa Kitila Mkumbo wa CCM.

Mbali na huyo, John Heche, mbunge wa zamani wa Tarime Vijijini alisema “CCM hawana tena ile free ride (kufanya wenyewe siasa) waliyoifaidi tangu mwaka 2016; tutawakabili kwa hoja kupitia mikutano ya hadhara kuanzia vijiji na mitaa, kata hadi majimbo huku tukionyesha mapungufu yao na ahadi ya nini sisi tutafanya tukipata dhamana ya kuongoza Serikali.”

Alisema tofauti na wengi wanavyodhani kuwa kazi ya upinzani ni kukosoa chama tawala, wao Chadema wamejiandaa kuing’oa CCM madarakani kupitia sanduku la kura kwa kutangaza sera mbadala na kushawishi wapigakura.

Kwa mtazamo huo, Heche anaungwa mkono na Katibu wa chama hicho Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami aliyesema “ni kama tumetoka kwenye kifungo cha miaka saba. Tunajipanga kushambulia kila kona ya nchi kwa mikutano kueleza mapungufu ya CCM na Serikali yake huku tukiwashawishi wananchi watupe ridhaa ya kuongoza dola.”

Kwa upande wake, katibu wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Mashiku alisema chama chake kitatumia vema fursa hii kujiimarisha ili kushinda uchaguzi wa serikali ya mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

“Tunaenda kufakamia mikutano ya hadhara kila sehemu ya mkoa wa Mwanza; kupata fursa ya kufanya mikutano baada ya miaka saba ni sawa na mtu mwenye njaa kali aliyepata chakula, ambaye hufakamia bila kuacha hata punje, labda inayoanguka chini. CCM wajipange sawa sawa,” alisema Mashiku.

Kujibu mapigo

Wakati wapinzani wakisema hayo, Mbunge wa Tarime vijijini, Mwita Waitara (CCM) alisema hana hofu kwa sababu ana mbinu za kuhimili ushindaji wa kisiasa kutokana na uzoefu wa kuwa kada na kiongozi wa CCM na Chadema kwa nyakati tofauti.

“Nimekuwa mwanachama, kada na kiongozi wa CCM kabla ya kuhamia upinzani mwaka 2008; sasa nimerejea tena CCM na kushinda ubunge, niko tayari na nina uzoefu wa kukabiliana na changamoto zote,” alisema Waitara.

Kauli ya utayari pia ilitolewa na mbunge wa Bukoba Mjini (CCM), Steven Byabato akitamba kufanya mambo mengi yanayoonekana kwa wapiga kura katika miaka mitatu ya ubunge.

“Binafsi sina hofu, hata chama changu CCM hakina hofu ya mikutano ya hadhara kwa sababu yapo mengi yamefanyika tangu tuliposhinda ubunge na kuongoza halmashauri mwaka 2015. Tuko tayari kukosolewa na kuonyeshwa mapungufu yetu kwa lugha ya staha, tutayafanyia kazi,” alisema Byabato ambaye pia ni naibu waziri wa nishati

Naye Stanslaus Mabula, mbunge wa Nyamagana (CCM) alisema amejiandaa kupokea, kujibu na kufanyia kazi ukosoaji na hoja zitakazoibuliwa na vyama vya upinzani kupitia mikutano ya hadhara.

“Ukosoaji na changamoto zitakazotolewa na upinzani tutazigeuza kuwa fursa ya kujirekebisha na kufanya vema zaidi. Bahati nzuri nina uzoefu wa kukabiliana na hoja za upinzani tangu nikiwa meya wa Jiji la Mwanza lililokuwa na madiwani wengi kutoka vyama vya upinzani,” alisema Mabula.

Mwenyekiti wa wabunge Mkoa wa Mbeya ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Vijijini, Oran Njeza alisema kuruhusiwa kwa mikutano ni jambo walilokuwa wakilitegemea kwa kipindi kirefu na wako tayari kukosolewa ili kutatua kero za wananchi.

“Kwa sasa tunachotarajia ni kukubali kukosolewa ili kuweza kusonga mbele na kumsaidia Rais Samia katika kufuatilia changamoto za wananchi na kuzitatua,” alisema.

Mbunge wa Moshi Mjini (CCM), Priscuss Tarimo alisema kuruhusu mikutano ya hadhara kunaleta mawazo mbadala na pengine kukosoa na ni kitu ambacho ni kizuri.

Hoja za Tarimo zinaungwa mkono na Mbunge wa Ngorongoro, Joseph Ole Shanghai aliyesema Rais amepanua wigo wa demokrasia nchini na mikutano ya hadhara itaimarisha utendaji wa Serikali kwani kuna watu watakuwa wanakosoa na Serikali kujirekebisha.

Hata Zelothe Steven, mwenyekiti wa CCM mkoa wa Arusha alisema kufuatia tamko hilo wanajipanga kuzikabili hoja za upinzani makujwaani.

Fursa ya kukosoa

Pamoja na kauli za wanasiasa, Wakili Elia Kiwia alisema kuruhusu mikutano ya hadhara kwenye vyama vya siasa kutatoa nafasi kuikosoa Serikali kwa kuwa ndilo jukumu lao kubwa.

