'Mwendokasi’ za Mbagala kutumia nishati ya gesi

Kaimu Meneja wa Mipango ya Usafirishaji  Dart, Mhandisi  Mohammed Kuganda, akiwa anafafanua jambo kuhusu mradi wa mabasi yaendayo haraka

What you need to know:

  • Mradi wa mabasi yaendayo haraka utatekelezwa kwa awamu sita ambapo miradi yote gharama yake ni Sh2.2 trilioni.

Dodoma. Mradi wa awamu ya pili ya mabasi yaendayo haraka barabara ya Mbagala unatarajiwa kuanza kazi rasmi Desemba mwaka huu, huku mabasi yake yakitarajiwa kutumia nishati ya gesi.

Hayo yamesemwa jana Mei 20, 2023 na Kaimu Meneja  wa Mipango ya Usafirishaji wa wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (Dart), Mhandisi Mohamed Kuganda katika mafunzo elekezi kwa waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa mradi wa Dart.

Kuganda amesema mradi huo utakaohusisha mabasi 750 tayari mchakato wa kumpata mzabuni unaendelea na moja ya masharti ni kuleta mabasi yanayotumia gesi.

Hatua hiyo za kutumia gesi amesema inatokana na malengo ya mradi mzima kwamba pamoja na mambo mengine ni kupunguza hewa ya ukaa ili kuhifadhi mazingira.

"Tayari kwa kuanza kazi mradi huu awamu ya kwanza tumeweza kupunguza moshi na kelele ambazo zilikuwa zikisababishwa na daladala ambazo nyingine zilikuwa zimeshachoka kutokana na kutumika kwa muda mrefu,”alisema.

"Hivyo kwa kutumia nishati gesi katika mradi wa Mbagala tutakuwa tuaendelea kuhifadhi mazingira yetu ikiwemo kupunguza hewa ya ukaa na matarajio ya baadaye ni kutumia nishatai hiyo kwa barabara zote na kufika hatua pia ya kutumia hadi umeme,"aliongeza.

Ili kuhakikisha gesi inapatikana wakati wote, Kaganda alisema wamejipanga kufunga mitambo ya kujazia nishati hiyo katika karakana zao.

Kuhusu kuanza kazi Desemba, Kuganda amesema ilitokana na mkandarasi kuomba kuongezewa muda wa miezi sita na kwa namna walivyoangalia pia hiyo miezi sita asingeweza kumaliza na kumuongezea hadi Desemba. Awali mradi huo ilikuwa uanze kazi Machi mwaka huu.

Hata hivyo amesema mara tu baada ya kukamilika kwa miundombinu na mabasi yataingia barabarani ambapo kwa awamu ya kwanza yanatarajiwa kuingizwa mabasi yasiyopungua 200.

Kuanza kazi kwa mradi huo awamu ya pili kutawezesha kusafirisha abiria 600,000 hadi 700,000 kwa siku.