Pima na wenzake kukata rufaa kupinga hukumu
Muktasari:
- Agosti 31, 2023 aliyekuwa mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dk John Pima na wenzake walihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa makosa tisa yaliyokuwa yanawakabili ikiwemo utakatishaji fedha Sh103 milioni.
Arusha. Aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dk John Pima na wenzake wawili, wanatarajia kukata rufaa baada ya kutoridhishwa na hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.
Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 5/2022, mbali na Dk Pima watuhumiwa wengine ni aliyekuwa Mwekahazina wa Jiji hilo, Mariam Mshana na aliyekuwa mkuu wa idara ya mipango, takwimu na ufuatiiaji, Innocent Maduhu.
Agosti 31, 2023 Dk Pima na wenzake walihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa makosa tisa yaliyokuwa yanawakabili ikiwemo utakatishaji fedha Sh103 milioni.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo Jumatatu Septemba 4, 2023 kwa simu, mmoja wa mawakili waliokuwa wanawatetea watuhumiwa hao, Sabato Ngogo amesema watakata rufaa na wanatarajia kuwa na sababu zaidi ya 15.
"Tutakata rufaa kwa kishindo kikubwa sana, tuliambiwa tunapewa nakala ya hukumu leo hii Jumatatu, tutaisoma na kesho au kesho kutwa tutakuwa tumewasilisha notisi ya nia ya kukata rufaa,"amesema wakili huyo na kuongeza;
"Tutahakikisha tunapata mwenendo wa kesi mapema na haraka iwezekanavyo. Sababu za rufaa tunazo tayari na tunazo zaidi ya sababu 15.”
Kesi hiyo ilikuwa inasikilizwa na Hakimu Mkazi Serafini Nsana, huku Jamhuri wakiwakilishwa na Mawakili wa serikali waandamizi Patrick Mwita, Hebel Kihaka, Timotheo Mmari, Mawakili wa serikali Nickson Shayo na Reuben Maduhu huku utetezi wakiwakilishwa na Mpaya Kamara, Mosses Mahuna na Ngogo.
Mei 24, 2022, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwasimamisha kazi watumishi sita wa Halmashauri ya Jiji la Arusha akiwemo Dk Pima, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za umma.
Katika kesi hiyo, upande wa Jamhuri walikuwa na mashahidi 26, huku utetezi wakiwa na mashahidi watatu.
Mbali na kesi hiyo watuhumiwa hao wanakabiliwa na kesi nyingine mbili ambapo katika kesi ya uhujumu uchumi namba 3/2022 watuhumiwa ni Dk Pima, Mariam, Maduhu na Nuru Ginana(aliyekuwa mchumi) ambapo wanakabiliwa na makosa manne ikiwemo ufujaji na ubadhirifu na matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri.
Kesi ya uhujumu uchumi namba 4/2022 watuhumiwa ni Dk Pima, Mariam, Maduhu na Alex Daniel, ambao kwa pamoja wanakabiliwa na makosa manne ikiwemo ufujaji na ubadhirifu na matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri.
Aidha, kesi hizo mbili watuhumiwa hao walishasomewa maelezo ya awali na zinasubiri kukamilika kusikilizwa kwa kesi namba 5/2022, ndipo zianze kusikilizwa.