Polisi Dodoma yashikilia wawili tuhuma mauaji ya mwanafunzi

Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma (RPC), Martin Otieno

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi mkoani Dodoma, linawashikiliwa watu wawili kwa tuhuma za mauaji wa mwanafunzi wa shule ya msingi Mtumba, Farida Makuya (16).

Dodoma. Jeshi la Polisi mkoani Dodoma, linawashikiliwa watu wawili kwa tuhuma za mauaji wa mwanafunzi wa shule ya msingi Mtumba, Farida Makuya (16).

Mwanafunzi huyo aliuawa usiku wa juzi Jumanne, Oktoba 4, 2022 nyumbani kwao Mtumba jijini Dodoma na watu wasiojulika.

Inadaiwa alipigwa na kitu kizito kichwani wakati mama yake akifanya biashara katika klabu cha pombe.

Farida alitakiwa kufanya mitihani ya kumaliza elimu ya msingi iliyoanza jana na kutarajiwa kumalizika leo Alhamisi ambapo mwili wake ulizikwa jana katika makaburi ya Mtumba na kuhudhuriwa na mamia ya wakazi wa jiji la Dodoma.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma (RPC), Martin Otieno amesema hadi leo Alhamisi Oktoba 6, 2022, jeshi hilo linawashikilia watu wawili kwa mahojiano lakini msako zaidi unafanyika.

Otieno amesema tukio hilo ni baya ambalo haliwezi kuvulimika kwani kitendo kilichofanyika kwa binti huyo ni cha kinyama kinachopaswa kulaaniwa.

"Kwa sasa tumewakamata watu wawili kwa mahojiano, tunaendelea na msako mkali, kwa kitendo hiki lazima wahusika wakamatwe na watiwe mbaroni, lakini hili ni tukio baya, baya, baya sana lazima tushughulike nao," amesema Otieno.

Ilivyokuwa

Jana Jumatano, Anderson Makuya, Mjomba wa marehemu akizungumza na Mwananchi kwenye msiba huo, alisema usiku wa Oktoba 4, 2022, alipokea simu kutoka kwa ndugu zake kwamba mjomba wake  amepigwa na watu wasiojulika na amepelelekwa hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwa ajili ya kupatiwa  matibabu.

“Alipaswa kufanya mitihani yake ya darasa la saba. Marehemu kwao wamezaliwa watano na yeye ni mtoto wa pili kuzaliwa kwa dada yangu"

Alisema siku ya tukio mama wa marehemu alienda kuuza pombe za kienyeji katika klabu kilichopo katika mtaa wa Mtumba Jijini hapa.

Alisema wakati akiondoka nyumbani kwake hakurudishia mlango ili akirudi iwe rahisi kuingia ndani kwani watoto wanaweza kuwa wamelala.

Mjomba huyo alisema dada yake alirudi majira ya saa nane usiku akiwa amelewa na aliingia moja kwa moja ndani kwani mlango ulikuwa haujafungwa.

“Aliporudi majira saa nane usiku alikutana na michirizi ya damu, aliona michiriki hiyo mara baada ya kuwasha tochi ya simu, alishtuka na kuifuata  michirizi hiyo mpaka nyuma ya nyumba karibu na uwanja wa mpira.

“Akakuta damu nyingi zaidi na alimkuta marehemu akiwa ametupwa hapo huku damu nyingi zikitoka kichwani.

“Walimchukua na kumpeleka katika zahanati  lakini baadae ilibidi wampeleke  katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

“Kabla hawajafika marehemu alifariki kabla hajapewa huduma yoyote na mimi walinipigia simu  wale walioenda hospitali ndio nikawapa taarifa nyumbani.

“Inavyoonekana alipigwa na kitu kizito kwa sababu pale kuna mafiga ya kupikia yalikuwa nje, sasa jiwe moja halikuwepo lilikutwa na damu nyingi, kwa  haraka haraka unaweza ukaona jiwe lile limehusika kumpiga mjomba wangu,”alisema.

Alisema marehemu  nyumbani alikuwa amelala  na wadogo zake wanne  na wote walikuwa wamelala katika chumba kimoja lakini cha kushangaza hakuna yeyote aliyesikia tukio hilo.

“Cha kushangaza hawakujua chochote kwani hata damu ziliwarukia lakini hawakujua chochote mpaka Mama yao alipokuwa akiomba msaada ndio walipoamka hatujui labda walipuliziwa dawa,”alisema Makuya.