Mkoa wa Tanga wajipanga kufuga nyuki kwa wingi
Picha kwa hisani ya Handenikwetu blog.
Muktasari:
Mkoa wa Tanga unajipanga kushika nafasi ya kwanza nchini na barani Afrika katika uzalishaji wa mazao yatokanayo na nyuki, kutokana na eneo hilo kuwa na mazingira mazuri ya kufuga nyuki.
Tanga. Mkoa wa Tanga unajipanga kushika nafasi ya kwanza nchini na barani Afrika katika uzalishaji wa mazao yatokanayo na nyuki, kutokana na eneo hilo kuwa na mazingira mazuri ya kufuga nyuki.
“Ufugaji nyuki ni mradi mzuri sana wananchi wenzangu, nyuki hawahitaji chanjo wala hakuna kulipia kodi na pia wanasaidia utunzaji wa mazingira. Handeni pekee ina hekta takriban 50,000 zinazofaa kwa ufugaji nyuki. Mizinga hii inatoa kilo 30 kwa msimu mmoja,” alisema Muhingo Rweyemamu Mkuu wa Wilaya ya Handeni.
Rweyemamu ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Galawa, aliyasema hayo juzi, wakati wa Maadhimisho ya siku ya utundikaji wa mizinga Kanda ya Kaskazini, ambapo kikanda yalifanyika katika Kijiji cha Kwamatuku wilayani hapa.
Kaimu Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo ya kufuga nyuki, ili kujipatia kipato kisichokuwa na gharama kubwa za uendeshaji.
Taarifa ya wilaya hiyo iliyotolewa na Ofisa Nyuki, Jembe Chifuno, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Hassan Mwachibuzi, ilisema uharibifu wa mazingira uliotokana na kuchoma mkaa, ugawaji holela wa ardhi kwa ajili ya mashamba, kilimo cha kuhamahama pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, vimechangia kushuka kwa uvunaji wa mazao yatokanayo na nyuki wilayani Handeni.
Uharibifu huo wa mazingira umesababisha wilaya hiyo, kukumbwa na ukame katika kipindi cha kuanzia mwaka 2009/12. ambapo awali mwaka 2005 hadi 2008 wilaya hiyo ilivuna jumla ya Sh 988 milioni kutokana na mauzo ya asali.
Chifumo alisema licha ya kukabiliwa na changamoto hiyo ya ukame, lakini pia wafugaji wa nyuki, wameongezeka kutoka vikundi 36 hadi 48 katika kipindi cha 2012 hadi machi 2013, ambapo watu binafsi wameongezeka kutoka 577 hadi kufikia 700 katika kipindi hicho na wanamiliki jumla ya mizinga 11,509 ikiwamo ya kisasa 755.
Alisema mipango ni kuongeza wafugaji asali ili mkoa uweze kuwa kinara wa kuzalisha asali.