“Ni hatua nzuri kwa sababu vyama vingine vya siasa tofauti na CCM vilikuwa havipewi nafasi ya kutoa maoni yao ya kisiasa, hawakuwa na nafasi ya kukosoa Serikali kwani ndilo jukumu lao kuu, CCM walibaki tu upande mmoja na kusikilizwa na kuwanyima upande wa pili haki ya kikatiba ya kutoa maoni na kusikilizwa,” alisema.

Tija ya mikutano

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana CCM (UVCCM), Mohamed Ali Kawaida alikutana na wanahabari Zanzibar akisema wanatarajia kuona tija ya vyama vya siasa kupitia mikutano hiyo.

“Tunaamini kuwa maamuzi haya ni kielelezo kuwa CCM kinatambua mchakato wa maridhiano ulihitaji juhudi za makusudi na ustahimilivu na vyote vilionyeshwa na Rais Samia,” alisema.

Walichosema madiwani

Diwani wa Marangu Magharibi, Mkoa wa Kilimamnajro, Filbert Shayo alisema kuruhusu mikutano ya hadhara haiwatishi bali zitumike siasa safi na kwamba mikutano ya matusi na kejeli haitajenga kwani Watanzania wanahitaji kuona mabadiliko chanya.

“Kama sitoshi kwenye kata yangu, wananchi wana maamuzi na kama sijatosha kwenye kata yangu wananchi wanayo maamuzi pia, kwa hiyo tunafungua milango wananchi wawe huru kuchagua kiongozi wanayeona anaendana na ulimwengu wa sasa,” alisema

Diwani wa Katangara Mrere, mkoani humo, Venance Mallel alisema mikutano ya hadhara itatoa nafasi ya kukosoa na kukosolewa hasa kwa viongozi waliojisahau wakiwa na maana kwamba wao ndio pekee wanaofanya siasa.

“Kikubwa viongozi waliochaguliwa na chama kuhakikisha tunakubali kukosolewa ili tuangalie pale tulipojirekebisha tuweze kufanya kazi. Mara nyingi viongozi walijisahau hasa sisi madiwani wenyewe na wabunge wakiwa na maana tu kwamba wao tu ndio wanaofanya siasa,” alisema.

Njoolay aonya

Aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Daniel Ole Njoolay yeye alitumia mkutano na waandishi wa habari Arusha kuwataka viongozi wa CCM kumaliza matatizo yao ya ndani ili waweze kunufaika na fursa iliyotolewa.

Njoolay mwana CCM tangu enzi za Tanu na aliyeshika nafasi mbalimbali serikalini, alisema kuruhusu mikutano hiyo ni fursa kubwa inayofaa kuungwa mkono kila upande lakini itashindwa kuleta manufaa ndani ya CCM endapo hawatamaliza tofauti zao na kuwa kitu kimoja katika kuzikabili hoja za upinzani.

Wasemacho viongozi wa dini

Jana viongozi wa dini nchini walikutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kwa lengo la kumpongeza Rais Samia na kuwasihi wanasiasa kufanya mikutano ya hadhara ya kistaarabu, amani na itakayokuwa na tija ya maendeleo ya nchi na si vinginevyo.

“Kiwango chake, uamuzi na ujasiri wa Rais wetu ni mkubwa sana, sasa maridhiano yamefikia pazuri,” alisema Askofu Gadi Charles wa Good News for All Ministry.

Alisema neno la Mungu linataka kwanza tuombe amani, ndicho kimefanywa na Rais ambaye hotuba yake juzi iliwafurahisha Watanzania wengi na kuitaka amani hiyo kuendelea kutawala kwenye mikutano ya hadhara ya kisiasa.

Mchungaji, Bezalel Massawe ambaye pia ni katibu wa kanisa hilo alisema Watanzania wengi wamemuunga mkono Rais katika hotuba yake na hasa kuruhusu mikutano ya kisiasa kuendelea nchini.

Akiwa Moshi mkoani Kilimanjaro, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo alisema hatua aliyofanya Rais ni ya ujasiri na kwamba inaleta matumaini mapya katika kukuza demokrasia ya kweli nchini.

Askofu Shoo alivitaka vyama vyote vya siasa nchini kufanya siasa za kistaarabu na kuachana siasa za chuki, uadui, siasa za kuumizana na kujeruhiana na kila chama kufanya siasa za kistaarabu na kubishana kwa hoja.

“Tumepata taarifa za kufurahisha na kuleta matumaini, baada ya kuona Rais Samia amekutana na viongozi wa vyama vya kisiasa na kilichotufurahisha zaidi ni uamuzi wake wa kuondoa zuio la katazo la mikutano ya vyama vya siasa, hili ni jambo jema ambalo linapaswa kupongezwa na Watanzania wote,” alisema.

Imeandikwa na Daniel Mjema na Janeth Joseph (Kilimanjaro), Mussa Juma na Bertha Ismail (Arusha), Hawa Mathias (Mbeya) na Peter Saramba (Mwanza), Peter Elias na Iman Makongoro (Dar), Jesse Mikofu (Zanzibar)